Wakurugenzi wa Halmashauri zote mkoani Katavi, wameagizwa kurejesha
Sh200 milioni wanazodaiwa kuwalipa watumishi hewa ndani ya siku 21.
Mkuu
wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali mstaafu, Raphael Muhuga alitoa agizo
hilo jana katika kikao baina yake na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa
pamoja na waandishi wa habari.
Alikuwa akitoa taarifa ya kubainika kwa watumishi hewa wapya mkoani humo.
Muhuga
alisema kuendelea kubainika kwa watumishi hao hewa, itawabidi
wakurugenzi kuhakikisha fedha zote zilizolipwa kwa watu hao zinarejeshwa
serikalini kwa muda aliowataka wazirejeshe na wampatie taarifa
itakayothibitisha fedha hizo kurejeshwa.
Pia, mkuu huyo wa mkoa
aliagiza maofisi wa ofisi ya utumishi wachukuliwe hatua ya kinidhamu kwa
kusababisha watumishi hao hewa kulipwa fedha.
“Hili siyo suala
la bahati mbaya, bali hawa watu walidhamiria kulipa mishahara hiyo hewa
naimani wapo wenye maslahi juu ya jambo hili,” alisema Muhuga.
Aliagiza
wakurugenzi wote wa halmashauri, wahakikishe maofisa utumishi
wanawafuta watumishi hewa wote kwenye leja zao na wawachukulie hatua
wote waliohusika na suala hilo.
Hata hivyo, aliishukuru kamati ya watu wanne iliyoundwa kufanya kazi ya uhakiki wa watumishi mkoani humo.
Aliitaka iharakishe kukamilisha uchunguzi wa watumishi 15 ambao taarifa zao zimebainika kuwa na utata.
0 comments:
Post a Comment