Saturday, November 22, 2025

DC NYUNDO AWASIMAMISHA KAZI VIONGOZI WA KIJIJI KWA TUHUMA ZA UUZAJI ARDHI

Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amewasimamisha kazi viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Nanjirinji A, Kata ya Nanjirinji, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ugawaji na uuzaji wa ardhi kinyume cha utaratibu pamoja na matumizi mabaya ya mali za umma.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amewasimamisha kazi viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Nanjirinji A, Kata ya Nanjirinji, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ugawaji na uuzaji wa ardhi kinyume cha utaratibu pamoja na matumizi mabaya ya mali za umma.
Baadhi ya wananchi wakiwasikiliza viongozi kutoka wilaya ya Kilwa


Na Fredy Mgunda,Kilwa Lindi.


Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, amewasimamisha kazi viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Nanjirinji A, Kata ya Nanjirinji, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ugawaji na uuzaji wa ardhi kinyume cha utaratibu pamoja na matumizi mabaya ya mali za umma.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya wananchi kuwasilisha malalamiko mbele ya Mkuu wa Wilaya, wakimtuhumu Mwenyekiti Hamadi Makakala na Mtendaji Mbaruku Malukula kwa kufanya maamuzi makubwa bila kuwashirikisha wanajamii, kinyume na misingi ya utawala bora.

Akizungumza baada ya kusikiliza malalamiko hayo, DC Nyundo alisema kuwa ameunda kamati maalumu ya uchunguzi itakayopitia tuhuma hizo kwa kina na kutoa mapendekezo yatakayoiwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki.

“Hatutaacha mwanya kwa mtu yeyote kutumia madaraka vibaya au kudhulumu rasilimali za wananchi. Uchunguzi utafanyika kwa uwazi na hatua kali zitachukuliwa kulingana na matokeo,” alisema Nyundo.


Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, akiwataka kutegemea vyanzo vya uhakika ili kuepuka kupotoshwa.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Hemed Magaro, alitoa ufafanuzi kuhusu utofauti kati ya kuuza ardhi na kugawa ardhi kwa utaratibu maalumu, akisisitiza kuwa ardhi ya kijiji haiwezi kuuzwa bila kufuata sheria, taratibu na ridhaa ya mkutano mkuu wa kijiji.

Thursday, November 20, 2025

RC KHERI AWAAGIZA TFS KUONGEZA ELIMU YA UHIFADHI KWA JAMII.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi ya kulinda rasilimali za misitu na nyuki, huku akiutaka wakala huo kuongeza kasi ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto za kimazingira
Mkuu wa mkoa wa Iringa Kheri James akiwa na Mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt Linda na baadhi ya viongozi wa shamba la miti la Sao Hill mkoani humo
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri  James, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi ya kulinda rasilimali za misitu na nyuki, huku akiutaka wakala huo kuongeza kasi ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto za kimazingira
Mkuu wa mkoa wa Iringa Kheri James akiwa na Mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt Linda na baadhi ya viongozi wa shamba la miti la Sao Hill mkoani humo

Na Fredy Mgunda,Mufindi Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi ya kulinda rasilimali za misitu na nyuki, huku akiutaka wakala huo kuongeza kasi ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto za kimazingira zinazoongezeka nchini.


Ametoa wito huo wakati wa ziara yake katika Shamba la Miti Sao Hill, wilayani Mufindi, akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo.


Akizungumza na wahifadhi, Mkuu wa Mkoa amesema nidhamu na weledi ndani ya TFS ni sharti kuzingatiwa ili kuhakikisha sera na taratibu za uhifadhi zinatekelezwa kikamilifu.


“Nidhamu ni msingi wa ufanisi. Kama wahifadhi wa misitu yetu, ni lazima mjikite kwenye uwajibikaji na kutanguliza maslahi ya Taifa,” amesema James.


Amesifu uhusiano mzuri baina ya TFS na wananchi wanaoishi pembezoni mwa shamba hilo, akisema ushirikiano huo unaimarisha ulinzi wa misitu na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali hizo.


“Kulinda misitu ni jukumu la Taifa zima. Endeleeni kutoa elimu mara kwa mara ili jamii ielewe kuwa misitu ni uchumi, ni mazingira, na ni uhai,” amesema.


Mhe. James ametahadharisha kuwa ukame unaoikumba nchi katika miaka ya hivi karibuni unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa misitu, hali inayosababisha kupungua kwa mvua na kuongezeka kwa joto.


“Ukame unaongezeka kwa sababu tumeshindwa kuhifadhi misitu. TFS iendelee kuhamasisha upandaji na utunzaji wa miti bila kuchoka,” amesisitiza.


Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, amesema Shamba la Miti Sao Hill limekuwa msaada mkubwa kwa jamii kwa kushiriki miradi mbalimbali ya maendeleo.


“TFS imetoa madawati, kujenga madarasa, mabweni, bwalo la chakula na kuendelea kusaidia jamii kwenye miradi ya kijamii. Ni taasisi inayowajibika,” amesema.


Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, amesema TFS imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kuhakikisha misitu inatumika kwa manufaa bila kuhatarisha uendelevu.


Ametaja shughuli zinazotekelezwa kuwa ni pamoja na ufugaji nyuki, uvunaji wa utomvu, uvunaji endelevu wa miti, na utoaji wa elimu kwa wananchi wa maeneo jirani.

Friday, October 24, 2025

OSHA YADHAMIRIA KUONGEZA UELEWA WA WADAU KUPITIA VYAMA VYA WAFANYAKAZI

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya kuhitimisha kikao kazi cha siku mbili cha viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Kibaha Mkoani Pwani.
Mwenyekiti na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam (Brendan Maro na Sara Rwezaula-Kulia) wakimpokea Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alipowasili Kibaha, Pwani kwa ajili ya kufunga kikao kazi cha Viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la OSHA, Bi. Beatrice Lengereri.
Mkufunzi wa OSHA, Bw. Simon Lwaho, akiwasilisha mada kuhusiana na masuala ya usalama na afya kazini katika kikao kazi cha viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani
Viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia mada mbalimbali kuhusiana na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi katika kikao kazi chao kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wenyeviti na makatibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kuhitimisha kikao kazi chao kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani
Na Fredy Mgunda.

Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wa Mkoa wa Dar es Salaam wapatao 180 wamepatiwa mafunzo ya awali ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwawezesha kuzishauri menejementi za Taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi na hivyo kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Mafunzo hayo yaliyowahusisha wenyeviti na makatibu wa matawi yote 90 ya TUGHE ya Mkoa wa Dar es Salaam, yamefanyika katika kikao kazi cha siku mbili Kibaha Mkoani Pwani ambapo viongozi wapatao 180 wameshiriki.

Pamoja na masuala mengine, mada mbalimbali zinazolenga kujenga uelewa wa jumla kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi zimewasilishwa na wataalam wa OSHA. Mada hizo ni pamoja na; Dhana ya Usalama na Afya mahali pa kazi, Uwakilishi na Kamati za Afya na Usalama mahali pa kazi, Mifumo ya Usalama na Afya mahali pa kazi pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi.

Wawasilishaji wa mada kutoka OSHA, Bw. Simon Lwaho na Moteswa Meda wamesisitiza washiriki kuwahamasisha wafanyakazi wenzao katika sehemu za kazi kujifunza kanuni bora za usalama na afya kutegemeana na shughuli zao za kila siku ili kupata mbinu za kujilinda dhidi ya vihatarishi mbalimbali vya magonjwa na ajali mahali pa kazi.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha kikao kazi cha viongozi hao, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, aliyekuwa Mgeni Rasmi wa hafla ya kufunga kikao kazi hicho, amesema viongozi hao wanayo nafasi muhimu katika kushawaishi menejimenti za Taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi ili kuleta ustawi wa wafanyakazi. 

“Kupitia kikao kazi hiki tumewaeleza wenzetu wa TUGHE jitihada za serikali katika kuimarisha afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi ambapo mbali na kuiwezesha OSHA kusimamia uzingatiaji wa taratibu za usalama na afya, masuala haya yamejumuishwa katika kanuni za kudumu za utumishi wa umma. Aidha, uzingatiaji wa masuala ya usalama na afya unaangaliwa katika ukaguzi wa CAG pamoja na Tume ya Utumishi wa Umma,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA. 

Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA nchini, Bi. Mwenda, ameahidi kuendelea kushirikiana na TUGHE pamoja na vyama vingine vya wafanyakazi katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi nchini wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na kanuni bora za usalama na afya zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao ya msingi katika hali ya ya usalama na kubakia na afya njema.
Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Komredi Brendan Maro ameielezea OSHA kama mdau muhimu katika utekelezaji majukumu ya chama chao.
 
“Tunawashukuru sana OSHA kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitupatia katika utekelezaji wa majukumu yetu hususan suala la kutoa elimu kwa wanachama wetu ambao ni wafanyakazi,” amesema Komredi Maro. 

Akitoa neno la shukrani, mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Norbetha Sanga ambaye ni Katibu wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) amesema mafunzo ya usalama na afya ni muhimu kwa wafanyakazi na waajiri ili kuwa na uzalishaji wenye tija.



Tuesday, October 7, 2025

SERIKALI YAENDELEA KUWAUNGA MKONO WAKULIMA WA PAMBA KASULU

 Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu Serikali inaendelea kuleta unafuu kwa wakulima wa zao la pamba wilayani Kasulu kwa kuwapatia pembejeo muhimu kama mbegu, viuatilifu na vinyunyizi, hatua iliyochochea kilimo chenye tija na matokeo chanya.

Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Theresia Mtewele, amesema maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyoanzishwa mwaka 2019 yanalenga kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa zao hilo kama chanzo kikuu cha kipato kwa wakulima wadogo na wafugaji vijijini
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu Serikali inaendelea kuleta unafuu kwa wakulima wa zao la pamba wilayani Kasulu kwa kuwapatia pembejeo muhimu kama mbegu, viuatilifu na vinyunyizi, hatua iliyochochea kilimo chenye tija na matokeo chanya.


Na Fredy Mgunda 


Serikali imeendelea kuleta unafuu kwa wakulima wa zao la pamba wilayani Kasulu kwa kuwapatia pembejeo muhimu kama mbegu, viuatilifu na vinyunyizi, hatua iliyochochea kilimo chenye tija na matokeo chanya.


Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amesema hayo leo Jumanne, Oktoba 7, 2025, katika Kata ya Asante Nyerere, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyokwenda sambamba na uzinduzi wa msimu mpya wa zao hilo kwa mwaka 2025/2026.


Amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa Serikali, wanunuzi na vyama vya msingi kujadili maendeleo ya zao hilo na kuweka mikakati ya kuliboresha zaidi.


 Aidha, amewataka wananchi kutumia kipindi hiki cha kampeni kusikiliza sera za wagombea wa vyama mbalimbali ili siku ya uchaguzi, Oktoba 29, watumie haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Theresia Mtewele, amesema maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyoanzishwa mwaka 2019 yanalenga kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa zao hilo kama chanzo kikuu cha kipato kwa wakulima wadogo na wafugaji vijijini.


Mkulima wa Pamba, Joel Kingi, ameishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuhamasisha kilimo hicho, akieleza kuwa idadi ya wakulima imeongezeka kutoka 50 hadi kufikia 1,000 kutokana na upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu.


Awali, Mkaguzi wa Pamba wa Wilaya hiyo, Michael Kiliga, amesema wilaya inashirikiana na vyama vya ushirika (AMCOS) nane kusambaza pembejeo kwa wakulima bure, hatua inayochangia kuimarisha uzalishaji wa zao hilo.

CCM WAFANYA BONANZA KUHAMASISHA WANANCHI KUSHIRIKI UCHAGUZI KWA AMANI

 
Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda,mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Richard Kasesela kwa pamoja walihimiza kufanya mazoezi kila siku na kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu 
Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda,mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Richard Kasesela kwa pamoja walihimiza kufanya mazoezi kila siku na kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu 

Na Fredy Mgunda.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeandaa Bonanza Maalum katika Jimbo la Segerea, mkoani Dar es Salaam, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, kwa njia ya amani na utulivu.


Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda, ambaye aliwataka wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kupiga kura kwa amani, akisisitiza kuwa kiongozi anayechaguliwa leo ndiye atakayekuwa na mamlaka ya kuleta maendeleo kwa miaka mitano ijayo.


“Kupiga kura ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania. Tuchague viongozi wanaotuletea maendeleo ya kweli,” alisema Chatanda.


Akimnadi mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Chatanda alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imeitekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa asilimia 100, na hivyo anastahili kupewa tena ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.


Aidha, alitoa wito kwa wananchi kumchagua mgombea wa CCM katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani ili kuimarisha juhudi za maendeleo nchini.


Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, alisisitiza kuwa mojawapo ya sera zake ni kuhamasisha mazoezi ya mara kwa mara kwa wananchi, ili kuboresha afya ya mwili na akili.


“Afya bora ni msingi wa maendeleo. Tukifanya mazoezi tutakuwa na nguvu za kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa,” alisema Kamoli.


Kamoli aliwaomba wakazi wa Segerea kumpigia kura nyingi pamoja na kumpa kura ya kishindo Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika jimbo hilo.


Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kasesela, aliwataka wananchi kupuuza wanasiasa na wanaharakati wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea vurugu na hofu wakati huu wa uchaguzi.


“Wachochezi wengi wapo nje ya nchi. Vurugu zikitokea, ni Watanzania waliopo hapa ambao watateseka. Amani ni tunu ya taifa letu,tuilinde,” aliongeza Kasesela.


Katika bonanza hilo, wananchi walishiriki katika michezo mbalimbali, burudani, na kupata elimu juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa njia ya amani.

Sunday, October 5, 2025

MNEC KASESELA AWASIHI WATANZANIA KUSOMA VITABU VYA DINI

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Dar es Salaam, Richard Kasesela, amewataka Watanzania kumuabudu Mwenyezi Mungu kila wakati ili waweze kupata amani ya moyo na nafsi.
Baadhi ya waumini wa dini ya wananchi waliohudhuria kongamano la waislamu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu lilofanyika mlimani city jijini Dar es salaamBaadhi ya waumini wa dini ya wananchi waliohudhuria kongamano la waislamu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu lilofanyika mlimani city jijini Dar es salaam


Na Fredy Mgunda 

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Dar es Salaam, Richard Kasesela, amewataka Watanzania kumuabudu Mwenyezi Mungu kila wakati ili waweze kupata amani ya moyo na nafsi.


Akizungumza katika kongamano la Waislamu kuelekea uchaguzi mkuu, Kasesela alisema ni muhimu kwa wananchi kusoma vitabu vya dini mara kwa mara, kwani vinafundisha maadili mema na kuleta baraka katika kazi zao za kila siku.


"Vitabu vya dini vinatufundisha subira, heshima na upendo – misingi ambayo ni muhimu katika maisha na maendeleo ya taifa," alisema Kasesela.


Aidha, aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu ya kiroho sambamba na mafunzo ya mbinu za kujikwamua kiuchumi, ili wananchi waweze kujitegemea na kuboresha maisha yao.


Katika hatua nyingine, Kasesela aliwahimiza wananchi wote kumpigia kura kwa wingi Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa amefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika kipindi chake cha uongozi.


"Ni wajibu wetu kuonyesha shukrani kwa kumpigia kura Dkt. Samia tarehe 29 Oktoba. Tuonyeshe mshikamano wetu kwa kupitia sanduku la kura," alihitimisha Kasesela.

Tuesday, September 30, 2025

VIONGOZI, WANANCHI WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUDHIBITI MOTO MISITUNI

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Reuben Chongolo, ametoa wito kwa viongozi na wananchi kushirikiana kwa dhati katika kudhibiti matukio ya moto misituni, akisisitiza kuwa misitu ndiyo uti wa mgongo wa uchumi na ustawi wa jamii.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, amesema kubwa TFS imekuwa ikitoa elimu kila mwaka kwa vijiji 60 vinavyozunguka shamba hilo juu ya matumizi sahihi ya moto na aliwataka wananchi kutoa taarifa za mapema pale wanapoona viashiria vya moto, ili kuepusha madhara makubwa.
Baadhi ya washiriki kikao hicho cha kuzibiti na kupambana na moto katika shamba la miti Zao Hill na maeneo mengine 
Baadhi ya washiriki kikao hicho cha kuzibiti na kupambana na moto katika shamba la miti Zao Hill na maeneo mengine 


Na Fredy Mgunda,Mufindi Iringa.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi, Reuben Chongolo, ametoa wito kwa viongozi na wananchi kushirikiana kwa dhati katika kudhibiti matukio ya moto misituni, akisisitiza kuwa misitu ndiyo uti wa mgongo wa uchumi na ustawi wa jamii.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Dkt. Linda Salekwa, katika kikao kilichofanyika leo kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Chongolo alisema moto umekuwa ukileta madhara makubwa kwenye mashamba ya miti ya wananchi na yale yanayosimamiwa na Serikali, ikiwemo Shamba la Miti Sao Hill.

“Nchi yetu hasa maeneo yenye misitu tumekua tukipata changamoto kubwa za moto. Lakini kutokana na mikakati ya TFS, tumekuwa na kamati za vijiji zinazoratibu matumizi ya moto, jambo ambalo limeleta manufaa makubwa,” alisema Chongolo.

Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya TFS na wananchi ndio silaha pekee ya kuhakikisha misitu inabaki salama na kuendelea kuchangia mapato ya taifa. Pia aliwataka viongozi wa vijiji na kata kuwapa wananchi elimu endelevu kuhusu matumizi salama ya moto hasa kipindi cha kiangazi.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, alisema TFS imekuwa ikitoa elimu kila mwaka kwa vijiji 60 vinavyozunguka shamba hilo juu ya matumizi sahihi ya moto. Aliwataka wananchi kutoa taarifa za mapema pale wanapoona viashiria vya moto, ili kuepusha madhara makubwa.

Viongozi waliohudhuria kikao hicho waliipongeza TFS kwa jitihada hizo na kuahidi kuendelea kushirikiana katika kutoa elimu na kusimamia uhifadhi wa misitu.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, maafisa tarafa, watendaji wa kata na vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji.

Sunday, September 28, 2025

ELIMU YA USALAMA NA AFYA KAZINI YAWAFIKIA WASIOONA.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda, akihitimisha mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa watu wasioona ambao ni wanachama wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB) wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Mafunzo hayo yamefanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu Wa OSHA Bi. Khadija Mwenda akikambidhi Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona, Bw. Omary Itambu vifaa saidizi vikiwemo vitabu vya usalama na afya vyenye maandishi ya nukta nundu, karatasi maalum za nukta nundu pamoja na fimbo nyeupe kwa ajli ya wanachama wake
Mkufunzi wa Huduma ya Kwanza wa OSHA, Bi. Moteswa Meda akiwasilisha mada kuhusu Misingi ya Huduma ya Kwanza mahali pa kazi kwa wanachama wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB) katika semina ya mafunzo iliyoandaliwa na OSHA kwa kundi hilo.
Washiriki wa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi ambao ni wanachama wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania, wakifuatilia mada mbalimbali katika semina iliyoandaliwa na OSHA kwa ajili ya kundi hilo la watu wenye ulemavu.  
Afisa Mafunzo wa OSHA, Bw. Simon Lwaho, akiwasilisha mada kuhusu vihatarishi mahali pa kazi na udhibiti wake kwa wanachama wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB) katika semina ya mafunzo iliyoandaliwa na OSHA kwa kundi hilo.

Na Fredy Mgunda.


Watu wasioona kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wamenufaika na mafunzo yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kuwawezesha kushiriki shughuli za uzalishaji kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kazini.

Mafunzo hayo ya siku moja ambayo yametolewa kwa wanachama 50 wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB) yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo utambuzi na udhibiti wa vihatarishi vya usalama na afya pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi. Washiriki wa mafunzo hayo wanajihusisha na shughuli mbalimbali zikiwemo ushonaji, kilimo, ufugaji, uzalishaji wa bidhaa zikiwemo sabuni na biashara ndogondogo.

Akifungua mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema Taasisi anayoiongoza inatambua thamani na mchango wa watu wenye ulemavu katika kujenga uchumi wa Taifa jambo ambalo limepelekea mafunzo hayo kuandaliwa pamoja na mafunzo mengine ambayo OSHA imekuwa ikayatoa kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu.

“Niwapongeze washiriki wote wa mafunzo kwa kuitikia mwaliko wa kushiriki mafunzo haya muhimu kwenu kwani ni dhahiri kuwa ulemavu ni hali tu ambayo haipaswi kuwa kikwazo kwenu kushiriki katika shughuli za kiuchumi,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza"Alisema Ni Mwenda

Bi Mwenda alisema kuwa watawapatia vifaa saidizi zikiwemo fimbo nyeupe, karatasi za nukta nundu pamoja na vitabu maalum vya nukta nundu vyenye maudhui ya mafunzo ya usalama na afya kwa ajili ya rejea zaidi.

Aidha, Bi. Mwenda ameahidi kuwa mafunzo ya usalama na afya kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu yatafuatiwa na zoezi la kutembelea maeneo yao ya kazi kwa ajili ya kutathmini mazingira ya kazi ili kushauri namna sahihi ya kuboresha mazingira hayo. 

Awali, akiwasilisha salamu za Jumuiya ya Wasiiona Tanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Bw. Omary Itambu, ameipongeza OSHA kwakuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha watu wasioona pamoja na makundi mengine ya watu wenye ulemavu.

“Tunaiomba OSHA kuendeleza utamaduni huu wa kutujali watu wenye ulemavu. Kwa niaba ya washiriki wenzangu niwahakikishie OSHA kuwa mafunzo mliyotupatia si tu yatakwenda kuimarisha afya na usalama wetu bali yatatusaidia sana kuongeza thamani ya huduma na bidhaa tunazozalisha,” amesema Itambu.

Itambu ametoa wito kwa washiriki wenzake wa mafunzo kuwa mabalozi wazuri wa OSHA ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wenzao ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wengine wa mafunzo, Mratibu wa Idara ya Vijana wa Jumuiya ya Wasioona, Bw. Bakari Hassan, amesema jambo lililofanywa na OSHA ni la kuigwa na Taasisi nyingine za kiserikali na zisizo za kiserikali, akisisitiza kwamba mafunzo hayo na vifaa saidizi walivyopewa vitarahisisha utendaji na kuongeza tija katika shughuli zao za kila siku. 

Friday, September 19, 2025

OSHA YAKABIDHI VIFAA CHUO CHA UFUNDI MIRONGO JIJINI MWANZA

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi, akiwasilisha hotuba yake wakati wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR BONANZA 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo Jijini Mwanza akiwa ni Mgeni Rasmi wa Bonanza hilo. Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda wakimkabidhi Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mirongo vifaa mbalimbali vya msaada vilivyotolewa na OSHA kukiwezesha chuo hicho. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, makoti ya usalama na vifaa vya michezo. 

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda wakimkabidhi Mkuu wa Chuo cha Ufundi cha Mirongo vifaa mbalimbali vya msaada vilivyotolewa na OSHA kukiwezesha chuo hicho. Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, makoti ya usalama na vifaa vya michezo.
Mwenyekiti wa timu ya OSHA Iliyoshiriki SHIMIWI mwaka 2025 Ndugu Charles Mhilu akimkabidhi kikombe  Mtendaji Mkuu wa OSHA Bi Khadija Mwenda, mara timu hiyo ya OSHA kuibuka timu Bora yenye nidhamu miongoni mwa timu 50 shindani kwenye mashindano yailyoshirikisha zaidi ya timu 50 toka taasisi,wakala za Serikali na Timu toka RAS mashindano yaliyofanyika hivi karibuni jijini Mwanza.

Na  Fredy Mgunda,Kwanza.


Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mheshimiwa Amina Makilagi, amewataka waajiri na wafanyakazi kote nchini kuitekeleza kikamilifu Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Na. 5 ya mwaka 2003 ili kupunguza au kuondoa kabisa ajali na magonjwa yanayotokana na mazingira duni ya kazi.


Mheshimiwa Makilagi alitoa wito huo jana wakati wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2025) lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nyakabungo, Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza. Bonanza hilo lilihusisha shughuli mbalimbali za kijamii na michezo kwa lengo la kuimarisha mshikamano kati ya OSHA na jamii inayohudumiwa, pamoja na kutoa msaada kwa wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Mirongo, wakiwemo wenye ulemavu.


Katika tukio hilo, OSHA ilikabidhi vifaa mbalimbali kwa Chuo cha Ufundi Mirongo, vikiwemo kompyuta, vifaa kinga vya usalama kazini, pamoja na vifaa vya michezo kama mipira na jezi za michezo.


Akizungumza kama Mgeni Rasmi, Mheshimiwa Makilagi aliipongeza OSHA kwa juhudi zake za kuhakikisha mazingira salama na yenye afya sehemu za kazi na kuonesha moyo wa huruma kwa makundi maalum katika jamii.


“Nitoe rai kwa waajiri na wafanyakazi nchini kuisoma na kuitekeleza Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Sheria hii ikitekelezwa ipasavyo, maeneo ya kazi yatakuwa salama, bila ajali wala magonjwa, hivyo kuongeza tija kazini,” alisema Mkuu wa Wilaya Makilagi.


Aidha, aliihakikishia OSHA ushirikiano wa Halmashauri na Ofisi yake katika kusimamia usajili na ukaguzi wa maeneo ya kazi, sambamba na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya maboresho ya mazingira ya kazi.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, alisema Bonanza hilo ni sehemu ya mpango wa taasisi hiyo wa kurudisha kwa jamii (Corporate Social Responsibility) na kwamba msaada uliotolewa kwa Chuo cha Mirongo umetokana na tathmini iliyofanywa na wataalam wa OSHA baada ya kutembelea chuo hicho.


“Tunaamini kuwa kwa kusaidia vyuo vya ufundi kama Mirongo, tunachangia kwa kiasi kikubwa maandalizi ya wataalamu wa baadaye katika fani muhimu za kiufundi na kazi,” alisema Bi. Mwenda.


Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mirongo, Bi. Herieth Richard, pamoja na mwanafunzi wa fani ya ushonaji, Bi. Aneth Augustino, waliishukuru OSHA kwa msaada huo ambao wamesema umeongeza ari ya kujifunza na kushiriki katika shughuli za kijamii.


Bonanza hilo lilihusisha michezo ya mpira wa miguu, mpira wa pete, riadha, na michezo ya jadi kama kukimbia kwenye magunia, kukimbia na ndimu kwenye kijiko, rede na kukamata kuku. Washiriki walitoka OSHA na vyuo vya Ufundi vya Mirongo, Nyakato na Kisesa.


Chuo cha Ufundi Mirongo kinamilikiwa na Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), na hutoa mafunzo ya umeme, useremala, ushonaji na uchomeleaji kwa vijana wakiwemo wenye mahitaji maalum.

Thursday, September 18, 2025

MWENGE WA UHURU WAWEKA JIWE LA MSINGI WODI YA MAMA NA MTOTO MWAMI NTALE

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha Mwami N’tale, kilichopo kata ya Heru, Halmashauri ya Mji Kasulu.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha Mwami N’tale, kilichopo kata ya Heru, Halmashauri ya Mji Kasulu.

Na Fredy Mgunda,Kasulu, Kigoma.

 Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ali Ussi, ameweka jiwe la msingi katika wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya cha Mwami N’tale, kilichopo kata ya Heru, Halmashauri ya Mji Kasulu.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Ussi amesisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao kwa amani, utulivu, na kuchagua viongozi wanaowataka. Amesema kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu inahimiza amani kama msingi wa maendeleo ya taifa.

“Maendeleo tunayoyaona leo ni matokeo ya utulivu na amani inayotamalaki nchini. Hivyo ni wajibu wetu kuilinda na kuithamini hali hii,” alisema Ussi.

Mradi wa ujenzi wa kituo hicho umegharimu kiasi cha Tsh milioni 300, na tayari umekamilika kwa asilimia 100. Utaanza kutoa huduma za afya kwa kina mama na watoto katika eneo la Heru na maeneo jirani.

Kituo hiki kinatarajiwa kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya mama na mtoto kwa kutoa huduma bora, za karibu, na za uhakika kwa wananchi.

Mwenge wa Uhuru umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuhamasisha maendeleo, uwajibikaji, na uzalendo miongoni mwa Watanzania.

Wednesday, September 17, 2025

MWENGE WA UHURU WAZINDUA KITUO CHA POLISI NYAKITONTO KWA AJILI YA KUONGEZA USALAMA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Alli Issu, amesema uwepo wa miradi mingi yenye thamani kubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ni kielelezo tosha kwamba usalama kwa sasa si hiari tena bali ni sharti la lazima katika kuendeleza maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amesema kwa kuwa halmashauri hiyo ni mpya, suala la maendeleo linaendana moja kwa moja na uwepo wa ulinzi na usalama wa uhakika.
Kituo cha Polisi Nyakitonto chenye hadhi ya Daraja B kimezinduliwa na mbio za Mwenge wa uhuru 
Kituo cha Polisi Nyakitonto chenye hadhi ya Daraja B kimezinduliwa na mbio za Mwenge wa uhuru 


Na Fredy Mgunda,Kasulu Kigoma.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Alli Issu, amesema uwepo wa miradi mingi yenye thamani kubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu ni kielelezo tosha kwamba usalama kwa sasa si hiari tena bali ni sharti la lazima katika kuendeleza maendeleo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kituo cha Polisi Nyakitonto chenye hadhi ya Daraja B, Issu amesisitiza kuwa mara nyingi panapojengwa vituo vya polisi vya kisasa, basi tambua eneo hilo limepiga hatua kubwa za maendeleo.

“Mkuu wa Wilaya amesema tumejenga kituo hiki kwa sababu uhitaji wake umekuwa mkubwa. Ninyi wenyewe ni mashahidi, miradi yenye thamani kubwa iliyopo hapa Kasulu ndiyo kielelezo cha kasi ya maendeleo,” amesema Issu.

Ameongeza kuwa kutokana na hatua kubwa zilizopigwa, ana uhakika si muda mrefu Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu itapanda hadhi na kuwa Manispaa.Amewataka wananchi kushirikiana katika kulinda amani na usalama ili matarajio hayo yaweze kutimia kwa haraka.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amesema kwa kuwa halmashauri hiyo ni mpya, suala la maendeleo linaendana moja kwa moja na uwepo wa ulinzi na usalama wa uhakika.

Kituo hicho cha Polisi Nyakitonto kimejengwa kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri kwa gharama ya shilingi milioni 114 kikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha usalama, amani na utawala wa sheria vinadumu katika wilaya hiyo.

Tuesday, September 16, 2025

TRA NACHINGWEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAJASIRIAMALI WADOGO

Meneja wa TRA wilaya ya Nachingwea, Novatus Chamu akielezea namna dawati hilo litakavyo kuwa chombo muhimu cha kusikiliza kero, kutoa elimu ya kodi na ushauri wa kukuza mitaji kwa wajasiriamali wadogo.
Meneja wa TRA wilaya ya Nachingwea, Novatus Chamu akiwa kwenye picha pamoja na mgeni rasmi Stella kategile na baadhi ya watumishi wa TRA Nachingwea 
Mgeni rasmi Stella kategile akikataa utepe kuzindua rasmi dawati la TRA kwa ajili ya kusikiliza,kutoa huduma na elimu kwa wajasiriamali wadogo wadogo wa wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Meneja wa TRA wilaya ya Nachingwea, Novatus Chamu akiwa kwenye picha pamoja na mgeni rasmi Stella kategile na baadhi ya wajasiriamali wadogo wadogo wa wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.


Na Fredy Mgunda, Nachingwea Lindi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani Nachingwea imezindua rasmi dawati maalum la kushughulikia changamoto za wajasiriamali wadogo, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha kiuchumi na kuwainua kutoka ngazi ya chini ya biashara hadi kuwa wafanyabiashara wakubwa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa TRA wilaya ya Nachingwea, Novatus Chamu, alisema kuwa dawati hilo litakuwa chombo muhimu cha kusikiliza kero, kutoa elimu ya kodi, na ushauri wa kukuza mitaji kwa wajasiriamali wadogo.

“Kupitia dawati hili, tutaweza kusikiliza kero zao moja kwa moja, kuwapa elimu ya kodi na pia kuwashauri namna ya kukuza mitaji yao ili waweze kuchangia pato la taifa kwa ufanisi zaidi,” alisema Chamu.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kusogeza huduma karibu na wananchi, hasa wale waliopo kwenye sekta isiyo rasmi ambao mara nyingi hukumbwa na changamoto ya uelewa mdogo kuhusu masuala ya kodi na taratibu za biashara.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Stella Kategile, alieleza kuwa dawati hilo ni jukwaa muhimu la kukuza uchumi wa wafanyabiashara wadogo. Alisisitiza kuwa serikali inalenga kuwawezesha wajasiriamali kupitia utatuzi wa changamoto zao badala ya kuwabana kwa kodi bila kuelewa hali zao halisi.

“Lengo la serikali siyo kukusanya kodi tu, bali pia kusikiliza na kutatua changamoto za wajasiriamali ili waweze kukua na kuchangia kikamilifu katika pato la taifa,” alisema Kategile.

Baadhi ya wajasiriamali waliopata fursa ya kuzungumza walipongeza hatua hiyo ya TRA, wakisema kuwa imekuja kwa wakati muafaka kwani changamoto nyingi zimekuwa zikiwakwamisha katika kuendeleza biashara zao.

“Kwa muda mrefu tumekuwa hatuna pa kupaza sauti zetu. Kupitia dawati hili, tuna matumaini kuwa sauti zetu zitasikika na biashara zetu zitakua,” alisema mmoja wa wajasiriamali hao.

Dawati hilo linatarajiwa kuwa kiunganishi muhimu kati ya TRA na wajasiriamali, na mchango wake unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika muktadha wa ukusanyaji wa mapato na ukuaji wa sekta ya biashara nchini.


Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More