Wednesday, March 14, 2018

WATANZANIA TUSIICHOKE AMANI

Na Emmanuel J. Shilatu

Misingi mizuri iliyojengwa na waasisi wa Taifa, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume ,  imesababisha Wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu kuishi kwa amani na utulivu, huku wakifanya mambo yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu yeyote wa ndani ama wa nje.
Tofauti na mataifa mengine, Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote wanakotaka na hata kuishi ama kufanya kazi au biashara bila ya bughudha yeyote endapo taratibu na sheria za nchi zitafuatwa ama kuzingatiwa vyema. Hali hiyo ni tofauti kabisa na nchi nyingine zikiwamo zile za jirani zetu kama Kenya, Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda, nchi ambazo kwa kiasi kikubwa ukabila na chokochoko za kisiasa zimetamalaki kuanzia ngazi za kijiji hadi Taifa. Hapa kwetu tumeishi kamaNdugu bila ya u-rangi, udini, ukabila wala harakati za kiitikadi na kisiasa kutugawa.
Jambo la kushangaza ni kuwa misingi hiyo ya amani na utulivu iliyogharamikiwa na Waasisi wetu, hivi sasa ipo shakani  na hatarini kutoweka kwani ilishaanza kuchezewa na chokochoko za aina mpya ya siasa (kwa maana ya ukosefu wa uvumilivu na uchu wa madaraka) iliyoanza kurindima katika siku za hivi karibuni.
Kuna kundi dogo la watu ambao wanasema bila ya woga, hofu wala aibu yeyote ile kuwa ni heri kukosa amani kuliko kuishi maisha ya amani na utulivu bila ya kuheshimiwa. Na huku wengine kwenye magari yao wakisadikiwa kuweka bango la maandishi makubwa yanayosema ni heri ya vita inayofuata haki na usawa kulikoamani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa Mwanadamu. Mbaya zaidi ni kuwa ujumbe huu umekuwa ukipeperushwa karibu kila kona waendapo na magari yao. Hao ndio Wanasiasa wetu.
Kinachoonekana hapa ni baadhi ya wawania madaraka kutaka machafuko kutokana na uroho ama kasumba ya  kuiga siasa za baadhi ya nchi ambazo hazijatulia huku wakijua vyema hatma ya madhara yake yalivyo.
Kama si utahira basi ni utoto kwa kufikiria dhana ya kheri ya kukosa amani ili kupata heshima pasipo uchanganuzi wa fikra ya madhara yake ya kama si kuuawa ama kupata ulemavu endapo amani itatoweka. Pia, hiyo heshima wanayoitafuta itakuwa na heshima gani endapo amani itayeyuka na vita kutawala?

Hizi ni chokochoko za kuchezea amani tuliyonayo, haina tofauti na mtu achezeaye shilingi katikati ya kina cha bahari. Inavyoonekana watu hawa wamesahau ule msemo wa wahenga “ usione vyaelea, ujue vimeundwa”; wanafikiria amani tuliyonayo imeletwa na Mungu kutoka mbinguni bila ya uwepo wa wajenzi wa amani . Hawajiulizi, kwanini nchi za Rwanda, Burundi, Kongo walifikia kwenye hatua ya kupigana wenyewe kwa wenyewe. Je, ni kwamba Mungu hawawapendi (ila anatupenda sisi tu) hadi akaruhusu hali ya vita kutokea? Tusijidanganye, wajenga amani ni Wazawa wenyewe.
Tangu mwaka huu uanze tumeuanza kwa masikio na macho yetu kupokea yale ambayo hatukuwahi kuyazoea maishani mwetu. Ni ajabu sana lakini ni kweli ya Watanzania tumefikia hatua ya raia wake kutaka kupima nguvu na vyombo vya dola, Hii haijawahi kutokea.
Leo hii si kaskazini, kusini, mashariki wala Magharibi kote huko kumejaa vumbi linaloashiria kuichoka amani tuliyonayo. Tatizo kubwa tulilonalo hapa ni kuruhusu siasa na Wanasiasa kutuburuza pasipo sie kuwa ndio waongozaji wa maisha yetu binafsi.
Katika siku za hivi karibuni kumetokea mijadala mikali sana ya juu ya sakata la maandamano linalochochewa kupitia mitandao ya kijamii huku yakichagizwa na Wanasiasa, Wanaharakati na Watu wengineo wasio na uchungu na Taifa letu la Tanzania.
Tumesikia kauli mbalimbali nzito toka kwa vyombo vya dola pamoja na viongozi wa Kitaifa. Tumemsikia IGP, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Nchini, tumemsikia Waziri wa Mambo ya Ndani na kama haitoshi tumesikia kauli nzito toka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli akitoa angalizo, onyo, tahadhari juu ya wale wote waliopanga kuandamana kuwa wasifanye hivyo yasije yakawakuta makubwa.
Ndugu zangu, Kuna Mwanamapinduzi mmoja wa Burkina Faso aitwaye Hayati, Kapteni Thomas Sankara. Kijana huyu aliacha hiba njema ya kuenziwa ndani ya nchi yake, Afrika na duniani.
Katika kauli zake Sankara alipata kukaririwa akisema; “Ningependa kuacha nyuma yangu, imani ya kuwa, kama tunaimarisha kiwango fulani cha uangalifu na oganaizesheni, basi, tunastahili ushindi. Kamwe huwezi kuleta mabadiliko ya kimsingi bila ya kuwa na kiwango fulani cha uwendawazimu”.
Mara nyingi chochezi za sampuli hii (ya kufanya maandamano unaofanywa mitandaoni), wanaoathirika ni Wananchi wa kawaida yaani mimi na wewe, wanyonge na walalahoi tusio na kimbilio zaidi ya kugeuzwa madaraja na mitaji kwao, na maumivu kwetu.
Historia inajidhihirisha kuwa nchi zilizotokea machafuko, tumeshuhudia wanaoshabikia ndio huwa chambo na wa kwanza kukumbwa na madhara ya kujeruhiwa, kuuawa ama mali zao kuharibiwa vibaya. Hata siku moja haijawahi kutokea wachochezi ama viongozi hao kuwa ni waathirika katika kile wanachowahamasisha watu wakifanye.
Tuchukulie kwa mfano mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 ama machafuko yaliyowahi kutokea Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007, mamia kama si maellfu ya watu (wananchi wa kawaida) walijeruhiwa, wengine kupoteza maisha yao huku mali zao zikiharibiwa vibaya mno.
Lakini hakuna kiongozi wa chama angalau wa ngazi ya wilaya, tuliyemsikia akipata madhara yeyote yale. Viongozi wote walioshinikiza hali hizo kutokea walikuwa nchi za nje na si Afrika tena wakila kuku kwa mrija wao, wake na watoto zao.
Kwa upande wa Kenya, baada ya hali kutulia, huku watu wakiishi kwenye mahema na misiba kila kona ikirindima, walijitokeza (wale wale wachochezi) kutoa pole kwa waliouawa, kuumia au kupoteza mali na Wapendwa wao. Kama haitoshi wakaamua kuwang’ong’a kama si kuwakebehi kwa kuwaita mashujaa, kisha viongozi hao wakaendelea na shughuli za kisiasa na baadhi yao ni wakubwa serikalini mpaka kesho. Wale wananchi wa kawaida wameambulia sifa na shukrani za kikebehi yenye majuto tele.
Nadhani umejionea ni  jinsi gani ambavyo wananchi wa kawaida wanavyoathirika pindi machafuko yanapotokea. Ni vyema Wananchi na wazalendo wote wa Taifa hili, kukataa nguvu yeyote ile ya uchochezi, iliyo na mapandikizi ya chuki,  na wanaotaka kutugawa kwa nguvu na akili zetu zote.
Historia inadhihirisha kuwa ni rahisi sana kuchochea machafuko, lakini ni ngumu sana kulitoa Taifa katika machafuko hayo, ni jambo linaweza kuchukua miaka na miaka katika kupata ufumbuzi wake na vyema sana Watanzania kutokuichoka amani tuliyonayo.
Ndugu zangu, hatuna sababu ya kuanza kuonyeshana misuli ya nani anaweza kumwoa binti Fulani wakati bado yu tumboni mwa Mama yake. Kwa kufanya hivyo niwazi tunavidhulumu vizazi vijavyo ambao wao haswaa ndio wenye gesi yao na wao ndio wajenzi wa Taifa la baadae.
Inawezekana kabisa miaka zaidi ya 50 tuliyoishi kwa amani na utulivu imewapumbaza baadhi ya Watu na kuanza kufikiria maisha ya Taifa la Mapigano ambayo siye hatujayazoea.
Ndugu zangu, Wapo wanaosema kuwa amani ni sawa na yai mkononi, ukilivunja hautaweza kuliunganisha kamwe; wengine wanasema kuwa amani haina bei na ikipotea haina soko la kununua. Tuitunze amani yetu na kamwe tusiizoee wala kuichoka!
Mungu Ibariki Tanzania.
0767488622


0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More