Monday, September 5, 2016

Uhuru Kenyata Akanusha Kuwepo Mvutano Wa Kiuchumi Kati Ya Tanzania Na Kenya

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya Jumamosi alikanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba kuna mvutano baina ya Kenya na Tanzania.

Akizungumza mjini Mombasa wakati wa ufunguzi gati la makontena katika bandari ya Mombasa, Kenyatta alipuuzia maneno kwamba kuna mvutano wowote na badala yake akasema kuwa nchi hizo zinasaidiana.

Alisema anaona kwenye vyombo vya habari kwamba kuna “mgogoro baina yetu, lakini nataka kusema wazi wazi kwamba Kenya na Tanzania hazina mgogoro wowote baina yao,” alisema.

Kenyatta alisema uchumi wa nchi hizo mbili umefungana kwa miaka mingi na ni kwa ajili ya faida ya watu wa nchi hizo mbili.

Alitaja kufunguliwa kwa njia inayojulikana kama “northern frontier” ambayo itaunganisha bandari ya Mombasa kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania, hadi Bujumbura, Burundi – njia ambayo itafupisha urefu wa kutoka Bujumbura hadi Mombasa kwa kilomita 300 nzima.

“Afrika Mashariki haiko katika mashindano ya wenyewe kwa wenyewe,” alisema Kenyatta. “Afrika Mashariki inashindana na dunia. Tunataka kujaliana (pale penye mapungufu). Tunataka tutumie nguvu zetu ili kukua, kuendeleza na kuinua uchumi wetu,” alisema.

Kutokuwepo kwa Rais John Magufuli wa Tanzania katika mkutano wa hivi karibuni wa kimataifa na Tokyo mjini Nairobi kulizusha uvumi kuhusu uhusiano wa nchi za eneo hilo.

Kiongozi huyo wa Tanzania ametembelea Uganda na Rwanda tu tangu achukue madaraka Oktoba mwaka jana ukilinganisha na rais aliyemtangulia Jakaya Kikwete ambaye alikuwa akisafiri sana nchi za nje.

Rais Magufuli pia hakuhudhuria mikutano karibu mitano ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na mkutano wa shirika la biashara duniani na mikutano mikuu ya AU mjini Addis Ababa na ule wa Kigali Rwanda hivi karibuni.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More