Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Riziki Mngwali amepinga mpango wa
Serikali kuajiri wakunga wanaume katika baadhi ya zahanati kuhudumia
wajawazito wakati wa kujifungua kuwa ni udhalilishaji dhidi ya wanawake.
Mbunge huyo ameitaka Serikali kuzingatia mila za Kiafrika,
akisema imezoeleka kuwa huduma ya ukunga kwa wajawazito wakati wa
kujifungua hutolewa na wataalamu wanawake.
“Serikali haioni kuwa
kwa kuweka wakunga wanaume katika baadhi ya zahanati zake nchini ni
kuwadhalilisha wajawazito wanaojifungua?”alihoji Mngwali.
Akijibu
swali hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani
Jaffo alisema wakunga wanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na
Ukunga inayowataka kutoa huduma ya kumsimamia mjamzito wakati wa
uchungu, kujifungua na baada ya kujifungua bila kujali jinsia.
Alisema
pamoja na sheria hiyo, kumekuwa na changamoto zinazotokana na mila na
desturi za jamii ambazo husababisha baadhi ya wahitaji wa huduma hiyo
kutokubali kuhudumiwa na wakunga wanaume.
“Kutokana na hali hii,
Serikali itaendelea kuajiri wataalamu wengi ili pale penye changamoto
paweze kupatiwa ufumbuzi bila kukwaza jamii husika,” alisema Jaffo.
Naibu
waziri alisema hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa mbunge huyo kuuliza
swali hilo bungeni, lakini tayari amewasiliana na uongozi wa Mkoa wa
Pwani ambao umeeleza kuanza kulifanyia kazi jambo hilo na kwa baadhi ya
maeneo wameshaanza kupeleka wakunga wanawake.
0 comments:
Post a Comment