Kauli hiyo
ilitolewa na naibu katibu mkuu wa Chadema, Salim Mwalimu juzi kwenye
mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Moto wilayani Monduli Mkoa wa Arusha
ambako Lowassa alizungumza na wananchi kuwashukuru kwa kumpigia kura na
akatangaza mpango wa kuzunguka nchi nzima kwa lengo hilo.
Tangu
Rais atangaze kudhibiti uagizaji sukari kutoka nje na baadaye Bodi ya
Sukari kutangaza bei elekezi, bidhaa hiyo muhimu imepanda bei kutoka
Sh1,800 hadi kufikia Sh5,000 kwa kilo na kwa sasa imeadimika madukani,
wakati Serikali ikisaka wafanyabiashara inaowatuhumu kuwa wameificha
kwenye maghala kwa lengo la kuihujumu.
Akizungumza kabla ya
kumruhusu Lowassa kuongea na wananchi hao, Mwalimu alisema inaonekana
tatizo la sukari linaelekea kuishinda Serikali na hivyo inahitaji msaada
wa ushauri.
“Tatizo la sukari kalianzisha yeye mwenyewe Magufuli na sasa anashindwa kulitatua,” alisema Mwalimu na kuongeza:
“Mtu pekee atakayemsaidia ni Lowassa. Huyu alijipanga na alijiandaa kuongoza nchi.”
Mwalimu alisema Lowassa amevumilia mengi kwa kuwa amenyanyaswa, ameonewa na kusimangwa lakini hakujibu.
“Amepitia
kipimo cha mwisho cha utu, ni cha mwisho. Walimuonea mchana kweupe
akavumilia. Walimsimanga mchana kweupe mpaka watoto wadogo walikuwa
wakimuona Lowassa kama vile saizi yao, akavumilia,” alisema Mwalimu.
“Ninajua
vijana waliumia, mzee. Lakini leo warudi nyuma wafikirie maisha yao. Ni
nani angetoka nyumbani kwa kauli moja ya Lowassa, kumshika mtoto wake
mkono kumpeleka shule kama Lowassa angeangalia ushetani na kumuacha
Mungu,” alisema akirejea kauli ya Lowassa kuwa alikuwa akipigiwa simu na
watu kumtaka atoe kauli baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana
kutangazwa, lakini akaawaambia watulie.
Lowassa, ambaye
aligombea urais kwa tiketi ya Chadema baada ya kuenguliwa CCM, alishika
nafasi ya pili kwenye mbio hizo akipata kura milioni 6.07 idadi ambayo
ni rekodi kwa mgombea wa upinzani tangu siasa za ushindani zirejeshwe
mwaka 1992. Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura milioni 8.8.
Akizungumza
kwenye mkutano huo, Lowassa aliwataka wananchi kuendelea kutulia,
akisema mwaka 2020 hauko mbali na Chadema inaendelea kujipanga upya ili
kuhakikisha inashika dola na kuondoa kero zao.
Katika mkutano
huo uliohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Chadema kutoka makao
makuu, mkoa pamoja na makada waliojiunga wakitokea CCM wa wilaya ya
Monduli, Lowassa alisema wafuasi wa ukawa wajiandae kwa mikutano hiyo.
Huku
akishangiliwa na wananchi hao waliokuwa wakimkatisha kwa kelele za
shangwe, Lowassa alisema kwa kushirikiana na viongozi wenzake
wamejipanga kufanya ziara ya kuijenga Chadema nchi nzima.
“Nina
hakika tumewashika pabaya CCM na tumewaumiza sana. Sasa kwa kushirikiana
na viongozi wenzangu tutazunguka nchi nzima tunataka kuiweka Chadema
kwenye chama cha siasa na si uanaharakati,” alisema.
Akizungumzia
Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba 25 mwaka jana, Lowassa aliwashukuru
wananchi kwa kumpa kura nyingi akisema hata walioiba kura zake wanajua
na dunia inajua kuwa alishinda.
“Niliamua kukaa kimya kwani
najua ningesema jambo moja nchi yetu ingeangamia. Na vijana kila kona ya
nchi walikuwa wakinipigia simu wakidai wanasubiri neno kutoka kwangu,”
alisema.
“Sikufurahishwa na kwenda Ikulu kwa mikono iliyojaa
damu. Kuna siku nitakwenda Ikulu kwa mikono safi ya Watanzania, nina
hakika na rafiki zetu wanajua kabisa kwamba hawakushinda.”
0 comments:
Post a Comment