Na Fredy Mgunda, IRINGA
MDAU mkubwa wa michezo mkoani Iringa Michael Mlowe amewataka wadau kuichangia timu ya soka ya Lipuli kuweza kufanya vyema katika mchezo wake dhidi ya Yanga utakaopigwa Jumamosi hii katika dimba la Samora.
Akizungumza na Tanzania Daima Michael Mlowe, ‘Kasonzo’ alisema kuwa kutokana na timu kukabiliwa na ukosefu wa wadhamini hakuna budi wanachama, wadau na wapenzi wa mpira wanaoipenda timu ya Lipuli kujitokeza kwa wingi ili kuweza kupata matunda wanayohitaji katika soka la mkoa wa Iringa na Nyanda za Juu kusini.
Mlowe ambaye ameanzisha utaratibu wa kuchangia timu mbalimbali kupitia makundi mbalimbali ya mitandao ya Kijamii hasa wa Whatsup alisema kuwa mpira wa miguu una mahitaji makubwa kuliko watu wanavyodhani ili kufikia mafanikio.
Alisema kuwa endapo watu wengi watajitokeza kuichangia timu ya Lipuli inayoshiriki ligi kuu soka Tanzania Bara (VPL) wachezaji wa timu hiyo wana morali kubwa ya kuleta ushindi dhidi Yanga ambayo katika mechi ya Ufunguzi walifanikiwa kutoka nayo sare ya bao 1 – 1 huku Yanga wakisawazisha kwa tabu haswa.
Alisema kuwa endapo watu wengi watajitokeza kwa wingi kuweza kuichangia Lipuli itakuwa mwanzo mzuri wa wadhamini kuweza kujitokeza kuidhamini timu hiyo inayoshika nafasi ya 7 katika ligi kwa kuwa mwenendo wake ni mzuri zaidi kuliko ambavyo watu wengi waliichukulia hapo mwanzo.
"Mchezo wa soka una mahitaji makubwa sana kwa sasa hivyo ili timu iweze kufanya vyema misaada mbalimbali inahitajika hasa kwa timu ambayo haina vyanzo vya mapato hali inayoleta ugumu kwa wachezaji kufanya vyema lakini endapo wadau watajitokeza kwa wingi hasa kuelekea mechi na Yanga tujitokeze kuichangia timu" alisema
Aliongeza kuwa licha ya ushabiki alionao kwa Yanga lakini safari hii lazima timu ya Lipuli iondoke na ushindi katika uwanja wa nyumbani.
0 comments:
Post a Comment