Tuesday, May 3, 2016

Picha si ya tukio halisi
Watu wasiofahamika wamechoma moto Kanisa Katoliki Kigango cha Nyarwele, Parokia ya Kimiza, Jimbo la Kayanga wilayani Karagwe, Mkoa wa Kagera.

Katika tukio hilo la jana usiku, mali zote zilizokuwamo ndani ambazo thamani yake haijajulikana ziliteketea.

Shuhuda wa tukio hilo, Paulina Nkuba (67) alisema alifika eneo la tukio asubuhi baada ya kupewa taarifa na mjukuu wake anayesoma Shule ya Msingi Kimiza.

Alisema baada ya kufika katika eneo la tukio alipiga yowe kuomba msaada na alipoona watu hawatokei, alitoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji ndipo waliwajulisha wananchi na kuanza kukusanyika. 
Paroko wa Parokia ya Kimiza, Padre Fortunatus Bijura alisema kitendo hicho ni cha kuhuzunisha na kusisitiza hawataacha kusali kwa kuwa hata chini ya mti watafanya ibada.

Askofu wa jimbo hilo, Almachius Vicent Rweyongeza aliwataka waumini wasilipize kisasi hata kama wakimjua aliyechoma kanisa hilo.

Mwenyekiti wa kamati ya kanisa hilo, Sabas Kafuba alivitaja baadhi ya vitu vilivyoteketea kuwa ni jengo, nyaraka, meza, viti, kinanda na jenereta.

Akizungumza na wananchi, ofisa upelelezi wa Wilaya ya Karagwe aliyejitambulisha kwa jina la Masoud aliwataka kuunda vikundi vya ulinzi na kutoa taarifa za kukomesha uhalifu huo.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More