Friday, October 24, 2025

OSHA YADHAMIRIA KUONGEZA UELEWA WA WADAU KUPITIA VYAMA VYA WAFANYAKAZI

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akiwasilisha hotuba yake katika hafla ya kuhitimisha kikao kazi cha siku mbili cha viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Kibaha Mkoani Pwani.
Mwenyekiti na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam (Brendan Maro na Sara Rwezaula-Kulia) wakimpokea Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alipowasili Kibaha, Pwani kwa ajili ya kufunga kikao kazi cha Viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la OSHA, Bi. Beatrice Lengereri.
Mkufunzi wa OSHA, Bw. Simon Lwaho, akiwasilisha mada kuhusiana na masuala ya usalama na afya kazini katika kikao kazi cha viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani
Viongozi wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam wakifuatilia mada mbalimbali kuhusiana na masuala ya usalama na afya mahali pa kazi katika kikao kazi chao kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wenyeviti na makatibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam mara baada ya kuhitimisha kikao kazi chao kilichofanyika Kibaha Mkoani Pwani
Na Fredy Mgunda.

Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wa Mkoa wa Dar es Salaam wapatao 180 wamepatiwa mafunzo ya awali ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwawezesha kuzishauri menejementi za Taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi na hivyo kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Mafunzo hayo yaliyowahusisha wenyeviti na makatibu wa matawi yote 90 ya TUGHE ya Mkoa wa Dar es Salaam, yamefanyika katika kikao kazi cha siku mbili Kibaha Mkoani Pwani ambapo viongozi wapatao 180 wameshiriki.

Pamoja na masuala mengine, mada mbalimbali zinazolenga kujenga uelewa wa jumla kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi zimewasilishwa na wataalam wa OSHA. Mada hizo ni pamoja na; Dhana ya Usalama na Afya mahali pa kazi, Uwakilishi na Kamati za Afya na Usalama mahali pa kazi, Mifumo ya Usalama na Afya mahali pa kazi pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi.

Wawasilishaji wa mada kutoka OSHA, Bw. Simon Lwaho na Moteswa Meda wamesisitiza washiriki kuwahamasisha wafanyakazi wenzao katika sehemu za kazi kujifunza kanuni bora za usalama na afya kutegemeana na shughuli zao za kila siku ili kupata mbinu za kujilinda dhidi ya vihatarishi mbalimbali vya magonjwa na ajali mahali pa kazi.

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha kikao kazi cha viongozi hao, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda, aliyekuwa Mgeni Rasmi wa hafla ya kufunga kikao kazi hicho, amesema viongozi hao wanayo nafasi muhimu katika kushawaishi menejimenti za Taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi ili kuleta ustawi wa wafanyakazi. 

“Kupitia kikao kazi hiki tumewaeleza wenzetu wa TUGHE jitihada za serikali katika kuimarisha afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi ambapo mbali na kuiwezesha OSHA kusimamia uzingatiaji wa taratibu za usalama na afya, masuala haya yamejumuishwa katika kanuni za kudumu za utumishi wa umma. Aidha, uzingatiaji wa masuala ya usalama na afya unaangaliwa katika ukaguzi wa CAG pamoja na Tume ya Utumishi wa Umma,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA. 

Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA nchini, Bi. Mwenda, ameahidi kuendelea kushirikiana na TUGHE pamoja na vyama vingine vya wafanyakazi katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi nchini wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na kanuni bora za usalama na afya zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao ya msingi katika hali ya ya usalama na kubakia na afya njema.
Mwenyekiti wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Komredi Brendan Maro ameielezea OSHA kama mdau muhimu katika utekelezaji majukumu ya chama chao.
 
“Tunawashukuru sana OSHA kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitupatia katika utekelezaji wa majukumu yetu hususan suala la kutoa elimu kwa wanachama wetu ambao ni wafanyakazi,” amesema Komredi Maro. 

Akitoa neno la shukrani, mwakilishi wa washiriki wa mafunzo hayo, Bi. Norbetha Sanga ambaye ni Katibu wa TUGHE Tawi la Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) amesema mafunzo ya usalama na afya ni muhimu kwa wafanyakazi na waajiri ili kuwa na uzalishaji wenye tija.



Tuesday, October 7, 2025

SERIKALI YAENDELEA KUWAUNGA MKONO WAKULIMA WA PAMBA KASULU

 Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu Serikali inaendelea kuleta unafuu kwa wakulima wa zao la pamba wilayani Kasulu kwa kuwapatia pembejeo muhimu kama mbegu, viuatilifu na vinyunyizi, hatua iliyochochea kilimo chenye tija na matokeo chanya.

Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Theresia Mtewele, amesema maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyoanzishwa mwaka 2019 yanalenga kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa zao hilo kama chanzo kikuu cha kipato kwa wakulima wadogo na wafugaji vijijini
Mkuu wa wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu Serikali inaendelea kuleta unafuu kwa wakulima wa zao la pamba wilayani Kasulu kwa kuwapatia pembejeo muhimu kama mbegu, viuatilifu na vinyunyizi, hatua iliyochochea kilimo chenye tija na matokeo chanya.


Na Fredy Mgunda 


Serikali imeendelea kuleta unafuu kwa wakulima wa zao la pamba wilayani Kasulu kwa kuwapatia pembejeo muhimu kama mbegu, viuatilifu na vinyunyizi, hatua iliyochochea kilimo chenye tija na matokeo chanya.


Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amesema hayo leo Jumanne, Oktoba 7, 2025, katika Kata ya Asante Nyerere, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyokwenda sambamba na uzinduzi wa msimu mpya wa zao hilo kwa mwaka 2025/2026.


Amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa Serikali, wanunuzi na vyama vya msingi kujadili maendeleo ya zao hilo na kuweka mikakati ya kuliboresha zaidi.


 Aidha, amewataka wananchi kutumia kipindi hiki cha kampeni kusikiliza sera za wagombea wa vyama mbalimbali ili siku ya uchaguzi, Oktoba 29, watumie haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Theresia Mtewele, amesema maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyoanzishwa mwaka 2019 yanalenga kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa zao hilo kama chanzo kikuu cha kipato kwa wakulima wadogo na wafugaji vijijini.


Mkulima wa Pamba, Joel Kingi, ameishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuhamasisha kilimo hicho, akieleza kuwa idadi ya wakulima imeongezeka kutoka 50 hadi kufikia 1,000 kutokana na upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu.


Awali, Mkaguzi wa Pamba wa Wilaya hiyo, Michael Kiliga, amesema wilaya inashirikiana na vyama vya ushirika (AMCOS) nane kusambaza pembejeo kwa wakulima bure, hatua inayochangia kuimarisha uzalishaji wa zao hilo.

CCM WAFANYA BONANZA KUHAMASISHA WANANCHI KUSHIRIKI UCHAGUZI KWA AMANI

 
Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda,mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Richard Kasesela kwa pamoja walihimiza kufanya mazoezi kila siku na kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu 
Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda,mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Richard Kasesela kwa pamoja walihimiza kufanya mazoezi kila siku na kupiga kura siku ya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu 

Na Fredy Mgunda.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeandaa Bonanza Maalum katika Jimbo la Segerea, mkoani Dar es Salaam, kwa lengo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, kwa njia ya amani na utulivu.


Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Pius Chatanda, ambaye aliwataka wananchi kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa kupiga kura kwa amani, akisisitiza kuwa kiongozi anayechaguliwa leo ndiye atakayekuwa na mamlaka ya kuleta maendeleo kwa miaka mitano ijayo.


“Kupiga kura ni haki ya msingi kwa kila Mtanzania. Tuchague viongozi wanaotuletea maendeleo ya kweli,” alisema Chatanda.


Akimnadi mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Chatanda alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imeitekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa asilimia 100, na hivyo anastahili kupewa tena ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.


Aidha, alitoa wito kwa wananchi kumchagua mgombea wa CCM katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani ili kuimarisha juhudi za maendeleo nchini.


Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, alisisitiza kuwa mojawapo ya sera zake ni kuhamasisha mazoezi ya mara kwa mara kwa wananchi, ili kuboresha afya ya mwili na akili.


“Afya bora ni msingi wa maendeleo. Tukifanya mazoezi tutakuwa na nguvu za kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa,” alisema Kamoli.


Kamoli aliwaomba wakazi wa Segerea kumpigia kura nyingi pamoja na kumpa kura ya kishindo Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili kuendeleza kasi ya maendeleo katika jimbo hilo.


Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni za CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kasesela, aliwataka wananchi kupuuza wanasiasa na wanaharakati wanaotumia mitandao ya kijamii kuchochea vurugu na hofu wakati huu wa uchaguzi.


“Wachochezi wengi wapo nje ya nchi. Vurugu zikitokea, ni Watanzania waliopo hapa ambao watateseka. Amani ni tunu ya taifa letu,tuilinde,” aliongeza Kasesela.


Katika bonanza hilo, wananchi walishiriki katika michezo mbalimbali, burudani, na kupata elimu juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa njia ya amani.

Sunday, October 5, 2025

MNEC KASESELA AWASIHI WATANZANIA KUSOMA VITABU VYA DINI

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Dar es Salaam, Richard Kasesela, amewataka Watanzania kumuabudu Mwenyezi Mungu kila wakati ili waweze kupata amani ya moyo na nafsi.
Baadhi ya waumini wa dini ya wananchi waliohudhuria kongamano la waislamu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu lilofanyika mlimani city jijini Dar es salaamBaadhi ya waumini wa dini ya wananchi waliohudhuria kongamano la waislamu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu lilofanyika mlimani city jijini Dar es salaam


Na Fredy Mgunda 

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) na Mratibu wa Kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Dar es Salaam, Richard Kasesela, amewataka Watanzania kumuabudu Mwenyezi Mungu kila wakati ili waweze kupata amani ya moyo na nafsi.


Akizungumza katika kongamano la Waislamu kuelekea uchaguzi mkuu, Kasesela alisema ni muhimu kwa wananchi kusoma vitabu vya dini mara kwa mara, kwani vinafundisha maadili mema na kuleta baraka katika kazi zao za kila siku.


"Vitabu vya dini vinatufundisha subira, heshima na upendo – misingi ambayo ni muhimu katika maisha na maendeleo ya taifa," alisema Kasesela.


Aidha, aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu ya kiroho sambamba na mafunzo ya mbinu za kujikwamua kiuchumi, ili wananchi waweze kujitegemea na kuboresha maisha yao.


Katika hatua nyingine, Kasesela aliwahimiza wananchi wote kumpigia kura kwa wingi Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa amefanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo katika kipindi chake cha uongozi.


"Ni wajibu wetu kuonyesha shukrani kwa kumpigia kura Dkt. Samia tarehe 29 Oktoba. Tuonyeshe mshikamano wetu kwa kupitia sanduku la kura," alihitimisha Kasesela.

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More