Wananchi wanaozunguka Shamba la Miti Sao Hill wameendelea kunufaika kielimu na kiuchumi kupitia ushiriki wao katika shughuli za uchukuaji miche ya miti zinazofanyika katika bustani za miche zilizopo Tarafa ya Kwanza Irundi na Tarafa ya Tatu Ihalimba.
Shughuli hizo ni sehemu ya mpango endelevu wa upandaji miti unaotekelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kuendeleza misitu ya kupandwa, kuongeza uzalishaji wa rasilimali za misitu na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Said Singano, alisema uchukuaji wa miche unafanyika kwa kuzingatia taratibu na kanuni za kitaalamu ili kulinda ubora wa miche.
“Tunasisitiza miche ichukuliwe kwa uangalifu mkubwa ili isiharibu mizizi, kwa sababu ubora wa miche ndiyo msingi wa mafanikio ya upandaji miti mashambani,” alisema Singano.
Shughuli hizo pia zimeongeza uelewa wa wananchi kuhusu mchango wa Shamba la Miti Sao Hill katika uhifadhi wa mazingira, mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na upatikanaji endelevu wa mazao ya misitu kwa manufaa ya Taifa.
Mmoja wa wananchi walioshiriki zoezi hilo, Bw. Joshua Ng'umbi kutoka Kijiji cha Igowole Wilaya ya Mufindi, alisema ushiriki wake umemsaidia kuongeza kipato na kupata ujuzi mpya katika shughuli za misitu.
“Mbali na kupata ajira, nimejifunza kuchagua miche bora na namna sahihi ya kupanda miti ili iweze kuota vizuri na kukua kwa ubora unaoweza kuleta kipato kizuri wakati wa uvunaji,” alisema Bw. Joshua.
Kwa ujumla, zoezi la uchukuaji miche katika Tarafa za Irundi na Ihalimba limeendelea kuleta manufaa makubwa kwa Shamba la Miti Sao Hill na wananchi kwa kuimarisha juhudi za upandaji miti, kutoa ajira na kukuza uelewa wa masuala ya misitu na uhifadhi wa mazingira.






Sunday, January 11, 2026
mwangaza wa hbari







