MBUNGE wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi akizindua
gari la kubeba wagonjwa (ambulance)
na fredy mgunda,iringa
|
MBUNGE wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi kwa
kushirikiana na asasi ya kimataifa ya Rafiki Surgical Mission ya Australia
ametoa msaada wa gari la kubeba wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya matumizi ya
hospitali ya wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa iliyopo katika jimbo lake hilo.
Gari hilo aina ya Toyota Hiace lenye
thamani ya Sh Milioni 40 lilikabidhiwa jana kwa uongozi wa halmashauri ya mji
wa Mafinga inayosimamia uendeshaji wa hospitali hiyo katika mkutano mkubwa wa
hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mashujaa, mjini Mafinga.
Akikabidhi msaada huo Chumi alisema; “napenda
ifahamike kwamba gari hilo limenunuliwa na asasi hiyo ambayo mimi ni rafiki yao
mkubwa. Uadilifu na uaminifu kwa taasisi hiyo umetufanya tushirikiane vyema
katika mambo mengi kwa faida ya wananchi wa jimbo langu la Mafinga.”
Alisema gari hilo la wagonjwa ni rafiki kwa wagonjwa
na wajawazito kwa kuwa lina vifaa tiba vinavyoweza kutumika kutolea huduma
wakati wakipelekwa hospitalini.
Baada ya kukabidhi gari hilo, Chumi ambaye
ni mbunge wa kwanza wa jimbo hilo jipya, mkoani Iringa alikumbusha vipaumbele
vyake kwa wapiga kura wake kuwa ni kuhakikisha linapata huduma bora ya maji,
elimu, afya na miundombinu ya barabara.
Akishukuru kwa msaada huo, Kaimu Mganga
Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Dk Innocent Mhagama alisema kabla ya
msaada huo, hospitali hiyo ya wilaya ilikuwa na gari moja tu la kubeba
wagonjwa.
“Pamoja na kuhudumia hospitali hiyo ya
wilaya, gari hilo moja lilikuwa likihudumia vituo vingine 18 vya kutolea huduma
katika wilaya hiyo hivyo,” alisema.
Alisema kupatikana kwa gari hilo jipya
kutasaidia kuboresha huduma hiyo kwa
kuokoa maisha ya wagonjwa na maisha ya mama na mtoto ambayo ni kipaumbele
katika utoaji wa huduma za afya.
Akizungumzia huduma ya mama na mtoto
katika hospitali hiyo ya wilaya, Dk Mhagama alisema kwa wastani wajawazito 500
wanajifunga kila mwezi hospitalini hapo.
“Kati yao wajawazito zaidi ya 100 huwa
wanapata huduma za dharula huku wastani wa wajawazito 10 wakipatiwa huduma za
rufaa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment