Friday, September 23, 2016

Mhadhiri chuo kikuu mbaroni kwa kumkashfu Rais Magufuli

Idadi ya watu wanaokamatwa kwa tuhuma za kumkashfu Rais John Magufuli kupitia mitandao ya kijamii imezidi kuongezeka baada ya polisi kumkamata Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa (Muce), Dk Oscar Magava (48).

Dk Magava amekuwa mtu wa kumi kukamatwa na polisi katika kampeni za jeshi hilo kudhibiti uhalifu chini ya sheria ya uhalifu wa mtandaoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi alisema Dk Magava alikamatwa akiwa Sumbawanga na alirudishwa mkoani Iringa.

Mjengi alisema Septemba 15, mwaka huu walipata taarifa kuwa mhadhiri huyo anatumia mitandao ya kijamii kumkashfu Rais. Alisema waliamua kumsaka na walipopata taarifa kuwa Dk Magava amekwenda Sumbawanga waliwasiliana na polisi wa huko wakamkamata na kumrudisha Iringa.

Hata hivyo, Kamanda Mjengi hakuyataja maneno aliyotumia Dk Magava kumkashfu Rais kwa madai kuwa bado wanaendelea na uchunguzi na kwamba ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Kamanda Mjengi aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa kuitumia kwa ajili ya maendeleo na si kutukana wala kukashfu viongozi au watu wengine.

Watu mbalimbali wamekuwa wakikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la kumkashifu Rais au jeshi la polisi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More