Wednesday, November 4, 2015

Walioihujumu CCM Wakati Wa Kampeni Kutimuliwa

WANACHAMA na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliohusika kwa namna moja ama nyingine kukihujumu chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na kukikosesha ushindi katika kata na majimbo kadhaa, wametakiwa kutafuta pa kwenda kabla ya kufukuzwa uanachama.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora Mjini, Abdulrahman Nkonkota alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa wana CCM kutoka maeneo mbalimbali ya mji huo wa kumpongeza Rais Mteule wa awamu ya tano, Dk John Magufuli kupitia chama hicho.

Alisema ili CCM iendelee kupata kibali kwa wananchi na kushika dola ipo haja ya kusafisha chama kwa kuondoa wanafiki na wasaliti walioko ndani ya chama.

Alisema hao kwa kuwa wanadumaza maendeleo ya chama pamoja na serikali huku akibainisha wazi kuwa wataanza operesheni safisha chama ili kiweze kutekeleza malengo yake yapatayo 19.

“Naunga mkono kauli ya Rais wetu Mteule Dk Magufuli ya kuwaondoa wanafiki katika chama ambao wamerudisha nyuma maendeleo ya chama chetu hali iliyowafanya baadhi yao kupoteza imani kwa chama chao”, alisema.

Awali Katibu wa CCM wilaya ya Tabora Mjini, Kameth Ndaghine alisoma tamko la wana CCM wa wilaya hiyo la kumpongeza Dk Magufuli na mgombea mwenza Samia Suluhu Hassan kwa kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu uliofanyika nchini kote Oktoba 25 mwaka huu.

Alisema wanaamini uwezo mkubwa walio nao viongozi hao utawavusha Watanzania na kuwaondoa katika dimbwi la umasikini sambamba na kuongeza ajira kwa vijana.

Aidha alimwomba Magufuli mara tu atakapoapishwa ahakikishe anaanza kutekeleza ahadi zake hasa kwa kujenga mahakama ya mafisadi na kuwachukulia hatua kali wala rushwa ambao wamelifikisha taifa pabaya.

Ndaghine alisema pamoja na kuanzisha mahakama ya mafisadi awashughulikie watumishi wa umma wanaoendekeza uzembe na wale wanaofanya kazi kwa mazoea ili kurudisha imani kwa Watanzania waliomwamini na kuiamini CCM hadi kuipa ushindi wa kishindo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More