Wednesday, January 17, 2018

ZAIDI YA WANAFUNZI ELFU SABA WAANDIKISHWA DARASA LA KWANZA GEITA MJINI HUKU TATIZO LA UHABA WA MADARASA LIKIWATESA WANAFUNZI NA WALIMU.

Mwl Risa Nkya akiwa darasani akiwafundisha wanafunzi wa darasa la tatu  kwenye shule ya Msingi Nyankumbu iliyopo Halmashauri ya mji wa Geita huku wanafunzi wakiwa ni wengi zaidi darasani hali ambayo imepelekea wengine kukaa chini. 

Nje ya shule ya Msingi Nyankumbu baadhi ya madawati yakiwa yamebebanishwa kutokana na uhaba wa madarasa Shuleni Hapo.

Wanafunzi wakiwa darasani katika hali ya Mlundikano mkubwa zaidi.

Na,Joel Maduka.Geita.

Afisa elimu wa shule za msingi katika Halmashauri ya mji wa Geita Bw Yesse Kanyuma amesema Idara yake imeandikisha wanafunzi 7 713 wa Darasa la kwanza.

Bw Kanyuma alisema  malengo ni kuandikisha wanafunzi  10109 na kwamba anaamini malengo hayo yatafikiwa kutokana na mwenendo wa uandikishaji.

“Zoezi la uandikishwaji linaendelea kwenye halmashauri yetu na hadi sasa tuna asilimia sabini na tisa (79%) hata hivyo bado tunamatarajio ya kuandikisha wanafuzi wengi zaidi  kutokana na kwamba zoezi hili linaendelea hadi mwezi March”Alisema Kanyuma

Hata hivyo mtandao huu umetembelea baadhi ya shule za msingi mjini Geita na kuzungumza na Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Nyankumbu Mwl Swalala David na Mwl Mkuu wa shule ya msingi Mbugani Florence Leonard ambao wamesema changamoto kubwa inayowakabili ni upungufu wa vyumba vya madarasa.

“Nina vyumba kumi na moja vinavyotumika lakini idadi ya wanafunzi ni zaidi ya elfu tatu na kitu ,mwaka jana nilikuwa na watoto elfu tatu na mia tano themanini na saba lakini vyumba ni hivyo hivyo aviongezeki kwa hiyo kilio kikubwa ni vyumba vya madarasa imefikia hatua tumeamua kutumia baadhi ya miradi tuliyonayo ili kujenga vyumba vitatu vya madarasa ingawa na vyenyewe havitoshi kutokana na wengi uliopo wa wanafunzi”Alisema Mwl Swalala.

Aidha Mwl Swalala ameendelea kusema pamoja na matatizo ya uhaba wa madarasa hata hivyo bado wanakabiliwa na tatizo la madarasa kuchakaa na kutengeneza nyufa hali ambayo ni hatarishi kwa wanafunzi ambao wanasoma kwenye madarasa hayo.

“Kutokana na wingi wa wanafunzi imekuwa ni kazi ngumu sana kwa mwalimu pindi anapofundisha kumpitia kila mwanafunzi na kumuelekeza hata hivyo pamoja na changamoto hizo walimu wameendelea kujitahidi kufundisha”Alisema Mwl Leornad

Hata hivyo kwa upande wake Mwl Risa Nkya alisema idadi kubwa ya wanafunzi madarasani kumekuwa kukiwanyima amani walimu wengi na kujikuta wakitimiza wajibu tu wakufundisha kwani hali ya mlundikano wa wanafunzi ni kubwa sanaa.

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Nyankumbu akiwemo Devid Cosmas na Devota John wameelezea kuwa hali ya mlundikano ni tatizo ambalo linaweza kuchangia kushusha kiwango cha cha Elimu kwani wamekuwa wakishindwa kusoma vizuri kutokana na wingi wa wanafunzi kwenye madarasa ambayo wanasomea hivyo wameiomba serikali pamoja na wadau kujitoa kwa dhati kutatua kero ya uhaba wa madarasa shuleni hapo.


0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More