Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imeahirisha kwa mara ya pili hafla ya vyama vya siasa kumuaga Rais Jakaya Kikwete baada ya kumaliza miaka 10 ya uongozi wake kwa mujibu wa katiba.
Hafla hiyo inayoratibiwa na Baraza la Vyama vya Siasa ilipangwa kufanyika jana baada ya Oktoba 2, mwaka huu kuahirishwa ili kutoa fursa kwa Rais Kikwete kushughulikia mvutano wa uchaguzi wa Zanzibar ulioibuka kufuatia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kufuta matokeo yote ya uchaguzi huo.
Vyama vilivyoalikwa kushiriki hafla hiyo ya kumuaga Rais Kikwete ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi ( Ukawa) vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Cuf), NLD na vyama vingine vya upinzani.
Akitangaza kuahirishwa kwa hafla hiyo kwa mara ya pili, jijini Dar es Salaam jana, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, alisema kikao hicho kimeahirishwa tena kutokana na Rais kubanwa na majukumu mengine ya kitaifa ikiwamo suala la Zanzibar.
“Tumeamua kuahirisha hadi siku tutakayotangaza tena kutokana na Rais kukabiliwa na majukumu mengine na suala la Zanzibar bado linashughulikiwa,” alisema.
Alisema akiwa msajili wa vyama vya siasa amefurahishwa na hatua ya Rais Kikwete kulishughulikia suala la Zanzibar kwa vitendo ili kuhakikisha amani inaendelea kudumishwa nchini.
0 comments:
Post a Comment