Suala
la uhaba bandia wa sukari limeendelea kuitikisa nchi, lakini vyombo vya
ulinzi na usalama vikifanya kazi nzuri baada ya kuwatia nguvuni
wafanyabiashara wengine, waliohodhi bidhaa hiyo kinyume cha sheria huku
ikiwamo kukamata kilo 622,000 za mfanyabiashara Haruni Zakaria mkoani
Morogoro.
Mwishoni
mwa wiki, mfanyabiashara huyo anayemiliki Kampuni ya Al Naeem, alikutwa
akiwa ‘ameficha’ tani 4,579.2 za bidhaa hiyo katika maghala yake
yaliyoko Tabata, Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
wachunguzi wa taasisi hiyo na wa Jeshi la Polisi, walifanya ukachero wao
katika maghala ya kampuni hiyo yaliyopo Mbagala na Tabata, Mei 5, mwaka
huu.
Lakini
siku chache baada ya kunasa sukari hiyo, kikosi kazi cha Vyombo vya
Ulinzi na Usalama mkoa wa Morogoro kilichoundwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk
Kebwe Steven Kebwe kufuatilia wafanyabiashara walioficha sukari,
kimebaini kiasi cha kilo 622,000 za sukari zilizofichwa katika maghala
mbalimbali yaliyomo mkoani humo.
Dk
Kebwe amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Ulrich Matei kuweka ulinzi
kwenye maghala hayo yaliyokutwa yameficha sukari hiyo na kuhakikisha
inauzwa kwa bei elekezi, iliyowekwa na serikali kwa wananchi.
Pia
alimwagiza kuwafikisha wafanyabiashara walioficha sukari hiyo
mahakamani mara moja na kumsaka mfanyabiashara Sadick Yassin ambaye
alifunga duka lake wakati wa ukaguzi na kutokomea kusipojulikana.
Mali ya Zakaria wa Dar
Akizungumza
jana, Dk Kebwe alisema sukari hiyo imebainika kuwa ni mali ya
mfanyabiashara mmiliki wa Kampuni ya Al Naeem Enterprises na kuhifadhiwa
katika maghala mbalimbali ya Kiwanda cha Sukari Kilombero (K1) tani
429, Kiwanda cha Sukari Kilombero (K2) tani 135 na katika Manispaa ya
Morogoro tani 58.4, jumla kuwa ni tani 622.4
“Nimeunda
kikosi kazi cha kufuatilia wafanyabiashara walioficha sukari katika
maghala yao katika ukaguzi wa awali, jumla ya tani 622.4 za sukari
zimebainika kwenye maghala mbalimbali na sukari yote iliyobainika ni
mali ya Al-Naeem Enterprises na tayari maghala hayo yenye sukari yapo
chini ya ulinzi wa vyombo vya dola,” alisema.
Licha
ya kumwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa kuweka ulinzi katika maghala
hayo na kusimamia sukari hiyo inauzwa kwa bei elekezi ya serikali, pia
alimwagiza Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakiki iwapo
sukari hiyo imelipiwa kodi ya serikali.
Dk
Kebwe pia aliwataka wananchi katika maeneo mbalimbali mkoani humo,
kutoa taarifa za wafanyabiashara au watu walioficha sukari ili hatua
zichukuliwe mara moja dhidi yao.
Kabla
ya kuweka msimamo wa Serikali ya Mkoa dhidi ya wafanyabiashara dhalimu,
Dk Kebwe na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa walifanya
ziara ya kushtukiza ya kuhakiki upya maghala ya wafanyabiashara wa
maduka ya jumla katika Manispaa ya Morogoro.
Katika
ghala la Kampuni ya Sukari Kilombero lililipo mjini Morogoro lilikuwa
na tani 58.4 za sukari ambayo ni mali ya Al Naeem Enterprises.
Msimamizi
wa ghala hilo, Robert Charles alimfahamisha Mkuu wa Mkoa na timu yake
kuwa sukari hiyo ipo kwa muda wa mwezi mmoja sasa baada ya kununuliwa na
mfanyabiashara huyo kutoka kiwandani Kilombero.
Alisema
sukari tani 58.4 iliyokutwa ndani ya ghala hilo ni mali ya
mfanyabiashara Zakaria aliyeinunua kutoka kiwandani Kilombero na
kuihifadhi hapo akisubiri kusafirishwa na kuwauzia wanunuzi wa jumla.
Baadhi
ya wauzaji wa maduka ya jumla waliokaguliwa na timu ya Mkuu wa Mkoa,
Thabit Islam na Hassan Binzoo walisema hali ya upatikanaji wa sukari
katika kipindi hiki ni mgumu kutokana na kuadimika ghafla.
Dar yanaswa nyingine
Katika
Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, zimekamatwa tani 2,700 za
sukari zikiwa zimefichwa katika ghala moja eneo la Mbagala.
Akitoa
taarifa hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam jana, Paul Makonda,
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Photidas Kagimbo alisema sukari
hiyo imekamatwa baada ya Rais kutoa agizo la kuwabaini wale wote
walioficha sukari na kusababisha wananchi kuteseka kupata bidhaa hiyo.
Kagimbo
alisema licha ya kukamatwa kwa sukari hiyo Manispaa hiyo bado
inaendelea na msako ili kuwabaini na wafanyabiashara wengine waliohodhi
bidhaa hiyo.
Msako mkali Kahama
Wilayani
Kahama mkoani Shinyanga, Polisi imefanya upekuzi katika baadhi ya
maghala ya kuhifadhia sukari na kuwabaini baadhi ya wafanyabiashara
wanne wanaojihusisha na kazi hiyo.
Kamanda
wa Polisi mkoani Shinyanga, Michael Nyange alisema wamefanya ukaguzi
katika maghala ya wafanyabiashara wakubwa wa sukari, ambayo ni ya
wafanyabiashara John Hango (walikuta mifuko miwili ya kilo 50), Nyorobi
Kisabu (hakuna kilichokutwa), Mshaka Kaziro (hakuna kilichopatikana) na
Alex Magina (mifuko 40, yenye kilo 50 kila mfuko). Alisema kazi hiyo
itakuwa endelevu.
RC Dodoma aagiza iuzwe
Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana ameagiza tani 154 kuuzwa kwa
wananchi kwa bei elekezi, huku akiwataka wafanyabiashara ambao bado
wameficha sukari kuitoa mara moja kabla rungu halijawashukia.
Takukuru
kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoani hapa walikamata
na kuzifungia tani 154 za sukari katika ghala la mfanyabiashara Haidary
Gulamali na sasa Rugimbana ametoa agizo la kufunguliwa kwa ghala hilo
ili litoe huduma kwa wananchi.
Mkuu
wa Mkoa akiwa amefuatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa alisema
wameamua kufungua ghala na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ambao
wanauhitaji mkubwa kwa sasa wa sukari.
0 comments:
Post a Comment