Sunday, December 21, 2025

OSHA YATAJWA KUWA NA NAFASI MUHIMU KATIKA KUWEZESHA SHUGHULI ZA UZALISHAJI – KATIBU MKUU

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akitoa maelezo ya awali katika ufunguzi waKikao cha Tano cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa OSHA Kilichofanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dododma Desemba 20,2025.Wajumbe wa Baraza la OSHA wakiimba wimbo wa mshikamano (solidarity) wakati wa kikao cha Tano cha Baraza la Tano la wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma Desemba, 20, 2025

Wajumbe wa Baraza la OSHA wakifuatilia majadiliano mbalimbali yaliowasilishwa katika kikaocha Tano cha Baraza la Tano la wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma.Desemba, 20, 2025.


Na Fredy Mgunda 

Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Bi. Mary Maganga, amesema Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni taasisi yenye umuhimu mkubwa katika kuwezesha shughuli za uzalishaji kufanyika kwa tija na ufanisi.

Bi. Maganga ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikao cha Tano cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika leo, Desemba 20, 2025, jijini Dodoma, ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Amesema OSHA ina jukumu muhimu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, huku akiipongeza taasisi hiyo kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, amewasisitiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia kanuni za utumishi wa umma na kuimarisha ushirikiano kazini.

“Kabla ya kufungua rasmi kikao hiki, napenda kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa weledi. Mara nyingi tumekuwa tukiamini kuwa wito unawahusu zaidi viongozi wa dini, lakini hata kazi zetu hizi ni wito, kwani kuna wananchi wengi wanaotegemea huduma zetu,” amesema Bi. Maganga.

Awali, akimkaribisha Katibu Mkuu kufungua kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema kikao hicho kinalenga kutathmini utendaji wa taasisi kwa kipindi kilichopita na cha sasa, pamoja na kuweka mwelekeo wa maendeleo ya OSHA kwa kipindi kijacho.

Amesema kikao hicho kinatazama utekelezaji wa shughuli za mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na tathmini ya utendaji katika miezi mitano ya mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Bi. Mwenda ameongeza kuwa kikao hicho kilitanguliwa na mafunzo kwa watumishi wote wa OSHA yaliyohusu maadili ya utumishi wa umma, mpango mkakati wa taasisi wa miaka mitano ijayo (2026/2027–2030/2031), masuala ya afya ya akili na itifaki.

Kwa upande wake, akitoa salamu za wafanyakazi, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Bw. Rugemalila Rutatina, ameipongeza OSHA kwa kuzingatia ushirikishwaji wa watumishi wote bila ubaguzi katika kufanya maamuzi yanayohusu utendaji wa taasisi hiyo.


0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More