Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
ametembelea kiwanda cha kusindika tumbaku
cha mkoani Ruvuma na kuwasimamisha kazi
viongozi wa Chama Cha Kikuu Cha Ushirika cha SONAMCU.
Akizungumza jana jioni(Jumanne, Januari 5, 2016), katika
ukumbi wa mikutano wa Ikulu Ndogo ya Songea, wakati alipokutana na wakulima wa
zao la tumbaku wa Wilaya ya Namtumbo, Wananchama wa Vyama Vya Ushirika vya Mkoa
wa Ruvuma, viongozi wa Mkoa pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Edwin Ngonyani ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini.
Waziri Mkuu amesema, Serikali
ina dhamira ya kufufua kiwanda cha kusindika tumbaku cha SONAMCU, na lengo la
kutembelea kiwanda hicho ni katika utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe
Magufuli la kufufua viwanda nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa,
ametembelea maeneno mbalimbali ya kiwanda hicho na kukagua mitambo iliyokua
ikitumika kusindika tumbaku, kabla kiwanda hicho kuzimwa miaka kadhaa iliyopita
baada ya kukosa malighafi za kuendelea
na uzalishaji.
Pia, amemtaka Afisa Biashara
kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Bibi. Stela Lugongo kuandaa na kuwasilisha
kwake mkakati wa kufufua kiwanda hicho cha kusindika tumbaku, na baadae
kuwasimamisha kazi viongozi wote wa Chama Kikuu cha Ushirika cha SONAMCU
waliohusika na tuhuma hizo na kutaka wafikishwe Mahakamani.
“Serikali imeazimia kufufua
viwanda, hasa vile ambavyo havina wawekezaji vimebaki vyenyewe, Tunahitaji
kujua namna ya kuvifufua”. Alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa pia, amesikiliza
na kujibu kero mbalimbali za wakulima wa
tumbaku wa Mkoa huo, ambao walilalamikia mfumo wa Vyama vya Ushirika na namna ambavyo
vyama hivi vimekua vikiwaibia fedha zao
hadi kushindwa kuendelea kulima zao la tumbaku na kukosa masoko ya mazao
yao.
Aidha, Waziri Mkuu amewasihi
wakulima kuwa watulivu na kusubiri maamuzi ya Mahakama baada ya kuwa viongozi
wa Chama cha Ushirika SONAMCU ambao wamehusika na wizi wa fedha za wakulima
kiash cha Shilingi milioni 800 kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2014 tayari
wamefikishwa Mahakamani na uchunguzi unaendelea. Pia, amemwagiza Mkuu wa Mkoa
wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu kukutana na wakulima hao ili kupatia ufumbuzi
matatizo yao.
Aidha, ametoa wito kwa
wakulima kuendelea kulima zao la tumbaku kwa kuwa linaongeza pato la mtu mmoja
mmoja, linasaidia kuchangia pato la Mkoa na kukua kwa uchumi wa nchi. Amewashauri
wakulima kuunda na kuviendesha Vyama Vya
Ushirika kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Waziri Mkuu amemaliza ziara
yake mkoani Ruvuma, atafanya majumuisho ya ziara hiyo leo, kabla ya kuagana na
viongozi wa Chama na Serikali na kurejea jijini Dar es Salaam.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,11410 DAR ES SALAAM
JUMMATANO, JANUARI 6, 2016.
0 comments:
Post a Comment