WIZARA
ya Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu imetaka wananchi kuepuka kampuni za
uwakala wa ajira nchini ambazo hutangaza nafasi za ajira huku zikiwataka
waombaji kulipia ili kusailiwa.
Msemaji
wa Wizara hiyo, Ridhiwan Wema jana alisema kampuni za namna hiyo
hawazitambui na hivyo hazina usajili wa kufanya shughuli hiyo nchini.
“Hizi
kampuni sisi hatuzitambui, mtafuta kazi hatakiwi kutozwa fedha
isipokuwa kampuni inaingia makubaliano na mwajiri ambaye amempa kazi ya
kumtafutia wafanyakazi,” alisema Wema.
Alitaka
wananchi wawe makini na wasikurupuke kutuma maombi kabla ya
kujiridhisha kama kampuni zimesajiliwa na ili kupata taarifa sahihi,
mwombaji anaweza kufika Wizara ya Kazi na kuuliza, kwa kuwa wao ndio
wasajili pia wakibaini uwepo wa kampuni hizo watoe taarifa wizarani na
Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Aidha,
aliwasihi wananchi hususan vijana, wasiwe wepesi kulipia gharama, kwa
sababu huduma ya ajira haipaswi kutozwa fedha kwa kuwa si haki kutoa
kazi kwa masharti ya kulipwa, hali ambayo inaashiria vitendo vya rushwa.
Wema
alibainisha kuwa kampuni zinazofanya shughuli za uwakala wa ajira
nchini zimesajiliwa na Wizara ambapo moja ya masharti yanayotakiwa
kuzingatiwa ni pamoja na kutowatoza waombaji wa nafasi za ajira
zinazotangazwa.
Alisema
kuna vigezo vingine pia vinavyozingatiwa, ili kukidhi usajili ambapo
huainishwa kwa majina na taarifa za mahali pa kudumu zilipo ofisi za
kampuni na kufahamu kama zimesajiliwa kwenye mamlaka husika, mfano
Brela, hayo yote ni kwa ajili ya kufanya urahisi wa kizifuatilia pindi
kunapozuka utata.
Aliongeza
kwamba vigezo vingine ni kujiridhisha kama ina wataalamu wa kutosha
kwenye masuala ya ajira, ambapo baada ya kujiridhisha husajiliwa na
kuzitangaza kwenye vyombo vya habari.
Wema
alitaka wananchi watambue kuwa kampuni zinazotangaza nafasi za ajira
huku zikitaka waombaji walipie fedha kwa ajili ya usaili si salama kwao,
hivyo wanatakiwa kuepukana nazo na kutoa taarifa.
Nuh
Yusuf ambaye ni Ofisa wa kampuni ya Zoom ambayo ni wakala wa ajira
nchini, alisema sababu kubwa ya kuendelea kwa utapeli wa mtandao ni
kukosekana kwa ushikiano wa karibu na vyombo vya sheria hususan Jeshi la
Polisi katika kudhibiti suala hilo.
“Tumejaribu
kufuatilia suala hilo TCRA kitengo cha TZ-CERT, tukashauriwa twende
Polisi na mmoja ambaye alipatwa na hilo tatizo, tulipofika kituo cha
Polisi cha Oysterbay hawakuonesha ushirikiano wowote,” alisema Yusuf.
0 comments:
Post a Comment