Viongozi
wa vyama vya Siasa wametakiwa kuiga kwa vitendo uzalendo na moyo wa
kujitoa aliokuwa nao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
enzi za uhai wake ili kuliwezesha Taifa kupiga hatua kimaendeleo.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani mara baada kutembelea Kaburi na Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo wilayani Butiama.
Amesema
kuwa kumbukumbu za Baba wa Taifa zilizohifadhiwa vizuri katika
makumbusho hiyo zina mambo mengi ya kujifunza ambayo wanasiasa
wanatakiwa kuyafanya kwa vitendo hasa uzalendo kwa nchi, uvumilivu,
upendo na moyo wa kujitoa kwa dhati kuwatumikia wananchi.
“Kupitia
kumbukumbu hizi sisi watumishi wa Tume tumejifunza ukomavu wa
demokrasia aliokuwa nao Mwalimu Nyerere akiwa ndani na nje ya Bara la
Afrika, wengi wanadhani Demokrasia ni wakati wa uchaguzi tu, kumbe
demokrasia ni pamoja na kuheshimu watu wengine” Amesema Kailima.
Ameeleza
kuwa maisha aliyoishi Baba wa Taifa ni mfano wa kuigwa na viongozi na
watanzania wote hasa pale alipojitofautisha na viongozi wengi wa Bara la
Afrika alipoepuka tamaa ya madaraka na mali kwa manufaa ya taifa.
“Sote
ni mashahidi kupitia kumbukumbu zake tumeona mahali alipokuwa anaishi
mwalimu kabla hajajengewa nyumba na Jeshi kama Rais mstaafu wengi
walitegemea asingeishi katika eneo lile, kumbukumbu hii nzuri
aliyoiacha inatufundisha watanzania kuwa mwalimu aliitanguliza Tanzania
mbele kuliko maslahi yake binafsi” Amesisitiza.
Bw.
Kailima amebainisha kuwa NEC itaendelea kumuemzi Baba wa Taifa kwa
yale aliyoyafanya na kuyasimamia kwa manufaa ya taifa huku akitoa wito
kwa viongozi wa vyama vya Siasa wawe na kiasi na waridhike na vile
walivyonavyo.
“Suala
la kuridhika na kuwa na kiasi linapaswa kuzingatiwa, wanasiasa
wanapaswa kuwaheshimu wananchi wanaowachagua kupitia chaguzi
mbalimbali, matokeo yanapotoka kama ni sahihi basi wanasiasa
wakubaliane na maamuzi yao” Ameainisha Kailima.
Kwa
upande wake Mhifadhi wa Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere Bw. Jacob Thomas amesema kuwa watanzania wanayo mengi
ya kujifunza kupitia vitu alivyoviacha Baba wa Taifa ambavyo
vimehifadhiwa katika Makumbusho hiyo.
Amesema
kuwa maisha ya uadilifu aliyoishi enzi za uhai wake na mchango wake
katika kuiletea maendeleo Tanzania na Bara la Afrika vinapaswa kuenziwa
kwa nguvu zote na viongozi wa Tanzania.
“Ninyi
mliopata nafasi ya kuitembelea makumbusho hii mmejifunza vitu vingi
kumhusu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba alikuwa ni mtu wa namna
gani kwa viwango vya Afrika na dunia kutokana na kumbukumbu ya uadilifu
aliyoiacha ndani na nje ya mipaka ya Tanzania”
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani
akiwasili nyumbani kwa familia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere, Butiama Musoma akiwa ameambatana na watumishi wa NEC na
baadhi ya wajumbe wa mkutano wa ALAT kutoka maeneo mbalimbali kuzuru
kaburi la Baba wa Taifa, Mwitongo wilayani Butiama. Tume ya Taifa ya
Uchaguzi iko mkoani Mara kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani
(Kushoto) akisalimiana na Msemaji Mkuu na kiongozi wa familia ya Baba wa
Taifa Chifu Japhet Wanzagi (kulia) mara baada ya kuwasili eneo la
Mwitongo wilayani Butiama. Wa Pili kutoka Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya
Butiama Bi. Annarose Nyamubi.
Mkurugenzi
wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani
akiwasha mshumaa kwenye kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere eneo la Mwitongo, Butiama. Wengine wanaoonekana na baadhi ya
wajumbe wa mkutano wa ALAT na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC).
Mwongoza
wageni na Mhifadhi wa Makumbusho ya Mwalimu Nyerere Butiama, Jacob
Thomas akitoa maelezo kuhusu picha za kumbukumbu za Baba wa Taifa kwa
Mkurugenzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani na watumishi wa NEC
walioitembelea makumbusho hiyo eneo la Mwitongo, Butiama –Musoma.
0 comments:
Post a Comment