Wednesday, December 31, 2025

RUNALI YATATUA CHANGAMOTO YA MAJI KITUO CHA AFYA MARAMBO

Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea katika hafla ya kukabidhi kisima cha maji kilichojengwa na RUNALI katika kituo cha afya Marambo kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea katika hafla ya kukabidhi kisima cha maji kilichojengwa na RUNALI katika kituo cha afya Marambo kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea akifungua maji wakati hafla ya kukabidhi kisima cha maji kilichojengwa na RUNALI katika kituo cha afya Marambo kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea 


Na Fredy Mgunda, Nachingwea 

Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI kimetatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika Kituo cha Afya Marambo, changamoto iliyodumu kwa miaka mingi na kusababisha baadhi ya huduma kushindwa kutolewa ipasavyo katika kituo hicho.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kisima hicho cha maji, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI, Odas Mpunga, alisema kuwa lengo kuu la mradi huo ni kusogeza huduma muhimu kwa jamii inayohudumiwa na Kituo cha Afya Marambo.


Mpunga alisema chama hicho kilipokea maombi ya kusaidia kutatua changamoto ya maji katika kituo hicho cha afya, hali iliyopelekea RUNALI kuchukua jukumu hilo kwa dhamira ya kuisaidia jamii.


Aliongeza kuwa kisima hicho kimekamilika na kuanza kutoa huduma, hivyo ni jukumu la wananchi pamoja na viongozi wa eneo hilo kuhakikisha wanakitunza ili kiwe mradi endelevu wenye manufaa ya muda mrefu.


Kwa upande wake, Meneja wa RUNALI, Jahida Hassan, alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya kutimiza msingi wa saba (7) wa vyama vya ushirika, unaohimiza vyama hivyo kurudisha mchango kwa jamii inayowazunguka.


Jahida aliongeza kuwa kisima hicho ni kirefu na kina maji ya kutosha, hivyo kinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, hususan kuhudumia Kituo cha Afya Marambo.


Alisema kuwa RUNALI imetumia zaidi ya shilingi milioni 15 kuchimba kisima hicho hadi kukamilika kwake na kuanza kutoa huduma za maji katika kituo hicho cha afya.


Naye mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Hassan Ngoma, aliwataka wananchi na viongozi wa eneo hilo kuhakikisha wanauhudumia na kuutunza mradi huo ili uwe na manufaa ya kudumu kwa jamii na serikali kwa ujumla.


Ngoma alisema kuwa fedha nyingi zimewekezwa katika mradi huo wa kisima cha maji kwa lengo la kutatua kero ya maji kwa wagonjwa, wahudumu wa afya pamoja na wananchi wanaohudumiwa na kituo hicho, hivyo ni muhimu kulinda na kuutunza uwekezaji huo.


Aidha, aliwahimiza wananchi na wakulima ambao bado hawajajiunga na vyama vya ushirika kufanya hivyo kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Monday, December 22, 2025

SERIKALI YATOA SIKU 90 KWA WAMILIKI WA MAENEO YA KAZI KUJISAJILI OSHA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, akizungumza na watumishi wa OSHA kwenye ziara ya kikazi katika Ofisi za OSHA Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akimkabidhi Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Rahma Kisuo, vifaa kinga (Personal Protective Equipment-PPEs) ambavyo atakuwa anavitumia anapotembelea maeneo yakazi kwa ajili ya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akimkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi yaWaziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, vifaa kinga (Personal Protective Equipment-PPEs) ambavyo atakuwa anavitumia anapotembelea maeneo yakazi kwa ajili ya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya
Watumishi wa OSHA wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, wakati wa ziara ya kikazi katika Ofisi za OSHA Dar es Salaam.




Na Fredy Mgunda 

Serikali imewataka wamiliki wote wa maeneo ya kazi nchini ambao bado hawajayasajili maeneo yao na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuhakikisha wanasajili maeneo hayo ndani ya siku 90 kuanzia Januari 2026, hatua inayolenga kuimarisha usalama na afya kwa wafanyakazi nchini.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za OSHA zilizopo Kinondoni, Jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo ni ya kwanza kwa Waziri Sangu tangu alipoteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo, ikiwa na lengo la kujifunza kwa kina namna OSHA pamoja na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara hiyo zinavyotekeleza majukumu yao ya kisheria.

Akizungumza na menejimenti na watumishi wa OSHA leo (Desemba 22, 2025), Waziri Sangu amesema taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kulinda nguvu kazi ya Taifa dhidi ya ajali, magonjwa ya kazini pamoja na vifo vinavyosababishwa na mazingira hatarishi ya kazi.

Amesema ili OSHA iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo, ni lazima maeneo yote ya kazi yatambulike rasmi kupitia usajili, jambo litakaloiwezesha taasisi hiyo kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa waajiri.

“Uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi hauwezekani iwapo maeneo ya kazi hayajasajiliwa. Serikali imeamua kutoa siku 90 kuanzia Januari 2026 ili wamiliki wote wa maeneo ya kazi wahakikishe wanakamilisha zoezi hili,” amesema Waziri Sangu.

Aidha, amewataka watumishi wa OSHA kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kuzingatia weledi ili kuwawezesha waajiri kusimika mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi. Vilevile, amewahimiza waajiri kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa OSHA kwa lengo la kuzuia ajali na magonjwa ya kazini.

Waziri Sangu ameeleza kuwa usajili wa maeneo ya kazi unatekelezwa kwa mujibu wa kifungu cha 16 na 17 cha Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, inayoiwezesha OSHA kusajili maeneo ya kazi, kuyakagua na kutoa mapendekezo ya kitaalamu juu ya uboreshaji wa mazingira ya kazi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema taasisi hiyo imefarijika kumpokea Waziri na kupata maelekezo yake, huku akiahidi kuwa watumishi wa OSHA wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia miongozo ya serikali.

“Kwa niaba ya watumishi wenzangu, nakuhakikishia kuwa tutatekeleza maelekezo yote ya serikali kwa weledi na uadilifu mkubwa, ili kuhakikisha usalama na afya za wafanyakazi zinalindwa na taasisi yetu inaendelea kutimiza wajibu wake,” amesema Bi. Mwenda.

Katika ziara hiyo, Waziri Sangu aliambatana na Naibu Waziri, Rahma Kisuo, pamoja na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

OSHA ni taasisi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), yenye jukumu la kutoa na kusimamia miongozo ya usalama na afya mahali pa kazi. Kupitia usajili, ukaguzi na ushauri wa kitaalamu, taasisi hiyo inalenga kuboresha mazingira ya kazi na kulinda maisha ya wafanyakazi nchini.

Sunday, December 21, 2025

OSHA YATAJWA KUWA NA NAFASI MUHIMU KATIKA KUWEZESHA SHUGHULI ZA UZALISHAJI – KATIBU MKUU

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akitoa maelezo ya awali katika ufunguzi waKikao cha Tano cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa OSHA Kilichofanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dododma Desemba 20,2025.Wajumbe wa Baraza la OSHA wakiimba wimbo wa mshikamano (solidarity) wakati wa kikao cha Tano cha Baraza la Tano la wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma Desemba, 20, 2025

Wajumbe wa Baraza la OSHA wakifuatilia majadiliano mbalimbali yaliowasilishwa katika kikaocha Tano cha Baraza la Tano la wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika katika Ofisi za OSHA Jijini Dodoma.Desemba, 20, 2025.


Na Fredy Mgunda 

Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Bi. Mary Maganga, amesema Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) ni taasisi yenye umuhimu mkubwa katika kuwezesha shughuli za uzalishaji kufanyika kwa tija na ufanisi.

Bi. Maganga ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikao cha Tano cha Baraza la Tano la Wafanyakazi wa OSHA kilichofanyika leo, Desemba 20, 2025, jijini Dodoma, ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Amesema OSHA ina jukumu muhimu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, huku akiipongeza taasisi hiyo kwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Aidha, amewasisitiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia kanuni za utumishi wa umma na kuimarisha ushirikiano kazini.

“Kabla ya kufungua rasmi kikao hiki, napenda kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa weledi. Mara nyingi tumekuwa tukiamini kuwa wito unawahusu zaidi viongozi wa dini, lakini hata kazi zetu hizi ni wito, kwani kuna wananchi wengi wanaotegemea huduma zetu,” amesema Bi. Maganga.

Awali, akimkaribisha Katibu Mkuu kufungua kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema kikao hicho kinalenga kutathmini utendaji wa taasisi kwa kipindi kilichopita na cha sasa, pamoja na kuweka mwelekeo wa maendeleo ya OSHA kwa kipindi kijacho.

Amesema kikao hicho kinatazama utekelezaji wa shughuli za mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na tathmini ya utendaji katika miezi mitano ya mwaka wa fedha 2025/2026, ikiwa ni maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Bi. Mwenda ameongeza kuwa kikao hicho kilitanguliwa na mafunzo kwa watumishi wote wa OSHA yaliyohusu maadili ya utumishi wa umma, mpango mkakati wa taasisi wa miaka mitano ijayo (2026/2027–2030/2031), masuala ya afya ya akili na itifaki.

Kwa upande wake, akitoa salamu za wafanyakazi, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Bw. Rugemalila Rutatina, ameipongeza OSHA kwa kuzingatia ushirikishwaji wa watumishi wote bila ubaguzi katika kufanya maamuzi yanayohusu utendaji wa taasisi hiyo.


Saturday, December 20, 2025

BWANKU ASHAURI MELI MPYA YA MV MWANZA KUPITA BANDARI YA KEMONDO NA KUPUNGUZA NAULI

Afisa Tarafa ya Katerero, Bwanku M. Bwanku, ameshauri Meli mpya ya MV Mwanza kupitishwa katika Bandari ya Kemondo na nauli zake kupunguzwa ili wananchi wengi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania
Baadhi ya viongozi walioshiriki kikao hicho.


Na Fredy Mgunda.

Afisa Tarafa ya Katerero, Bwanku M. Bwanku, ameshauri Meli mpya ya MV Mwanza kupitishwa katika Bandari ya Kemondo na nauli zake kupunguzwa ili wananchi wengi waweze kunufaika na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania.

Bwanku alitoa ushauri huo umetolewa wakati wa kikao cha wadau wa bandari za Kagera kilichowakutanisha Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri wa majini.

Kikao hicho kililenga kupokea na kujadili maoni ya wadau kuhusu nauli za Meli mpya ya MV Mwanza, kikao kilichofanyika katika Hoteli ya ELCT mjini Bukoba.

Meli ya MV Mwanza ni meli kubwa na ya kisasa iliyojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 120, ikiwa na uwezo wa kubeba tani 400 za mizigo pamoja na abiria 1,200 kwa safari moja. Meli hiyo inatarajiwa kuanza safari zake rasmi katika Ziwa Victoria, ikihudumia mikoa ya Mwanza, Kagera na maeneo mengine ya ukanda wa Ziwa hivi karibuni.

Akizungumza katika kikao hicho, Bwanku alieleza kuwa licha ya mapendekezo ya awali ya TASAC na TASHICO kuwa meli hiyo itafanya safari kati ya Mwanza na Bukoba pekee, ni muhimu pia ipitie Bandari ya Kemondo ili kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo ya jirani.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kupunguza nauli za meli hiyo ili wananchi wa kawaida waweze kumudu gharama za usafiri na hivyo kunufaika moja kwa moja na uwekezaji huo wa Serikali.

Kikao hicho kilifunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera kupitia kwa Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali (Mst) Hamis Maiga, ambaye aliwataka wadau kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri wa majini katika Ziwa Victoria.

Thursday, December 18, 2025

WAHIFADHI TFS SAO HILL WAJENGEWA UELEWA WA AFYA

Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu,akiwa anapima afya akiwaongoza watumishi wengine wa Zao Hill kupima afya zao na amesema mafunzo hayo hutolewa kila mwaka kama sehemu ya mafunzo endelevu kwa watumishi wa TFS, yakilenga kuwajengea uwezo wa kujikinga na magonjwa yanayoathiri afya na kushusha kasi ya utendaji kazi.
Wahifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoka Shamba la Miti Sao Hill wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu masuala ya afya, yakilenga kuongeza uelewa juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wao na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa misitu.
Wahifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoka Shamba la Miti Sao Hill wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu masuala ya afya, yakilenga kuongeza uelewa juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wao na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa misitu.


Na Fredy Mgunda, Mufindi Iringa 

Wahifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoka Shamba la Miti Sao Hill wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu masuala ya afya, yakilenga kuongeza uelewa juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wao na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa misitu.

Mafunzo hayo yamelenga kuwaelimisha wahifadhi kuhusu hali halisi ya maambukizi ya VVU, njia za kujikinga, umuhimu wa upimaji wa hiari na wa siri, pamoja na kuondoa dhana potofu zinazokwamisha juhudi za kudhibiti maambukizi. Washiriki walikumbushwa kuzingatia maadili, kujilinda na kuchukua tahadhari stahiki katika maisha ya kila siku.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, amesema mafunzo hayo hutolewa kila mwaka kama sehemu ya mafunzo endelevu kwa watumishi wa TFS, yakilenga kuwajengea uwezo wa kujikinga na magonjwa yanayoathiri afya na kushusha kasi ya utendaji kazi.

“Afya njema ni mtaji muhimu katika kulinda rasilimali za misitu, kwani kazi ya uhifadhi inahitaji nguvu, umakini na utayari wa mwili na akili. Ni muhimu kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kujikinga na magonjwa mbalimbali,” amesema PCO Yoramu.

Katika mafunzo hayo, mada za magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani zilijadiliwa kwa kina. Wahifadhi walielimishwa kuhusu dalili za awali, visababishi na athari za magonjwa hayo kwa afya na ufanisi wa kazi.

Washiriki walihimizwa kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kudhibiti msongo wa mawazo na kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi pamoja na uvutaji wa sigara, ambavyo vimetajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya magonjwa yasiyoambukiza.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Dkt. Bonaventura Chitopela, amesema kila mmoja ana wajibu wa kulinda afya yake kwa kupima afya mapema na kufuata ushauri wa wataalamu ili kupata matibabu kwa wakati.

“Tumia fursa hizi kupima afya zenu mara kwa mara ili kujua hali za kiafya mapema, hatua itakayowezesha kupata matibabu na ushauri kwa wakati,” amesema Dkt. Chitopela.

Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka TACAIDS na Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Emmanuel Petro, amewataka wahifadhi kutumia kikamilifu elimu waliyoipata kwa kuchukua hatua za mapema dhidi ya changamoto za kiafya, akisisitiza kuwa uzingatiaji wa maelekezo ya wataalamu ni msingi wa kuzuia madhara ya kiafya.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za TFS kuhakikisha wahifadhi na watumishi wake wanakuwa na afya bora, nidhamu na uwajibikaji. Wahifadhi walioshiriki wameahidi kuzingatia elimu waliyoipata na kuwa mabalozi wa afya njema katika maeneo yao ya kazi na jamii zinazowazunguka.

MBUNGE LIWAKA KUWANUNULIA KOFIA NGUMU BODABODA ZAIDI YA 300.

Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Fadhili Liwaka akitoa ahadi ya kuwalipia bodaboda zaidi 300 shilingi Elfu tano (5000) kwa Kila bodaboda atakayekwenda kununua kofia ngumu kwenye duka maalum alilolipendekeza.
Baadhi ya madereva bodaboda wakiwa makini kumsikiliza Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Fadhili Liwaka akitoa ahadi ya kuwalipia bodaboda zaidi 300 shilingi Elfu tano (5000) kwa Kila bodaboda atakayekwenda kununua kofia ngumu kwenye duka maalum alilolipendekeza.


Na Fredy Mgunda, Nachingwea.

Mbunge wa Jimbo la Nachingwea Fadhili Liwaka ameahidi kuwalipia bodaboda zaidi 300 shilingi Elfu tano (5000) kwa Kila bodaboda atakayekwenda kununua kofia ngumu kwenye duka maalum alilolipendekeza.

Akizungumza katika kikao kazi na bodaboda hao, Mbunge Liwaka alisema kuwa ameamua kuwaunga mkono kwa kiasi hicho cha fedha kwa lengo kuwaondolea adha ya kukamatwa na polisi wa barabarani pamoja kujikinga na ajali za barabarani.

"Napokea simu kutoka kwa bodaboda juu ya kukamatwa na polisi wa barabarani kwa kosa la kutokuwa na kofia ngumu hivyo Mimi kama Mbunge wenu nimeamua kuwachangia kiasi hicho ili kila mmoja wenu aweze kulimiki kofia ngumu yake"alisema Mbunge Liwaka 

Mbunge huyo aliliomba Jeshi la Polisi wilaya ya Nachingwea kuwapa muda mfupi ili kila bodaboda aweze kununua kofia ngumu kwa ofa aliyoitoa ya kuwachangia kiasi Cha shilingi Elfu tano kununua kofia hizo.

Kwa upande wake kiongozi wa bodaboda alimshukuru Mbunge Liwaka kwa moyo wa dhati wa kuwasaidia vijana hao kupata kofia ngumu kwa bei ya ofa ambayo amechangia Kila kofia ngumu shilingi Elfu tano.

Nao baadhi ya waendesha bodaboda wilaya ya Nachingwea akiwemo Mohamed Rashidi wamemshukuru Mbunge na kuahidi kutoa kiasi hicho cha fedha ili kuwaezesha bodaboda kupata kofia ngumu na  wapo tayari kumuunga mkono kwa kununua kofia hizo kama alivyo waelekeza.

MWISHO.

Tuesday, December 16, 2025

MBUNGE LIWAKA AWAHAKIKISHIA MAMALISHE KUTATULIWA CHANGAMOTO ZA MAJI, MASOKO NA MIKOPO

Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka,akisonga ugali kwenye moja ya masoko ambayo mama nitilie wanaojihusisha na uuzaji wa vyakula
Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka, amewahakikishia mama lishe wa jimbo hilo kuwa atashughulikia changamoto zinazowakabili zikiwemo upatikanaji wa maji safi, usafi wa masoko, mikopo kwa wajasiriamali wadogo pamoja na maboresho ya miundombinu ya masoko ili yawe rafiki kwa wafanyabiashara na wateja.
Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka,akisonga ugali kwenye moja ya masoko ambayo mama nitilie wanaojihusisha na uuzaji wa vyakula

Na Fredy Mgunda, Nachingwea.


Mbunge wa Jimbo la Nachingwea, Fadhili Liwaka, amewahakikishia mama lishe wa jimbo hilo kuwa atashughulikia changamoto zinazowakabili zikiwemo upatikanaji wa maji safi, usafi wa masoko, mikopo kwa wajasiriamali wadogo pamoja na maboresho ya miundombinu ya masoko ili yawe rafiki kwa wafanyabiashara na wateja.


Mheshimiwa Liwaka ametoa ahadi hiyo wakati wa ziara ya mikutano mbalimbali na mamalishe katika Kata za Nachingwea na Ugawaji, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuimarisha ushirikiano na kusikiliza kero zao moja kwa moja.


Akizungumza katika Soko Kuu la Nachingwea, Mbunge Liwaka alisema ameanza ziara zake kwa wajasiriamali wadogo kutokana na kutambua mchango wao mkubwa katika kuendesha uchumi wa familia na jamii kwa ujumla. Alisisitiza kuwa mamalishe ni nguzo muhimu ya uchumi wa chini, hivyo wanastahili kupewa kipaumbele.


“Ni wajibu wangu kuwa karibu nanyi, kuwashukuru kwa kuniunga mkono katika Uchaguzi Mkuu na kuomba ushirikiano wenu katika kuendelea kulijenga Jimbo la Nachingwea,” alisema Mheshimiwa Liwaka.


Kwa upande wake, mmoja wa mamalishe wa Soko la Voda, Bi. Fortunata Robert Makarius, alimpongeza Mbunge huyo kwa kuwafuata uso kwa uso, akisema hatua hiyo imewapa faraja na matumaini makubwa kwani haijawahi kufanywa na mbunge yeyote aliyewahi kuliongoza jimbo hilo.


 Mbunge Liwaka alimalizia kwa kuwahakikishia mamalishe kuwa Serikali ya Wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri itaendelea kushughulikia changamoto zao kwa hatua, huku akisisitiza mshikamano na ushirikiano kama msingi muhimu wa maendeleo ya Jimbo la Nachingwea.

Tuesday, December 9, 2025

MAFUNZO YA OSHA YAWANUFAISHA ZAIDI YA WANAWAKE 200

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akitoa maelezo ya awali kuhusu mafunnzo ya usalama na afya kazini yalitolewa na OSHA kwa wanawake wanaojihusisha na uzalishaji wa bidhaa za batiki Dar es Salaam 
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo ambaye ameelezea umuhimu wa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa makundi ya wajasiriamali wadogo huku akiitaka OSHA kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu. 

Na Fredy Mgunda

Wanawake zaidi ya 200 wanaojihusisha na utengenezaji bidhaa za batiki wamenufaika na mafunzo ya usalama na afya yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya shughuli zao za kila siku kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliyogharamiwa na serikali yametolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA)  katika eneo la Ilala Jijini Dar es Salaam ambapo mada mbalimbali zikiwemo dhana ya usalama na afya mahali pa kazi, vihatarishi vya usalama na afya katika shughuli za uzalishaji bidhaa za batiki pamoja huduma ya kwanza mahali pa kazi zimefundishwa.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Rahma Kisuo ambaye ameelezea umuhimu wa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa makundi ya wajasiriamali wadogo huku akiitaka OSHA kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu. 

“Wajasiriamali wadogo ni kundi muhimu sana na lenye mchango mkubwa katika kukuza  uchumi wa Taifa letu hivyo ni muhimu kuwapatia mafunzo ili waweze kutekeleza shughuli zao katika hali ya usalama,” amesema Naibu Waziri.

Aidha, amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kutokea kutokana ukosefu wa mifumo ya usalama na afya ikiwemo wafanyakazi wenye uelewa wa masuala husika. 

Sambamba na hayo, ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kutojihusisha na makundi yenye nia ya kuvuruga shughuli za uzalishaji na kuvunja amani ya nchi ya Tanzania. 

Awali, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa utekelezaji wa program atamizi ya wajasiriamali wadogo ya Taasisi hiyo ijulikanayo- Afya Yangu, Mtaji Wangu.

“OSHA ilibuni na kutekeleza program ya Afya Yangu-Mtaji Wangu ili kuziba mwanya wa uelewa wa masuala ya usalama na afya uliopo baina ya sekta rasmi na sekta isiyo rasmi hivyo kupitia program hii tumekuwa tukiainisha makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo na kuyawezesha kwa mafunzo pamoja na kuwapatia vifaa kinga muhimu kutegemeana na aina ya shughuli zao,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA.

Aidha, amesema program hiyo itaendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali hususan vijana ambao kwa mujibu wa tafiti za OSHA za hivi karibuni ndio waathirika wakubwa wa ajali katika maeneo ya uzalishaji kutokana na uelewa mdogo na ukosefu wa uzoefu kazini. 

Akitoa maoni yake katika mafunzo hayo, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Jesca Charles, ameishukuru OSHA kwa kuwapatia elimu na vifaa kinga ambavyo vitawasaidia kujikinga dhidi ya vihatarishi vya ajali na magonjwa hususan kemikali ambacho ndio kihatarishi kikubwa katika uzalishaji wa bidhaa za batiki. 

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More