Monday, January 23, 2017

MKUU WA WILAYA YA IRINGA AJIUNGA NA UMOJA VICOBA








MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amejiunga na Umoja Vicoba ya mjini Iringa akilenga kuutumia kuwahamasisha wananchi wa wilaya yake kujenga utamaduni wa kujiwekea akiba kwa maendeleo yao.

Umoja huo unaoundwa na wanahabari wa mjini Iringa na wadau wake wa maendeleo nchini ulianzishwa mwaka 2015 ukiwa na wanachama 20 na sasa una wanachama 40.

Mwenyekiti wa umoja huo, Frank Leonard alisema umoja huo ulianzishwa Januari 2015 baada ya wanahabari hao kuchanga fedha walizozitumia kununua vyakula na vitu mbalimbali walivyotoa msaada kwa kituo cha watoto wenye mtindio wa ubongo, Image, wilayani Kilolo.

Baada ya kutoa msaada huo Leonard alisema; “ndipo tulipokuja na wazo la kuanzisha kitu tunachoweza kukitumia kujiwekea akiba nje ya utaratibu wa kawaida wa kila mmoja wetu ili tunapohitaji mikopo kwa utaratibu rahisi tuliojiwekea iwe rahisi kuipata.”

Alisema akiba hiyo imekuwa ikiwekwa kwa utaratibu wa kununua hisa kati ya moja na 150 kwa wiki, huku hisa moja ikiuzwa kwa Sh 2,000 tu.

“Mwaka 2015 tulipoanza, tuliongeza idadi ya wanachama hadi 30 na kwa ujumla wetu tulinunua hisa zenye thamani ya Sh Milioni 45,” alisema.

Wakati wanachama wakinunua hisa zao kila wiki, wenye mahitaji ya mikopo walikuwa wakikopeshwa kwa utaratibu uliowezesha kikundi kipate  zaidi ya Sh Milioni 6 kama faida.

Leonard alisema wapoanza mwaka 2016, waligawana akiba na faida kwa kadri kwa kuzingatia idadi ya hisa zilizonunuliwa na kila mwanachama.

Mwaka 2016, alisema wanachama wa Vicoba hiyo waliongezeka hadi 35 na kwa pamoja waliweza kununua hisa zenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 75, fedha zilizowatengenezea pia faida kupitia mikopo waliyokuwa wakiitoa.

“Mipango yetu ya mwaka jana ilikuwa ni kutumia sehemu ya akiba yetu kuwekeza katika biashara za muda mfupi tukilenga kutengeneza faida zaidi. Mpango huo hakufanikiwa kwasababu mbalimbali zilizojitokea, ni matarajio yetu mwaka huu tutafanikiwa” alisema.

Alisema amevutiwa na jitihada za wanahabari hao na wadau wao jambo lililomfanya ajiunge na Vicoba yao.

“Taarifa ya miaka yenu miwili toka muanze Vicoba hii inaonesha mnafanya kwa faida na malengo yenu ni kuitumia kujikwamua zaidi kiuchumi. Natamani kuwa mmoja wenu na naomba nafasi hiyo,” alisema huku akitoa Sh 400,000 taslimu kama ada yake ya kujiunga na akinunua hisa ya wiki ya kwanza ya Januari mwaka huu.

Akiwa mwanachama wake, Kasesela aliahidi kuchangia shughuli za maendeleo za Vicoba hiyo na kutoa mawazo yake yatakayoifanya iwe imara zaidi kifedha.


“Nafahamu vipo Vicoba vingi katika wilaya yangu, vinavyofanya vizuri na vilivyoishia katika mifarakano, ombi langu kwa wananchi wa wilaya yangu, waige utaratibu wa Umoja Vicoba na vingine vinavyofanya vizuri, ili kujijenga kiuchumi,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More