Na Jumia Travel Tanzania
Zimebaki takribani wiki tatu kabla ya sikukuu ya Pasaka kusherehekewa duniani kote, je umeshafahamu utakwenda kupumzika wapi?
Pasaka ni miongoni mwa sikukuu zinazopendwa na watu wengi kwa sababu husherehekewa kwa takribani wiki moja. Wakati wa sherehe hizi watu huitumia fursa hiyo kwa kufanya mapumziko ya muda mfupi kabla ya kurejea kwenye shughuli zao za kila siku.
Katika kukusaidia sehemu za kwenda kutembelea sikukuu hii, Jumia Travel imekukusanyia hoteli tano za kuvutia zilizopo pembezoni mwa Tanzania ambazo unaweza kwenda kupumzika kipindi cha likizo hii fupi.
Lupita Island Lodge. Ni hoteli ya kuvutia na tulivu inayopatikana kwenye kisiwa kinachomilikiwa na mtu binafsi ndani ya ziwa Tanganyika. Hoteli hii ina kiwanja binafsi cha ndege na boti ambazo huwachukua wageni kutoka nchi kavu mpaka kisiwani. Hii ni sehemu ambayo unapaswa kwenda kwa ajili ya mapumziko kwa sababu hata namna ya muundo wa vyumba na mazingira yake yamewekwa kumpatia mtu utulivu na usiri akiwa mapumzikoni. Miongoni mwa shughuli za kuvutia ukiwa kisiwani hapa ni pamoja na kutembelea kijiji cha wavuvi, kutalii ziwani kwa kutumia boti na burudani za maonyesho ya kiasili kutoka kwa wanakijiji.
Katuma Bush Lodge. Ikiwa inapatikana kwenye Hifadhi ya Taifa ya Katavi, hoteli hii imejengwa katika mtindo wa kuvutia na kustarehesha kwa kutumia mahema. Eneo hili linatoa wasaa mzuri kwa wateja kutembelea mbuga yenye mandhari nzuri ya uwanda wa Katisunga. Kwa kuongezea, ni sehemu nzuri kwa watalii ambao wangependa kutembelea na kujionea mazingira mapya tofauti na yale waliyokwishayazoea.
Wag Hill Lodge & Spa. Hoteli ina mazingira tulivu na vifaa vya kisasa, sehemu kwa ajili ya michezo ya watoto na mandhari nzuri ya Ziwa Victoria, inafaa zaidi kwa mapumziko ya kifamilia na watalii wanaotafuta sehemu nzuri ya kustarehe. Inapatikana kwa mwendo wa dakika 30 kwa kuendesha gari kutokea jijini Mwanza.
Kigoma Hilltop. Ikiwa ni kituo cha kuvifikia kwa wepesi vivutio vya kitalii katika ukanda wa Magharibi, hoteli hii ya kisasa imejengwa mbali kidogo na mji, kwenye eneo kubwa la milima linalotazamana na Ziwa Tanganyika. Ukiwa hotelini hapa utafurahia mandhari nzuri ya kuvutia ya Ziwa Tanganyika, lenye sifa ya urefu na kina kirefu Afrika na duniani, kutoka kwenye kila chumba. Shughuli za kitalii zipo lukuki mkoani Kigoma kama vile safari za boti ziwani, kupiga mbizi ziwani, kutalii miji ya kihistoria ya Ujiji na Livingstone pamoja na safari ya siku nzima ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Gombe.
Kungwe Beach Lodge. Ni hoteli ya kifahari yenye ufukwe wa kuvutia inayopatikana kwenye Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale. Ukiachana na mazingira tulivu na vyakula mbalimbali, mgeni anaweza kufurahia shughuli kama vile ziara ya kwenda kuwaona sokwe, kutazama ndege wa mwituni, kutalii mbugani, safari ya boti ziwani, uvuvi, pamoja na matembezi binafsi kwenye fukwe safi pembezoni mwa Ziwa Tanganyika.
Maeneo ya kutembelea ni mengi na yanafikika kwa urahisi zaidi na gharama nafuu endapo utaanza kufanya maandalizi mapema. Sikukuu zinakaribia, naamini miongoni mwenu mtakuwa na mapumziko mafupi. Hivyo ni vema kukitumia kipindi hiko kufanya kitu ambacho kitaacha kumbukumbu katika mwaka huu. Unaweza kufahamu mengi zaidi juu ya sehemu hizo kupitia mtandao wa Jumia Travel.
0 comments:
Post a Comment