Monday, January 15, 2018

MAMBO UNAYOTAKIWA KUYAFAHAMU KUHUSU MAPINDUZI YA ZANZIBAR


Na Jumia Travel Tanzania



Januari 12 ya mwaka huu wa 2018 Wazanzibari pamoja na Watanzania kwa ujumla watakuwa wakiadhimisha miaka 54 tangu kutokea kwa mapinduzi Visiwani Zanzibar mnamo Januari 12, 1964. Mapinduzi ambayo yaliyofanywa na wanamapinduzi wa kiafrika na kupelekea kuung’oa utawala wa kisultani na kiarabu visiwani humo na kuwa na utawala wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Pamoja na siku hii kuadhimishwa kila mwaka, bado kuna watu wengi hawafahamu mambo muhimu kuhusu historia ya Zanzibar na yaliyopelekea mpaka mapinduzi kutokea. Kutokana na umuhimu wa siku hii kwa vizazi vilivyopita, vya sasa na vijavyo, Jumia Travel imekukusanyia mambo muhimu ambayo huna budi kuyafahamu.



Ikiwa na historia ndefu ya utawala wa Kiarabu tangu mwaka 1698, Zanzibar ilikuwa ni sehemu ya nchi ya ng’ambo ya Oman mpaka ilipojitwalia uhuru wake mnamo mwaka 1858 na kuwa chini ya utawala wake wenyewe wa Kisultani.

 

Wakati wa utawala wa Sultani Ali Ibn Said mnamo mwaka 1890, Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Waingereza mpaka mwaka 1963 ilipowapatia wanzibar uhuru wao, ingawa haikuwahi kuwa chini ya utawala rasmi wa moja kwa moja wa dola ya Kiingereza.



Wananchi wa Zanzibar kwa kiasi kikubwa walikuwa ni mchanganyiko kutoka mataifa mbalimbali kama vile Waarabu, Wahindi, Waajemi, Washirazi na Waafrika, ambapo waarabu na wahindi ndio kwa kiasi kikubwa walikuwa wamehodhi ardhi na shughuli kuu na njia za biashara. Kadri muda ulivyozidi kwenda maingiliano baina ya watu wa mataifa hayo yalizidi kuongezeka kitu kilichopelekea utofauti baina yao kuanza kufifia.


Hata hivyo, walowezi wa Kiarabu kama wamiliki wa sehemu kubwa ya ardhi ya visiwani humo ndio walikuwa ni matajiri kuliko waafrika. Suala hilo pamoja na mambo mengine mengi ni miongoni mwa sababu zilizopelekea waafrika kuona sababu ya kufanya mapinduzi ili kuwa na utawala wa haki na usawa visiwani humo.



Kwa upande wa kisiasa, vyama vikuu visiwani Zanzibar vilikuwa vikiendeshwa na kuungwa mkono kulingana na utaifa (ukabila), kama vile Waarabu walikuwa wakitawala kwa sehemu kubwa ya chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) huku Waafrika ilikuwa ni Afro-Shirazi Party (ASP).

 

Baada ya Zanzibar kutwaliwa na utawala wa Kisultani wa Oman mnamo mwaka 1698, sehemu ya ardhi yote visiwani humo iligawiwa kwa wanafamilia wa Kifalme wa Oman, ambapo vizazi vyao viliendelea kuimiliki mpaka mwaka 1964.



Ingawa sio Waarabu wote walikuwa ni matajiri kama familia ambazo zilikuwa zikimiliki mashamba ya karafuu na minazi, hasira ambayo waliyokuwa nayo waafrika ambao walikuwa wakifanya kazi kwenye mashamba hayo ilipelekea kujisikia hali ya kubaguliwa kwenye ardhi yao wenyewe. Hususani kwa kisiwa kidogo kama cha Zanzibar ambapo ilikuwa ni rahisi kuona pengo na utofauti mkubwa kati ya familia tajiri za kiarabu zilizokuwa zinamiliki ardhi na vijakazi wao masikini wa kiafrika.

 

Harakati za kutaka uhuru Visiwani Zanzibar zilianza kutokana na vuguvugu za shughuli za kisiasa ambapo kwa kiasi kikubwa waafrika hawakuwa wanapata uwakilishi sawa na nafasi bungeni. Kuanzia mwaka 1961 na kuendelea kulianza kufanyika kwa chaguzi za kisiasa za kidemokrasia ambapo vyama vikuu vya ASP na ZNP vilikuwa vikichuana vikali.



Chama kilichokuwa kikiungwa mkono na waafrika wengi cha ASP kilikuwa kikiendelea kuungwa mkono na kukubalika miongoni mwa waafrika wengi. Katika maeneo mengi kulipokuwa kunafanyika chaguzi kilionekana kuungwa mkono ingawa matokeo ya uchaguzi yalipotoka yalikuwa yanaonyesha kushinda sehemu chache.



Sababu hiyo ambayo ilikuwa ikijirudia mara kwa mara kwenye kila chaguzi ndiyo iliyopelekea waafrika kuona haja ya kufanya mapinduzi. Mnamo Januari 12, 9164 mapinduzi yalifanyika visiwani Zanzibar na kumfanya kiongozi wa chama cha ASP, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kuwa Rais mpya na kiongozi wa nchi.



Mapinduzi hayo yalipelekea ukomo wa utawala wa kiarabu visiwani Zanzibar wa takribani miaka 200, hivyo kuifanya siku hiyo kusherehekewa kwa maadhimisho maalum na kuwa ni siku ya mapumziko ya kitaifa.  

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More