Kampuni ya uchunguzi na utafiti wa madini, Helium One, ambayo kwa sasa inafanya utafiti wa gesi ya heliamu mkoa wa Rukwa imegundua kuwapo kwa futi za ujazo bilioni 98.9 za gesi hiyo katika maeneo iliyokwishafanyia uchunguzi.
Hayo yalielezwa katika warsha ya siku moja iliyofanyika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, na kuratibiwa na Idara ya Jiolojia ya chuo hicho, Helium One na Chuo Kikuu cha Oxford.
Akizungumza katika warsha hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Helium One, Thomas Abraham-James, alisema kwamba kampuni yao imetafuta leseni 23 za uchunguzi na kwamba nyingine tatu zimeombwa.
Alisema kwamba leseni hizo zote zinamilikiwa na kampuni hiyo kwa asilimia 100 na kwamba ina haki za kipekee za gesi hiyo ya heliamu .
Pamoja na kutoa taarifa hiyo,alisema lengo la kuwa na warsha ni kuwaita wataalamu na wadau mbalimbali wa hapa nchini na kimataifa kubadilishana uzoefu na taarifa zilizopo kuhusu gesi hiyo na kuangalia fursa zinazoambatana na uwapo wa gesi hiyo katika harakati za kitaifa za kuwa na taifa la viwanda.
“Helium One inaamini kwamba kuna fursa kupitia utafiti huu kuweza kutengeneza utaalamu wa kiwango cha juu na utaalamu wa hapa nchini juu ya uendelezaji wa gesi hiyo. Tutaendelea kujenga uhusiano na Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuweza kubadilishana elimu, kutoa mafunzo kwa wanafunzi na maofisa wizara ya madini na kutengeneza mpango wa ufadhili wa masomo,” alisema.
Kwa mujibu wa Abraham-James, warsha hiyo ilihudhuriwa na wanasayansi waandamizi wa gesi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza na Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam,UDSM, watu wenye mamlaka na maamuzi, wadau wa maendeleo, watengeneza sera kutoka serikalini, watafiti na sekta binafsi.
Aidha kampuni hiyo imetoa ufadhili wa masomo ngazi ya shahada ya uzamili kwa wanafunzi wawili wa UDSM kusoma katika Chuo Kikuu cha Oxford , ikiwa ni sehemu ya kuingiza utaalamu wa hali ya juu wa kisayansi kwa watanzania na pia kuendeleza uhusiano mzuri kati ya Helium One na UDSM.
Wakati wa warsha hiyo, Profesa John Machiwa, akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo, Prof Cuthbert Kimambo, alisema kwamba jukwaa hilo ni jema kwa wanafunzi, wakufunzi na Chuo kizima kutafuta njia ya kuona namna ya kushirikiana na Helium One.
“Tunaweza kufanyakazi pamoja na kunoa taaluma na pia kupata utaalamu katika utafiti wa heliamu uzalishaji na usafirishaji wake,” alisema.
0 comments:
Post a Comment