Mfanyabiasha
Leonard Materu (31) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka ya kutuma ujumbe wa kumtishia
Rais John Magufuli kupitia mtandao wa WhatsApp.
Materu
ambaye ni mkazi wa Moshi Bar Kwadiwani, alifikishwa mahakamani hapo
jana na kusomewa mashitaka yake na Wakili wa Serikali, Diana Lukondo
mbele ya Hakimu Mkazi Magreth Bankika.
Akisoma
mashitaka Wakili Diana alidai, mshitakiwa huyo amefunguliwa kesi hiyo
ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa WhatsApp chini ya
Sheria ya Mtandao ya mwaka 2015.
Ilidaiwa
kuwa, Julai 17, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Materu aliandika ujumbe
wenye lengo la kudanganya umma kupitia WhatsApp ukisomeka; “Magu ajiandae tunaenda kupindua mpaka Ikulu.”
Inadaiwa
kuwa maneno hayo yalikuwa na lengo la kumtishia Rais John Magufuli.
Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa alikana kutenda kosa hilo, na
upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika na kuomba
tarehe nyingine ya kutajwa.
Mshitakiwa
aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na
wadhamini wawili ambao kila mmoja alisaini hati ya Sh milioni tano. Kesi
itatajwa tena Septemba 20, mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment