Saturday, September 16, 2017

Mabasi yakamatwa usiku wa manane kwa mwendokasi

Mabasi saba ya abiria yamekamatwa  na kutozwa faini kwa kosa la mwendokasi na kutofuata sheria za usalama barabarani huku wakihatarisha maisha ya abiria.

Kamatakamata hiyo  ambayo imesimamiwa na Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani   Fotunatus  Muslim akiwa na timu ya viongozi na askari  mkoa wa Morogoro imefanyika usiku wa kuamkia leo.

Zoezi la ukamataji mabasi hayo limefanyika eneo la Dumila Wilaya ya Kilosa mkoani hapa, zoezi lilichukua takribani masaa mawili ambapo mabasi hayo yamezuiwa kuondoka mpaka asubuhi huku yakitozwa faini.

Kamanda Muslim amesema jeshi hilo halitakubali kuona maisha ya watanzania yakipotea  kutokana na uzembe wa baadhi ya madereva.

Amesema  kikosi hicho cha usalama barabarani kimeahidi kupambana na madereva wa mabasi ya abiria hasa nyakati za usiku kwani ndio wamekuwa wakiendesha kwa mwendokasi huku wakidai  serikali muda huo inakuwa imelala.

Mabasi ya abiria zaidi ya saba yanayofanya safari kati ya mkoa wa Mara (Musoma) Dar es salaam, na Mwanza- Dar es salaam yamekaguliwa na kutozwa faini.

Muslim amesema  madereva wengi wamekuwa wakifuata sheria za barabarani nyakati za mchana kwa kuhofia kukamatwa kutokana na tochi zilizopo na inapofika nyakati za usiku madereva hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuendesha kwa mwendo kasi.

 Akizungumzia dhamira ya Polisi  Muslim amesema ni kuwalinda raia na mali zao na kuwataka askari wa usalama barabarani kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

Amesema doria ni endelevu na sasa itakuwa kwa nchi nzima kwa usiku na mchana huku akiwataka madereva hao kuacha kudanganyika kwa madai kuwa tochi usiku hazifanyi kazi usiku na kwamba tochi sasa zitakamata mpaka usiku.

"Nimekuja na slogani ya Kamata hii ni kwa wale madereva wasiotii na kufuata sheria na tutapambana nao kila wakati na nyakati zote na hiyo itasaidia abiria kusafiri salama na matumizi ya barabarani kuwa bora," amesema kamanda Muslim

Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Leon Mwete aliyekuwa katika moja ya basi yaliyokamatwa eneo hilo la Dumila amesema zoezi hilo ni zuri na linafaa kuendelea.

Amesema hii itapunguza ajali za barabarani na kwamba kwa sasa uendeshaji wa madereva wengi ni mzuri ukilinganisha na zamani.

Naye kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Morogoro Boniface Mbao ameeleza kuwa yeye akiwa msimamizi mkuu ataendelea kusimamia na kufanya oparesheni za usiku na mchana kama maelekezo yaliyotolewa.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More