Tuesday, September 16, 2025

TRA NACHINGWEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAJASIRIAMALI WADOGO

Meneja wa TRA wilaya ya Nachingwea, Novatus Chamu akielezea namna dawati hilo litakavyo kuwa chombo muhimu cha kusikiliza kero, kutoa elimu ya kodi na ushauri wa kukuza mitaji kwa wajasiriamali wadogo.
Meneja wa TRA wilaya ya Nachingwea, Novatus Chamu akiwa kwenye picha pamoja na mgeni rasmi Stella kategile na baadhi ya watumishi wa TRA Nachingwea 
Mgeni rasmi Stella kategile akikataa utepe kuzindua rasmi dawati la TRA kwa ajili ya kusikiliza,kutoa huduma na elimu kwa wajasiriamali wadogo wadogo wa wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Meneja wa TRA wilaya ya Nachingwea, Novatus Chamu akiwa kwenye picha pamoja na mgeni rasmi Stella kategile na baadhi ya wajasiriamali wadogo wadogo wa wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.


Na Fredy Mgunda, Nachingwea Lindi.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani Nachingwea imezindua rasmi dawati maalum la kushughulikia changamoto za wajasiriamali wadogo, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha kiuchumi na kuwainua kutoka ngazi ya chini ya biashara hadi kuwa wafanyabiashara wakubwa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Meneja wa TRA wilaya ya Nachingwea, Novatus Chamu, alisema kuwa dawati hilo litakuwa chombo muhimu cha kusikiliza kero, kutoa elimu ya kodi, na ushauri wa kukuza mitaji kwa wajasiriamali wadogo.

“Kupitia dawati hili, tutaweza kusikiliza kero zao moja kwa moja, kuwapa elimu ya kodi na pia kuwashauri namna ya kukuza mitaji yao ili waweze kuchangia pato la taifa kwa ufanisi zaidi,” alisema Chamu.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kusogeza huduma karibu na wananchi, hasa wale waliopo kwenye sekta isiyo rasmi ambao mara nyingi hukumbwa na changamoto ya uelewa mdogo kuhusu masuala ya kodi na taratibu za biashara.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Stella Kategile, alieleza kuwa dawati hilo ni jukwaa muhimu la kukuza uchumi wa wafanyabiashara wadogo. Alisisitiza kuwa serikali inalenga kuwawezesha wajasiriamali kupitia utatuzi wa changamoto zao badala ya kuwabana kwa kodi bila kuelewa hali zao halisi.

“Lengo la serikali siyo kukusanya kodi tu, bali pia kusikiliza na kutatua changamoto za wajasiriamali ili waweze kukua na kuchangia kikamilifu katika pato la taifa,” alisema Kategile.

Baadhi ya wajasiriamali waliopata fursa ya kuzungumza walipongeza hatua hiyo ya TRA, wakisema kuwa imekuja kwa wakati muafaka kwani changamoto nyingi zimekuwa zikiwakwamisha katika kuendeleza biashara zao.

“Kwa muda mrefu tumekuwa hatuna pa kupaza sauti zetu. Kupitia dawati hili, tuna matumaini kuwa sauti zetu zitasikika na biashara zetu zitakua,” alisema mmoja wa wajasiriamali hao.

Dawati hilo linatarajiwa kuwa kiunganishi muhimu kati ya TRA na wajasiriamali, na mchango wake unatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika muktadha wa ukusanyaji wa mapato na ukuaji wa sekta ya biashara nchini.


0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More