Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi ameishauri Serikali kuwapa vyeti au nakala ya vyeti vya kidato cha nne na sita watu ambao kwa namna moja au nyingine walipotelewa na vyeti hivyo.
Chumi alitoa ushauri huo kufuatia majibu ya Serikali kuwa imekuwa vigumu kuwapa vyeti watu waliomaliza masomo kabla ya mwaka 2009 kwa madai kuwa vyeti vya wakati huo havikuwa vinawekwa picha ya mhitimu.
Mbunge huyo alieleza kuwa, ili kuwaondolea usumbufu waliopoteza vyeti, serikali ikishathibitisha kuwa muhusika ndio mtu sahihi, basi apewe japo nakala ya cheti kama wanavyofanya Vyuo Vikuu.
Awali katika swali lake la msingi, Chumi alitaka kufahamu utaratibu unaotumika kwa mtu aliyepoteza cheti na kwanini kumekuwa na ucheleweshaji wa huduma hiyo kwa watu ambao wameomba ajira au nafasi za masomo.
'Unakuta mtu kaomba ajira au nafasi ya kuendelea na masomo, anajaza fomu Baraza la Mitihani ili cheti kitumwe sehemu husika, lakini mara nyingi NECTA wanachelewa kuwasilisha cheti na hivyo kuwakosesha watu nafasi walizoomba' alihoji Chumi na kusisitiza kuwa, wahusika wapewe japo nakala ya cheti.
Akijibu, naibu Waziri wa Elimu William Ole Nasha alisema kuwa NECTA baada ya kupokea maombi huyashughulikia ndani ya wiki nne kuyatuma yanakohitajika.
'Hata hivyo niseme wazi kuwa hakuna linaloshindikana, Serikali inachukua ushauri wa mbunge na kuona namna bora ya kulishughulikia jambo hili'. Alifafanua Ole Nasha.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na utitiri wa matangazo ya watu waliopotelewa vyeti, lakini pia baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kwanini baada ya kujiridhisha, Baraza la Mitihani lisiwape japo nakala za vyeti.
Chumi alisema kuwa, mfumo wa sasa unawakosesha fursa za ajira na nafasi za masomo waliopotelewa vyeti hasa pale NECTA inapochelewa kuwasilisha maombi yao kule kunakohusika.
0 comments:
Post a Comment