CCM
imesema kitendo cha Rais John Magufuli kumvua uwaziri Charles Kitwanga
kutokana na kuingia bungeni akiwa amelewa, kimedhihirisha kuwa bado kuna
baadhi ya watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma, lakini
hakitachukua hatua kwa kuwa ameshaadhibiwa.
Msemaji
wa CCM, Christopher Ole Sendeka jana alisema kitendo cha Kitwanga
kuingia bungeni akiwa amelewa kimewapa fundisho na sasa wanajua kuwa
kuna baadhi ya watumishi waliopewa dhamana na chama hicho, lakini
wanakiuka miiko ya maadili ya utumishi wa umma, jambo ambalo ni kinyume
na taratibu zao.
Sendeka
alisema licha ya kwamba Rais Magufuli amechukua hatua juu ya hilo na
kutoa adhabu, CCM itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya
wanasiasa waliopewa dhamana na chama hicho.
“Hatutasita kuchukua hatua endapo tutabaini kuna kada anayekiuka maadili ya viongozi wa umma,” alisema Sendeka.
Alisema
CCM inampongeza Rais Magufuli kwa uamuzi aliochukua dhidi ya Kitwanga
kwa kuwa hatua hiyo imedhihirisha kauli aliyowahi kusema kwamba
hataangalia mtu usoni wala kujali kabila au dini, ikiwa mtu huyo
atakiuka miiko ya uongozi.
Kuhusu CCM kumuadhibu Kitwanga, Sendeka alisema adhabu aliyopewa na Rais inatosha. “Hukumu haitolewi mara mbili,” alisema Sendeka.
Kitwanga
ambaye anatajwa kwenye sakata la utekelezaji mbovu wa mkataba wa
kufunga vifaa vya kuchukua alama za vidole baina ya Jeshi la Polisi na
kampuni ya Lugumi Enterprises, alivuliwa ukuu wa wizara hiyo nyeti baada
ya kutinga ndani ya ukumbi wa Bunge Ijumaa asubuhi na kujibu maswali
akiwa amelewa.
Hadi
jana jioni, Rais Magufuli alikuwa bado hajajaza nafasi hiyo nyeti huku
wananchi wakibashiri jina la mrithi wa Kitwanga kwa kuangalia jinsi
marais waliopita walivyokuwa wakijaza nafasi kama wa kumpandisha naibu
waziri wa wizara hiyo au nyingine, kumteua mtu anayemfahamu, kubadilisha
mawaziri na kumrejesha aliyewahi kuwa waziri ama kuteua kutoka kwenye
kanda anayotoka aliyetimuliwa.
Mara
nyingi katika uteuzi wa mawaziri, viongozi wakuu wa nchi wamekuwa na
utaratibu wa kuwapandisha baadhi ya manaibu kuwa mawaziri, kuwapa
uwaziri wabunge ambao amewateua au kuteua waziri kutoka katika mkoa
ambao anatokea waziri aliyeondolewa.
Mara zote saba ambazo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alifanya mabadiliko ya baraza la mawaziri alifuata utaratibu huo.
Alipomuondoa
aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka ambaye ni mbunge kutoka mkoa Kagera alimteua mbunge mwingine
kutoka mkoa huo, Charles Mwijage kuwa Naibu Waziri wa Nishati na
Madini.Kwa sasa Mwijage ni Waziri wa Viwanda na Biashara.
Utaratibu
huo unaweza kunufaisha wabunge sita wa majimbo yaliyopo mkoa wa Mwanza
ambao ni Chalres Tizeba (Buchosa), Mansoor Hirani (Kwimba), Kiswaga
Boniventura (Magu), Stanslaus Mabula (Nyamagana), William Ngeleja
(Sengerema) na Richard Ndassa (Sumve).
Mbali
na Kitwanga ambaye aliteuliwa kuwa waziri kutoka mkoa huo, Rais pia
alimteua mbunge wa Ilemela, Angelina Mabula kuwa Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Iwapo
Rais atatumia utaratibu wa kupandisha naibu waziri kuwa waziri, neema
huenda ikamuangukia mbunge wa Kikwajuni na Naibu Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mhandishi Hamad Masauni au naibu mawaziri kutoka wizara nyingine.
Katiba pia inampa Rais fursa ya kuteua wabunge 10 na tayari ameshatumia
nafasi sita.
0 comments:
Post a Comment