Sunday, August 2, 2015

DOSARI YAJITOKEZA KURA ZA MAONI UBUNGE JIMBO LA IRINGA MJINI, MGOMBEA ATAKA MCHAKATO USITISHWE


frank Kibiki ambaye pia ni Mwanahabari wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo wa mkoani
frank Kibiki akionyesha walivyo kosea jina lake.


na mwandishi wetu,iringa


WAKATI kura za maoni za kutafuta wagombea ubunge katika majimbo yote nchini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) zikipigwa leo, mmoja kati ya wagombea 13 wanaotafuta nafasi hiyo Jimbo la Iringa Mjini, Frank Kibiki anataka zoezi hilo jimboni humo libatilishwe.

Wagombea wengine ni pamoja na Dk Augustino Maiga, Dk Yahaya Msigwa, Frederick Mwakalebela, Nuru Hepautwa, Michael Mlowe, Aidan Kiponda, Addo Mwasongwe, Jesca Msambatavangu, Mahamudu Mgimwa, Peter Mwanilwa na Fales Kibasa.

Akizungumza na wanahabari hii leo, Kibiki ambaye pia ni Mwanahabari wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo wa mkoani hapa alisema kura hizo zinapoteza uhalali kwasababu jina lake limekosewa.

“Mimi naitwa Frank John Kibiki, lakini kwenye karatasi ya kupigia kura ameandikwa mgombea mpya aliyetajwa kwa jina la Frank John Kibiri,” alisema.

Alisema kwa kuwa Frank Kibiki na Frank Kibiri ni watu wawili tofauti, hawezi kukubali kutumia jina la Kibiri ili kuhalalisha mchakato huo na endapo atafanya hivyo wagombea wenzake wanaweza kukata rufani kupinga matokeo hayo.

Kibiki alisema ameandika barua ya malalamiko yake kwa uongozi wa CCM wa Manispaa ya Iringa huku kopi ya malalamiko hayo yanayotaka uchaguzi huo ufanyike upya baada ya karatasi ya kupigia kura kusahihishwa akiipeleka kwa Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara.

Akikiri kupokea barua ya mlalamikaji huyo na dosari iliyojitokeza kwenye karatasi hizo za kupigia kura, Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi alisema; “suala hili tulikubaliana na mgomea huyo tulimalize kwa kusahihisha kwa peni jina hilo. Baada ya kuifanya kazi hiyo kabla ya zoezi lenyewe la upigaji kura kuanza, zoezi limeendelea kama kawaida.”

Taarifa ya Mwampashi imepingwa na Kibiki mwenyewe aliyesema katika vituo 81 kati ya 90 vya upigaji kura alivyotembelea ni kituo kimoja tu cha Umati alichokuta jina lake limerekebishwa katika karatasi hizo.

Huku akiahidi kuishtaki kampuni iliyopewa kazi ya kuchapisha karatasi hizo kwa kukosea jina lake, Kibiki alisema; “katika hili sitanyamaza, nitakuwa sauti ya yoyote aliyewahi kuonewa ndani ya chama  vinginevyo nitalazimika kusubiri miaka mitano ijayo ili nishriki kwenye mchakato mwingine wa haki.” Alisema.

Wakati huo huo Katibu wa CCM wa Manispaa hiyo amezungumzia idadi ya wana CCM waliojitokeza katika mchakato huo wa kura za maoni kuwa ni ndogo ikilinganishwa na matarajio yao ya kushirikisha wanachama zaidi ya 18,000.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More