Na Fredy Mgunda.
Afisa Tarafa ya Katerero, Bwanku M. Bwanku, ameshauri Meli mpya ya MV Mwanza kupitishwa katika Bandari ya Kemondo na nauli zake kupunguzwa ili wananchi wengi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania.
Bwanku alitoa ushauri huo umetolewa wakati wa kikao cha wadau wa bandari za Kagera kilichowakutanisha Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri wa majini.
Kikao hicho kililenga kupokea na kujadili maoni ya wadau kuhusu nauli za Meli mpya ya MV Mwanza, kikao kilichofanyika katika Hoteli ya ELCT mjini Bukoba.
Meli ya MV Mwanza ni meli kubwa na ya kisasa iliyojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 120, ikiwa na uwezo wa kubeba tani 400 za mizigo pamoja na abiria 1,200 kwa safari moja. Meli hiyo inatarajiwa kuanza safari zake rasmi katika Ziwa Victoria, ikihudumia mikoa ya Mwanza, Kagera na maeneo mengine ya ukanda wa Ziwa hivi karibuni.
Akizungumza katika kikao hicho, Bwanku alieleza kuwa licha ya mapendekezo ya awali ya TASAC na TASHICO kuwa meli hiyo itafanya safari kati ya Mwanza na Bukoba pekee, ni muhimu pia ipitie Bandari ya Kemondo ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo ya jirani.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kupunguza nauli za meli hiyo ili wananchi wa kawaida waweze kumudu gharama za usafiri na hivyo kunufaika moja kwa moja na uwekezaji huo wa Serikali.
Kikao hicho kilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali (Mst) Hamis Maiga, ambaye aliwataka wadau kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa majini katika Ziwa Victoria.






Saturday, December 20, 2025
mwangaza wa hbari







0 comments:
Post a Comment