Tuesday, June 5, 2018

Chumi ashikilia shilingi kuitaka Serikali kutoa fedha za Miradi Viporo kama ilivyoahidi, Spika aokoa jahazi

Mbunge wa Mafinga Mjini Cosato Chumi ameitaka serikali kutoa fedha za miradi viporo kama ilivyoahidi kwa kuwa mwaka wa fedha unaelekea mwishoni.

Chumi alitoa hoja hiyo wakati Bunge limekaa kama Kamati kujadili bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ambapo alisema kuwa, ni Serikali yenyewe ndio ilizitaka Halmashauri kuwasilisha miradi viporo ambayo mingi ilitokana na nguvu za wananchi.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Ashantu Kijaji alisema kuwa Serikali inafanya uchambuzi wa miradi hiyo ndipo itoe fedha.

Hata hivyo, Chumi alihoji ni uchambuzi gani ikiwa miradi hiyo ilianishwa na kuchambuliwa kwa ushirikiano kati ya Halmashauri na Tamisemi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi upi huo ambao serikali inaufanya ikiwa Halmashauri kwa kushirikiana na Tamisemi walishafanya? Naomba Waheshimiwa Wabunge mniunge mkono, tujadili jambo hili

Baada ya kauli hiyo, wabunge wengi walisimama kuunga mkono hoja. 

Hata hivyo, Spika ambaye kwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti, aliitaka Serikali kuona uzito wa hoja hiyo na kwenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, jambo hili ni zito, mimi niwaombe Serikali, mlichukulie uzito unaostahili, Mheshimiwa Chumi unasemaje baada ya msisitizo huu

Akihitimisha hoja yake, Mbunge huyo wa Mafinga Mjini alisema kuwa, kwa msisitizo uliotoa Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini Serikali italifanyia kazi kwa uzito huo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti umeshasema kwa msisitizo, na wewe Mwenyekiti ndiye uliyekikalia kiti, narejesha shilingi na kuisihi Serikali itoe fedha hizo ili kuongeza morali ya wananchi kujitolea katika shughuli za maendeleo

Akizungumza na mwandishi wetu baadae, Chumi alisema kuwa katika Jimbo la Mafinga Mjini waliainisha kukamilisha miradi ya ujenzi wa kituo cha Afya Bumilayinga, kukamilisha Zahanati za Kitelewasi, Kisada, Ulole na nyumba tatu za wauguzi, na ukarabati wa madarasa katika shule ya Msingi Kikombo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More