Uuzwaji wa nyumba za serikali umegeuka mwiba huku wabunge wakiendelea kuhoji hatua zilizochukuliwa kutokana na kadhia hiyo
Hatua hiyo iliyotekelezwa mwaka 2002 hadi 2004 ilizusha malalamiko mengi tangu wakati huo na sasa imeibuka tena bungeni
Akichangia
mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na mawasiliano jana,
mbunge wa Nachingwea, Hassani Masala (CCM) alihoji mfumo uliotumika
kuuza nyumba za serikali
Alisema haungi mkono kwa vile umesababisha viongozi wapya wa serikali wanaoteuliwa kujikuta wakiishi katika nyumba za wageni.
Mjadala
huo uliibuliwa juzi na msemaji wa kambi ya upinzani Bungeni kupitia kwa
waziri kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema kabla
ya Mwenyekiti wa Bunge Mussa Azzan Zungu kumtaka kuondoa baadhi ya maneno katika hotuba yake likiweo suala la uuzwaji wa nyumba za serikali.
Ritha Kabati Amvaa Lowassa
Akichangia
mjadala huo jana, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ritha Kabati alimtaja
aliyekuwa mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Edward Lowassa kuwa alinunua nyumba ya serikali iliyouzwa mwaka 2002
yenye jengo namba 68.
Alisema hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilisema nyumba za serikali 7,921 ziliuzwa tangu mwaka 2002 hadi 2004 na
kutaka serikali ya awamu ya tano kurejesha nyumba hizo kutokana na
walionunua kukiuka mikataba na malengo ya mauzo.
“Naomba
niwaambie usiangalie boriti lililo katika jicho la mwenzako wakati
kwako lipo, kwani hata mgombea wao wa urais Edward Lowassa alihusika kwa
kununua nyumba ya plot namba 68 na Fredrick Sumaye alikuwa Waziri Mkuu
na kuhusika kuuza nyumba hizo,” alisema Kabati.
Baada
ya kueleza hayo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge
wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) aliomba kumpa taarifa mbunge huyo kuwa
taarifa hiyo ni kwa maslahi ya taifa, hata kama mhusika atakuwa katokea
kambi ya upinzani sheria itachukua hatua.
"Kambi
ya upinzani tunapoibua jambo huwa linakuwa kwa maslahi ya Taifa, hivyo
ni vyema wabunge wote mtambue kuwa kosa likifanywa na kiongozi ni
lazima hatua zichukuliwe bila kujali ni wa Chadema, CUF au CCM.
"Tunapokuwa tunatoa uamuzi kama kambi ina maana sheria ifuate mkondo wake." Alisema Mbowe huku akishangiliwa na wabunge wa UKAWA
Awali
katika michango mbalimbali ya wabunge wa upinzani wamekuwa
wakilalamikia kuuzwa nyumba hizo za serikali na kudai kuwa watumishi
wapya wengi walioajiriwa, wamekuwa wakikosa maeneo ya kuishi.
Mbunge
wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) akichangia mjadala huo alilalamikia
kuuzwa kwa nyumba hizo pamoja na nyingine za Tazara zipatazo 500 na
kuamua kumpatia Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano ripoti
aliyodai inaonesha nyumba hizo zilivyouzwa.
0 comments:
Post a Comment