Wakati
mchungaji wa Kanisa la Moravian akikamatwa na meno ya tembo 11 ndani ya
kanisa, huko Moshi wachungaji wawili wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT) wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.
Tukio
la wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro linawahusisha wachungaji wawili
wa KKKT, Rodrick Mlay (52) na Godbess Mamkwe (38) pamoja na wananchi
watatu ambao jana walipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
mjini humo kwa madai ya kuua kwa kukusudia.
Wakati
wachungaji hao wawili wakipanda kizimbani, Polisi mkoani Katavi kwa
kushirikiana na askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi wanawashikilia watu
wawili akiwamo mchungaji wa Kanisa la Moravian kwa tuhuma ya kunaswa
wakiwa na meno ya tembo 11 wakiwa wameyahifadhi ndani ya kanisa.
Akizungumzia
meno hayo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda
alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi katika Kanisa la Moravian
lililopo Kijiji cha Usevya, Wilaya ya Mlele.
Nyanda
alisema mchungaji huyo akiwa na mwenzake ambao wote majina yao
yamehifadhiwa kwa sababu za upelelezi, walikamatwa kufuatia taarifa
zilizolifikia jeshi hilo na askari wa hifadhi kuwa, watu hao
wanajihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo na wamekuwa
wakiyahifadhi ndani ya kanisa.
Baada
ya taarifa hizo, polisi na askari hao walifanya uchunguzi kuhusiana na
taarifa hizo kwa kufika katika kanisa hilo na kufanya upekuzi
uliofanikisha kukamatwa kwa meno hayo yakiwa yamehifadhiwa kwenye tenga
la kubebea mizigo.
Kaimu
kamanda huyo alisema katika matukio mengine mawili tofauti yaliyotokea
Mei 8, saa mbili usiku kwenye maeneo ya Mgolokani, Kata ya Sitarike
wilayani humo, polisi kwa kushirikiana na askari wa hifadhi hiyo
walimkamata mtu mmoja akiwa na jino moja la tembo.
Nyanda
alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya askari kufanya upekuzi ndani
ya nyumba yake na kukamata jino hilo na lingine la simba.
Alisema wote waliokamatwa kwenye matukio hayo wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote ili kujibu tuhuma zinazowakabili.
Katika
tukio la wachungaji waliofikishwa mahakamani mjini Moshi, Hakimu
Mfawidhi wa mahakama hiyo, Julieth Mawole alisema wakiwa na wananchi
watatu aliowataja kwa majina ya Fadhili Mkenda (36), Jackson Ruben (45)
na Mathayo Moses (27), Mei 4 katika eneo la Kilema Pofo wanadaiwa kumuua
kwa makusudi Frank Peter (19).
Hakimu
Mawole aliwataka watuhumiwa hao kutojibu lolote na kesi dhidi yao
itasikilizwa Mei 23 katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na wote
walipelekwa rumande kwa sababu shtaka waliloshtakiwa nalo halina dhamana
kisheria.
Katika
hatua nyingine, raia wa Marekani, Mbaraka Mtambo (50) amekamatwa katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na maganda
mawili ya kobe bahari aliyokuwa ameyafichwa kwenye begi la nguo.
Kamanda
wa Polisi wa JNIA, Martin Otieno alisema raia huyo mwenye asili ya
Tanzania, alikamatwa juzi saa 3.45 usiku akijiandaa kwa ajili ya safari
ya kwenda Marekani na ndege ya Shirika la KLM kupitia Uholanzi.
0 comments:
Post a Comment