Tuesday, March 6, 2018

WANANCHI WALALAMIKIA UBOVU WA BARABARA MAFINGA

 Diwani wa kata ya Boma ulipo mtaa huo wa Wambi “B’Julius Kisoma amekiri kuitambua changamoto hiyo ya barabara kwa wakazi wake
 Barabara ya mtaa wa Wambi “B’ ikiwa inaonekana jinsi ambavyo imeharibika na kuwa kikwazo kwa wananchi wa mtaa huo

NA OLIVER MOTTO,IRINGA.

WAKAZI wa mtaa wa Wambi “B’ uliopo katika mji wa Mafinga mkoani Iringa- wapo katika mazingira hatarishi kutokana na barabara ya mtaa huo kuharibika, na kushindwa kupitika, huku hali ya ubovu huo wa barabara ikidaiwa kuharibu hata shughuli za kibiashara .

Wakizungumzia ubovu wa barabara hiyo- Mkombozi Mgimwa na Elizabet Geofrey mkazi wa mtaa wa Wambi “B’ almaarufu kwa “Malingumu” amesema ubovu wa miundombinu ya barabara hiyo unasababisha  madhara ya kiuchumi kwakuwa wanunuzi wenye usafiri mbalimbali yakiwemo magari na hata Pikipiki wanashindwa kufika katika eneo hilo kutokana na mashimo makubwa yaliyopo.

Aidha Elizabet amesema pia kuchimbuka kwa barabara hiyo ya Mta wa Wambi “B’ni hatari kwa usalama wao nawa watoto, kwamadai kuwa kila mvua zinaponyesha barabara hujaa maji na hugeuka kama mto kutokana na kukosekana kwa mifereji ya maji jambo ambalo ni hatari kwao.

Judith Migodela mfanyabiashara wa eneo hilo amesema upatikanaji wa wateja umekuwa  mgumu na hasa mvua zinaponyesha kutokana na barabara kuwa na makorongo hatarishi na kuwa adha hiyo inadumaza hata hali ya uchumi.

Aidha Judith amesema hali huwa ngumu pindi wanapopatwa na wagonjwa - kwani magari hushindwa kufika katika mtaa huo jambo ambalo hunawalazimu kumbeba mgonjwa hadi eneo lilipoegeshwa gari.

Naye Fabian Sanga mwenye gari amesema namna ya kupita katika mtaa huo ni shida, kwani hulazimika kuliacha gari umbali mrefu kutokana na mashimo yaliyopo katika mtaa huoambapo Fabiani ameuomba uongozi husika uchukue jukumu la kuwaondolea adha wananchi hao.


Diwani wa kata ya Boma ulipo mtaa huo wa Wambi “B’Julius Kisoma amekiri kuitambua changamoto hiyo ya barabara kwa wakazi wake wa mtaa wa Wambi “B”na kuwa kuna mpango wa kuifanyia marekebisho barabara hiyo na bajeti kupitia Tarura imeshapangwa.

Kisoma amesema matengenezo ya barabara hiyo yatawalazimu baadhi ya wananchi nyumba zao kubomolewa na kuwataka wakazi wa eno hilo ambao nyumba zao zipo njea ya utaratibu waanze kujiandaa, na kuwa kupitia Wakala wa barabara mjini na Vijijini “TARURA” kuna uhakika wa barabara hiyo kufanyiwa matengenezo.
 
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri Willium amesema  kuna mpango mkubwa wa kuzifanyia ukarabati na matengenezo barabara mbalimbali za Wilaya hiyo ya Mufindi zikiwemo barabara za  Halmashauri ya mji wa Mafinga.

Aidha Jamhuri amesema katika makisio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2018/ 2019 Halmashauri ya mji wa Mafinga ilitenga kiasi cha shilingi milioni 830 na tayari Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 356 sawa na asilimia 42 kwa ajili ya utengenezaji wa barabara mbalimbali za mji huo wa Mafinga.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Mufindi amesema barabara ya Mtaa wa Wambi “B” kwa Malingumu inasubiri mkandarasi aweze kuendelea na kazi kupitia fedha hizo walizozipokea, lengo likiwa ni kurekebisha barabara zote zenye changamoto Wilayani humo.

Hata hivyo Jamhuri amesema lengo la kuyatambua maeneo mbalimbali yaliyo korofi ni kutaka wananchi wake waweze kusafiri na kusafirisha mali na mizigo kwa uhakika na tayari maeneo mengine yameanzwa kutengenezwa, ambapo Jamhuri amewataka wananchi wasiwe na wasiwasi kwakuwa mambo yatakuwa mazuri siku za hivi karibuni.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More