Mkurugenzi Mkuu mpya wa Kampuni ya Jumia Tanzania, Zadok Prescott (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo wakati akijitambulisha rasmi na kuzungumzia mambo mbalimbali ya kampuni hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Masoko wa Jumia Tanzania, Albany James.
Mkuu wa Masoko wa Jumia Tanzania, Albany James, akizungumza katika mkutano huo.
Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya Jumia Tanzania ambayo inajishughulisha na huduma za uuzaji na manunuzi ya bidhaa mbalimbali kwa njia mtandao imemtambulisha Zadok Prescott kuwa Mkurugenzi Mkuu wake mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa utambulisho wake uliofanyika kwenye ofisi za kampuni hiyo jijini Dar es Salaam, Bw. Prescott alibainisha kwamba ni fursa kwake kujiunga na kampuni ambayo imedhamiria kuleta mapinduzi ya biashara kwa njia ya mtandaoni hususani kwenye soko ambalo bidhaa zipo mbali na wateja pamoja na gharama kubwa za kufanya shughuli za masoko.
“Jumia ilianzishwa mnamo mwaka 2012 ikiwa na imani thabiti ya kwamba: ‘Mtandao wa intaneti unaweza kuboresha maisha ya Waafrika.’ Ni vigumu kupata bidhaa unayoihitaji kupitia mfumo wa sasa wa manunuzi ya bidhaa mbalimbali Tanzania. Upatikanaji wa bidhaa katika sehemu tofauti huwalazimu wateja kusafiri umbali mrefu kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Kwa kuongezea, bei hutofautiana kwa kila mfanyabiashara jambo linalopelekea kuwa ni changamoto kutambua kama unauziwa bidhaa kwa bei sahihi au la. Ni mfumo ambao humpotezea mteja muda na gharama katika maisha yake ya kila siku. Dhumuni kubwa la Jumia ni kuufanyia mabadiliko mfumo huu na kuufanya uwe wenye tija kwa wafanyabiashara nchini na kuwapatia wigo zaidi,” alisema Bw. Prescott.
Akifafanua namna Jumia ilivyodhamiria kuwa mkombozi kwa wafanyabiashara nchini ameelezea kuwa, “wafanyabiashara wanakumbwa na changamoto lukuki katika uendeshaji wa biashara zao zikiwemo gharama kubwa za pango hususani kwenye maeneo yenye wateja wengi. Hali hii hupelekea wafanyabiashara wengi kuwa na idadi ya wateja walewale kulingana na eneo walilopo,” alisema na kuongezea, “ili kuwafikia wateja kuwajulisha kuhusu biashara zao, inamlamzimu mfanyabiashara kufanya matangazo na kutafuta masoko, jambo ambalo ni gharama kubwa na sio wote wanakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.”
“Jumia ndio suluhu pekee kwa wateja na wafanyabiashara. Kwa sababu imekusanya bidhaa za aina tofauti sehemu moja, ikitoa bei zenye ushindani, pamoja na kumfikishia mteja popote alipo kwa urahisi. Mteja anaweza kufanya manununizi mwenyewe kwa kuingia kwenye mtandao wetu, akachagua bidhaa azipendazo na kisha akaletewe mpaka alipo baada ya kuagiza. Katika kujenga uaminifu kwa wateja wetu, malipo hufanyika baada ya kumfikia mteja. Kwa kuongezea, mteja huwa hadaiwi malipo pindi asiporidhika na bidhaa aliyopelekewa au akitaka ifanyiwe mabadiliko. Hivyo, tunawaahidi wateja wetu bidhaa nyingi zaidi kukidhi mahitaji yao, bei zenye ushindani zaidi na kuwafikishia bidhaa popote walipo kwa haraka, urahisi na gharama nafuu,” aliongezea.
“Zaidi ya kampuni 50,000 za kiafrika zinauza bidhaa zake kupitia Jumia kila siku. Tunafanya jitihada za kuhamisha shughuli za kiuchumi kwenda mtandaoni na kuziwezesha kampuni za Kiafrika ndogo, za kati na kubwa kupata wateja wapya na kuwahudumia kwa mbinu mpya. Takribani wajasiriamali na wafanyabiashara 50,000 wanauza bidhaa zao kupitia Jumia, zaidi ya bidhaa 10,000 zinajitangaza kupitia Jumia, pia kampuni kadhaa za usafirishaji husafirishaji mamilioni ya bidhaa kila mwaka kwa sababu ya Jumia.
Kila siku, tunasaidia na kuhamasisha migahawa, hoteli, wafanyabiashara wadogo, bidhaa, mawakala wa makazi na usafiri, makampuni makubwa, kampuni za usafirishaji kuwa bora na kubwa, kwa kutumia msaada wa ripoti za tafiti mbalimbali kuzisaidia kuwa bora na kutoa huduma nzuri kwa wateja, na tunaamini kupitia hivi tutaleta mabadiliko chanya barani Afrika.”
“Mojawapo ya fursa ambayo wafanyabiashara wengi wa kitanzania bado hawajaigundua ni namna ya kuwafikia wateja wanaopatikana mtandaoni. Kwa kujiunga na Jumia, tutakupatia fursa ya kukuunganisha na mamilioni ya wateja waliopo mtandaoni.
Tunaweza kumuwezesha mfanyabiashara mdogo anayefanya shughuli zake kwenye mitaa ya jiji la Dar es Salaam kuuza bidhaa zake kwa wateja walioko Tanzania nzima. Tunazitangaza bidhaa tofauti kwa kuziwezesha kuonekana kwa mtu yeyote aliyeunganishwa na mtandao wa intaneti,” alisema na kuhimitimisha Mkurugenzi Mkuu huyo mpya wa Jumia nchini Tanzania, “wafanyabiashara wanaojiunga nasi hawana haja ya kugharamia shughuli za kutafuta masoko au kukodisha maduka kwa gharama kubwa. Hii ni huduma ambayo Jumia huitoa kwa kamisheni nafuu kupitia mauzo yatakayofanyika mtandaoni.
Kitu pekee tunachokihitaji kutoka kwao ni kuuza bidhaa zenye ubora na bei nafuu kwa wateja wetu.”
Katika jitihada za kujenga hamasa ya biashara mtandaoni, Jumia huandaa shughuli za mara kwa mara za kimasoko ndani ya mwaka kama vile kuzindua bidhaa mpya, ofa kabambe na mapunguzo lukuki kwa ajili ya wateja.
Kwa upande wake Mkuu wa Masoko wa Jumia Tanzania, Albany James alipata fursa ya kugusia juu ya Jumia kuzindua kwa mara ya kwanza ‘Wiki ya Simu,’ kwa kushirikiana na kampuni ya simu ya Tigo. Alielezea kwamba kampeni hiyo inafanana na kampeni yao ya kila mwaka ya ‘Black Friday,’ lakini hii itajikita kwenye bidhaa za simu za mkononi pekee. Kampeni hii itahusisha uzinduzi wa bidhaa mpya, ofa kabambe, zawadi na punguzo kwa wateja.
Tukio hili tayari limekwishafanyika kwenye nchi za Kenya na Nigeria ambapo ni kubwa na maarufu, na kwa mara ya kwanza watanzania watanufaika na mapunguzo ya kuvutia na promosheni zitakazoletwa kwa ajili yao na Jumia. Itakuwa ni wiki ya aina yake kwa ajili ya kununua bidhaa za simu.
“Wiki ya Simu’ itaanza tarehe 19 mpaka 25 ya mwezi Machi mwaka huu ambapo itazinduliwa kwa muda wa siku mbili, tarehe 17 & 18 ya mwezi Machi katika viwanja vya Leaders Club. Uzinduzi huu utazileta pamoja kampuni mbalimbali maarufu za simu nchini katika tukio ambalo litakuwa ni la kipekee, la kifamilia, ambapo wahudhuriaji watakuwa na mazingira mazuri ya kununua bidhaa za simu pamoja na kufurahia chakula na muziki mzuri kwa ajili yao.
Tukio hili litawapatia wateja fursa ya kununua na kujionea matoleo mapya ya bidhaa za simu ambazo zinatawala soko kwa sasa kwa gharama nafuu pamoja na kujifunza mambo mengi zaidi kuhusu Jumia,” alielezea James.
Akijaribu kufafanua kwa kifupi juu ya bidhaa na ofa zitakazokuwepo kwenye ‘Wiki ya Simu,’ Mkuu huyo wa Masoko aliendelea kuwa Jumia kwa kushirikiana na Tigo, zimekuwa ndiyo kampuni za kwanza kuwapatia wateja fursa ya kuagiza simu ya Samsung S9 na S9+ kabla haijaingia sokoni.
Zoezi la kuagiza Samsung S9 lilianza mara moja kupitia Jumia mara baada ya hafla ya uzinduzi wa simu hiyo kufanyika kwa njia ya mtandao duniani kote kutoka kwenye Mkutano wa Dunia wa Simu za Mkononi uliofanyika jijini Barcelona, Hispania mnamo tarehe 25 ya mwezi Februari mwaka huu.
“Wateja watakaoagiza kupitia mtandao wa Jumia wataweza kujipatia simu zao wiki moja kabla ya Wiki ya kampeni, na watapokea kifaa cha kuchaji kwa haraka kinachotumia waya na miezi 6 ya bure ya kuunganishwa na intaneti kutoka Tigo. Vilevile tutakuwa na zawadi za kushtukiza siku ya tukio, katika wiki hiyo wateja wetu watapatiwa ‘chemsha bongo’ ya kuitafuta simu ya Samsung S9 yenye thamani ya zaidi ya milioni 2, ambayo itakuwa imefichwa kwenye mtandao wetu kwa kununua bidhaa zenye gharama isiyopungua shilingi 100,000! Mteja wa kwanza kuivumbua ataweza kujipatia simu hiyo kwa gharama nafuu zaidi nchini.
Tutakuwa na ofa za kuvutia, vocha na mapunguzo ambavyo vitawekwa wazi kadri tutakavyokaribia uzinduzi wa wiki hiyo,” alihitimisha James.
Kabla ya kujiunga na Jumia Tanzania, Bw. Zadok Prescott alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya Millicom (kampuni mama ya Tigo na Zantel) katika kitengo cha Kutafuta na Kuunganishaji biashara mpya kuanzia mwaka 2014 mpaka 2018. Bw. Prescott anao uzoefu mkubwa katika masuala ya ushauri wa mikakati, utafutaji na uunganishaji wa biashara mpya, kuboresha biashara, ambapo uzoefu wake unatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kupelekea Jumia kuwa mojawapo ya kampuni inayoongoza kwenye utoaji wa za huduma za biashara mtandaoni nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment