Wednesday, March 7, 2018

MADINI NI MALI YA WATANZANIA SIO WAWEKEZAJI WA KIGENI: BITEKO

Naibu waziri Wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo wakati akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Nyang'wale iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hivyo Mhe Hamim Gwiyama akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita Leo 6 Machi 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Naibu waziri Wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisalimiana na baadhi ya watendaji katika Wilaya ya Nyang'wale mara baada ya kuzuru wilayani Nang'wale akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita Leo 6 Machi 2018.
Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Nyang'wale iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hivyo Mhe Hamim Gwiyama ikimsikiliza kwa makini Naibu waziri Wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita Leo 6 Machi 2018.
Naibu waziri Wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko (aliyesimama) akielezea mikakati ya wizara hiyo wakati alipozuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Geita Leo 6 Machi 2018, Kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Nyang'wale Mhe Hussein Nassor Amari Kasu, na Mkuu wa Wilaya ya Nyang'wale Mhe Hamim Gwiyama

Na Mathias Canal, Geita

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli tangu ianze utendaji wake imejipambanua wazi kuwa rasilimali zote za nchi ikiwemo madini ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa hivyo ni Mali ya watanzania wenyewe sio wawekezaji wa kigeni.

Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusisitiza kuwa katika rasilimali Madini Taifa halipaswi kukurupuka kuyachimba kwa kuwa uwezo wa kitaaluma na kiteknolojia kuwezesha kuyachimba na kuyafaidi kama Taifa ulikuwa mdogo kwa mantiki hiyo, Baba wa Taifa akaenda mbali zaidi kwa kuagiza madini yasichimbwe hadi hapo Taifa litakapokuwa na uwezo wa kuyachimba ili watanzania waweze kunufaika ipasavyo.

Hayo yamebainishwa na Naibu waziri Wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko Leo 6 Machi 2018 wakati akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Nyang'wale iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya hivyo Mhe Hamim Gwiyama akiwa katika ziara ya kikazi Wilaya ya Nyang'wale Mkoani Geita.

Mhe Biteko alisema kuwa Mwalimu kwa wakati huo alijua fika kuwa Tanzani a ikifungua milango ya kuchimba madini bila Taifa  kujenga uwezo imara wa kufanikisha lengo hilo ipasavyo, wataalamu na wafanyabiashara au wale wanaoitwa wawekezaji kutoka nje, ilimradi wanazo fedha nyingi; watalilalia Taifa na kuwadanganya watanzania na hatimaye kuweza kufaidika zaidi kutokana na rasilimali madini.

Alisema kuwa Kwa mtazamo huo Rais Magufuli, aliamua kuweka mbele utaifa kuliko maslahi binafsi kwa kuifufua sheria ya Madini ya mwaka 2010 iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2017 ili kuiyafanya rasilimali Madini kuwa na manufaa kwa watanzania wenyewe kuliko ilivyokuwa awali.

"Mimi nataka niwaambie kuwa rasilimali madini ni mali ya Taifa letu au kwa maneno mengine ni mali ya Watanzania; na viongozi (kwa ngazi zote) tumepewa dhamana tu ya kusimamia na kuhakikisha Taifa letu linanufaika kutokana na uchimbaji madini, na si vinginevyo" Alisema Biteko

Aliongeza kuwa Taifa linaweza kuendelea zaidi endapo kwa wachimbaji kwa pamoja watakubali kufuata sheria na taratibu za uchimbaji huku wakiunga mkono juhudi za serikali kwa kulipa kodi ili kuwa na mafanikio wezeshi kwa watanzania wote.

Kwa upande wake Mbunge Wa Jimbo la Nyang'wale Mhe Hussein Nassoro Amari Kasu alisema kuwa Katika Wilaya hivyo serikali bado inapoteza kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya kutowarasimisha na kuwapa leseni Wachimbaji wadogo.

Aidha, aliiomba serikali kuwapatia leseni Wachimbaji wadogo kupitia vikundi vyao walivyovianzisha ili kurahisisha ukusanyaji Wa mapato sambamba na mafanikio ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake.

MWISHO.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More