Monday, March 12, 2018

ECO Bank Tanzania kufadhili wanafunzi shule za serikali

Benki ya Eco nchini Tanzania kuanzia mwaka huu inaanzisha mpango wa kutoa zawadi ya ufadhili kwa wasichana wanaofanya vyema katika masomo yao kwenye shule za serikali.
Aidha pamoja na ufadhili huo ili kuwaweka katika hali ya kuwa na uzoefu na kazi zao wanazosomea, watakuwa wanahakikisha wakati wa likizo wanawafanyia mpango wa kujishughulisha na kazi hizo ili kuwa na uzoefu.
Hayo yamesema na Mkurugenzi Mkuu benki hiyo nchini Mwanahiba Mzee wakati wa hafla ya mchapalo iliyofanyika hoteli ya Serena kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani mwishoni mwa wiki.
Alisema taasisi yake inaona umuhimu wa kumwezesha mtoto wa kike kusonga mbele kama moto wa taasisi hiyo ya kifedha unavyosema ‘press for progress’ ikimaananisha kujikita katika kutafuta maendeleo.
Alisema mwanamke anafanyakazi nyingi hivyo ni vyema kumwandaa tangu mapema ili kujua majukumu yake kama mzalishaji mkuu kwenye familia.
Alisema kwa sasa hawajaamua wanaanzia ngazi gani za ufadhili, lakini wanataka kufanya kitu tofauti chenye kulenga kupromoti maendeleo ya mtoto wa kike kama maazimio ya Beijing yanavyotaka kufikia asilimia hamsini kwa hamsini katika ngazi za kiutendaji.
Alisema sherehe hiyo ambayo inaambatana na siku ya mwanamke duniani inasherehekewa katika nchi 33 zenye benki hiyo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kibenki wa kuhakikisha kwamba wanawake wanasonga mbele kwa kuwa idadi yao ni asilimia 49.55 ya watu waliopo duniani na wanahaki ya kusaidia kukua kwa uchumi wa dunia, wa kaya na wakwao wenyewe kwa kuwezeshwa.
Anasema pamoja na ukweli kuwa wanawake wameachwa nyuma kwa miaka mingi, taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha kwamba inakuwa na asilimia 50 kwa 50 ifikapo mwaka 2030 huku hapa nchini inakaribia asilimia 49.
Alisema wakati sherehe hiyo ni kusherehekea mafanikio na kujifunza kutoka kwa wanawake waliofanya vyema, wanawake wanatakiwa kujiuliza wamesaidiaje wanawake wenzao kufikia ngazi ya juu kabisa ya uwezo walionao.
Alisema katika taasisi yake wametengeneza mpango wenye vipengele vitano vya kuhakikisha kwamba suala la jinsia linazingatiwa. Alitaja vipengele hivyo kama kushawishi fikira za jinsia katika maeneo ya kazi kuona kwamba kuna mizania. Kukabili fikira mgando dhidi ya wanawake, kuwezesha mwanamke kuonekana wazi, kushawishi kuinua wanawake kwa kutwaa huduma bora wanazozitoa na kusherehekea mafanikio ya mwanamke.
Alisema amefurahishwa na jinsi wanawake majasiri kama Getrude Mongella walivyoweza kupigania haki za wanawake wakikabiliana na makandokando yake na kufanikisha maazimio ya Beijing ambayo yanatumika kumkomboa mwanamke.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo alisema pamoja na kupokea maelekezo ya mama Mongella kuhusu ustawishaji wa mwanamke, aliwataka wanawake kuwa wajasiri na kupambana na hali zao bila kujali wanatoka katika mazingira gani.
Alisema yeye alisoma katika shule ambazo sasa zinaitwa za Kayumba (shule za Upe) akianzia Mizumbwini Kibada hadi Kurasini kabla ya kupata nafsi ya kusoma Masjid Quba iliyopo Sinza na Alharamain alipomalizia kidato cha sita.
Unaona nimesoma shule za kawaida tu, siri kubwa ni kujituma na kujitambua. Nilijituma kwani niliona familia ya mama yangu ni watu maskini japo familia ya baba yangu walikuwa wanajiweza, nilisema lazima nimsaidie mama yangu.
Mwanahiba alisisitiza katika mazungumzo yake kwamba kujituma kunasaidia sana kwani hata yeye alipo ajiriwa kwa mara ya kwanza kama karani na kulipwa sh laki moja hakujali kwani alijua ni nafasi yake ya kujifunza japo alikuwa na MBA.
Aidha alisema kwamba alijifunza kwa bidii na kujenga kuaminika wakati akiwa Stanbic hali iliyompatia heshima ya jina lake kupelekwa katika mamlaka za Benki ambako alipita michujo mbalimbali na kufanikiwa kupata nafasi ya Ukurugenzi Mkuu ECO bank.
Naye Mama Mongella, mwanasiasa mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake aliyeshiriki Mkutano wa Beijing, akitoa nasaha zake, alimtaka Mkurugenzi wa Eco Bank kuwapatia wanawake mitaji ili waweze kumiliki viwanda vyao waweze kuajiri na kufukuza.
Aidha aliwataka wafanyakazi wa benki hiyo kutomwangusha mkurugenzi wao na kuhakikisha wanajituma zaidi hasa benki inapowania kuwa na asilimia 50 kwa 50 katika utendaji wake.
Alisema wakati taifa hili linaelekea katika viwanda benki hiyo inayoendeshwa na mwanamama inastahili kupigania maslahi ya wanawake ili wawe na viwanda na kuchangia katika uchumi badala ya wao kuwa wasindikizaji.
"Si kuwakorogea uji wanaofanya viwandani bali wao ndio wawe wenye restaurants (migahawa) … wenye viwanda.." alisema mama Mongella.
Aidha aliwataka wanawake wanapopata nafasi ya kuajiriwa wawe makini katika utumishi wao na kuacha kuwataka mabosi ndio wawapigie magoti.
Pamoja na kutaka wanawake waendelezwe aliitaka jamii isisahau watoto wakiume kwani nao wanastahili kupata haki za elimu ili waweze kuwa watu bora na wanaoelewa.
Kama sasa kuna matatizo je kama wasipoenda shule wakabaki kuwa wapumbavu matatizo si yatazidi zaidi, alihoji mama Mongella.
Alkiwataka wanawake katika kila nafasi yao kufanya vyema na kuaminika huku wakiwasaidia wanawake wenzao kusonga mbele ili waweze kuwa na chakula cha kutosha kuwawezesha kufanya maamuzi yaliyoshiba pia.
Akizungumzia tasnia ya habari alisema kwamba toka walipotoka katika mkutano wa Beijing waandishi wa habari wamekuwa ndio wenye mabadiliko makubwa wakiwabeba wanawake katika muonekano mzuri na kumshauri Mkurugenzi huyo kuwatumia waandishi kuonesha watu mambo makubwa yanayofanywa na wanawake.
Alisema yeye na mafanikio aliyonayo sasa ni matokeo ya uamuzi wa kutaka kukabiliana na matatizo ya kiuchumi ambapo aliona jinsi mwanamke wa kijijini anavyohangaika na kusema ataendelea kupigana kumbadilisha mwanamke awe katika maisha bora.
Alisema amebahatika kuwa na watoto watatu wote wanaume, lakini amesema mabinti watakaoingia katika mji wake atahakikisha kwamba anawahoji wamefanya nini au wanampango gani wa kusaidia wanawake wenzao.
Katika hafla hiyo ya mchapalo wanawake walibadilishana mawazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa na wakati wa kujifunza na kushangilia mafanikio ya mwanamke.
Mshehereshaji Babbie Kabae (kulia) akitambulisha wageni waalikwa kwenye hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Eco Bank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mjasiriamali mwenye uthubutu ambaye pia ni mteja wa Eco Bank Tanzania, Halima Mamuya akijitambulisha na ku-“share” uzoefu wake katika ujasiriamali wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Eco Bank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kutoka kushoto ni Ofisa Uchumi na Mipango wa jiji la Mwanza, Bertiller Masawe, Mjasiriamali Chance Bishikwabo, Mgeni rasmi Mwanasiasa Mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake, Mama Getrude Mongella pamoja na Mkurugenzi Mkuu Ecobank Tanzania, Mwanahiba Mzee wakisikiliza kwa umakini shuhuda za Mama Mamuya.
Mkurugenzi Mkuu Ecobank Tanzania, Mwanahiba Mzee akizungumza kabla ya mgeni rasmi ambapo alielezea kwa undani safari ya maisha kama mwanamke wakati hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Eco Bank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mgeni rasmi Mwanasiasa Mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake, Mama Getrude Mongella akitoa nasaha zake kwa wageni waalikwa na wafanyakazi wa Eco Bank Tanzania (hawapo pichani) wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Eco Bank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mchungaji Basilisa Ndonde akielezea kuhusu nafasi ya mwanamke katika familia na majukumu yake kama mke wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Eco Bank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mgeni rasmi mwanasiasa mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake, Mama Getrude Mongella akipiga selfie na baadhi ya wageni waalikwa wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Eco Bank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mgeni rasmi mwanasiasa mkongwe nchini na mpigania haki za wanawake, Mama Getrude Mongella katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni waalikwa wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Eco Bank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Miamala Eco Bank Tanzania, Wende Mengele.
Baadhi ya wageni waalikwa katika picha ya pamoja wakati wa hafla mchapalo ya kusherehekea mafanikio ya mwanamke katika Siku ya Wanawake duniani iliyoandaliwa na Eco Bank Tanzania na kufanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More