Thursday, November 20, 2025

RC KHERI AWAAGIZA TFS KUONGEZA ELIMU YA UHIFADHI KWA JAMII.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi ya kulinda rasilimali za misitu na nyuki, huku akiutaka wakala huo kuongeza kasi ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto za kimazingira
Mkuu wa mkoa wa Iringa Kheri James akiwa na Mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt Linda na baadhi ya viongozi wa shamba la miti la Sao Hill mkoani humo
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri  James, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi ya kulinda rasilimali za misitu na nyuki, huku akiutaka wakala huo kuongeza kasi ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto za kimazingira
Mkuu wa mkoa wa Iringa Kheri James akiwa na Mkuu wa wilaya ya Mufindi Dkt Linda na baadhi ya viongozi wa shamba la miti la Sao Hill mkoani humo

Na Fredy Mgunda,Mufindi Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameipongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kazi ya kulinda rasilimali za misitu na nyuki, huku akiutaka wakala huo kuongeza kasi ya kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi ili kukabiliana na changamoto za kimazingira zinazoongezeka nchini.


Ametoa wito huo wakati wa ziara yake katika Shamba la Miti Sao Hill, wilayani Mufindi, akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo.


Akizungumza na wahifadhi, Mkuu wa Mkoa amesema nidhamu na weledi ndani ya TFS ni sharti kuzingatiwa ili kuhakikisha sera na taratibu za uhifadhi zinatekelezwa kikamilifu.


“Nidhamu ni msingi wa ufanisi. Kama wahifadhi wa misitu yetu, ni lazima mjikite kwenye uwajibikaji na kutanguliza maslahi ya Taifa,” amesema James.


Amesifu uhusiano mzuri baina ya TFS na wananchi wanaoishi pembezoni mwa shamba hilo, akisema ushirikiano huo unaimarisha ulinzi wa misitu na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa rasilimali hizo.


“Kulinda misitu ni jukumu la Taifa zima. Endeleeni kutoa elimu mara kwa mara ili jamii ielewe kuwa misitu ni uchumi, ni mazingira, na ni uhai,” amesema.


Mhe. James ametahadharisha kuwa ukame unaoikumba nchi katika miaka ya hivi karibuni unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa misitu, hali inayosababisha kupungua kwa mvua na kuongezeka kwa joto.


“Ukame unaongezeka kwa sababu tumeshindwa kuhifadhi misitu. TFS iendelee kuhamasisha upandaji na utunzaji wa miti bila kuchoka,” amesisitiza.


Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, amesema Shamba la Miti Sao Hill limekuwa msaada mkubwa kwa jamii kwa kushiriki miradi mbalimbali ya maendeleo.


“TFS imetoa madawati, kujenga madarasa, mabweni, bwalo la chakula na kuendelea kusaidia jamii kwenye miradi ya kijamii. Ni taasisi inayowajibika,” amesema.


Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, amesema TFS imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kuhakikisha misitu inatumika kwa manufaa bila kuhatarisha uendelevu.


Ametaja shughuli zinazotekelezwa kuwa ni pamoja na ufugaji nyuki, uvunaji wa utomvu, uvunaji endelevu wa miti, na utoaji wa elimu kwa wananchi wa maeneo jirani.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More