Kamati
ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), imeitisha kikao cha Baraza Kuu
la Uongozi Taifa, ili kumhoji mwenyekiti aliyerudishwa madarakani,
Profesa Ibrahim Lipumba.
Wakati
wajumbe wa baraza hilo wakijiandaa kukutana kesho visiwani Zanzibar
kutekeleza mpango huo, jana kutwa nzima, Profesa Lipumba alikuwa na
kikao kizito na walinzi wa chama hicho (Blue Guard) makao makuu ya chama
hicho Buguruni, Dar es Salaam.
Taarifa
iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Naibu Katibu Mkuu wa CUF
(Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui ilisema baraza hilo, linamtaka Profesa
Lipumba afike mbele ya kikao hicho ili ajieleze na kujitetea kwanini
asichukuliwe hatua za kinidhamu kutokana na kitendo chake cha kuvamia
ofisi za makao makuu na kusababisha uharibifu wa mali.
“Kamati
haijakubaliana na maoni na ushauri uliotolewa na Msajili wa Vyama vya
Siasa, Jaji Francis Mutungi juu ya Lipumba. Ilikutana jana (juzi) kwa
kikao cha dharura ofisi za Makao Makuu, Zanzibar na kujadili taarifa ya
msajili,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo, ilisema kamati pia ilijadili kitendo cha uvamizi wa ofisi za
Buguruni, kilichofanywa na Profesa Lipumba akiwa na kundi la vijana
ambao si wanachama wa CUF.
Alisema
baada ya kikao kupitia maoni ya msajili, kamati iliamua kukataa na
kupinga kwa hoja thabiti ushauri na maoni aliyoyapendekeza na badala
yake inaendelea kusimamia maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalumu Taifa
uliofanyika Agosti 21, mwaka huu.
“Katika
mkutano ule, wajumbe walikubali Lipumba kujiuzulu kama mwenyekiti wa
chama na katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa cha Agosti 28,
mwaka huu, waliridhia kuwasimamisha uanachama Lipumba, Magdalena Sakaya,
Maftaha Nachuma, Abdul Kambaya, Masoudi Mhina, Thomas Malima, Ashura
Mustafa, Kapasha H. Kapasha, Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa, Haroub
Shamis na kumfukuza uanachama Shashu Lugeye,” alisema.
Taarifa
hiyo, ilisema Katiba ya CUF haina kifungu chochote kinachompa mamlaka
Msajili wa Vyama vya Siasa kupokea rufaa kuhusiana na uamuzi wa vikao
vya chama na kubatilisha uamuzi wa vikao halali.
“Kutokana
na kitendo cha kuvamia ofisi za Buguruni na kusababisha uharibifu wa
mali za chama, kamati kwa mujibu wa ibara ya 85(5) na ibara ya 108 ya
Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la mwaka 2014 imeitisha kikao cha
Baraza Kuu la Uongozi Taifa Septemba 27, mwaka huu saa nne asubuhi ofisi
za Zanzibar.
“Kwa
mujibu wa Ibara ya 12 (6), (7) na (16) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 ,
toleo la mwaka 2014, Kamati imeandaa ajenda ya kumfikisha Lipumba mbele
ya Baraza Kuu na atatakiwa kujieleza na kujitetea kwa nini baraza
lisimchukulie hatua za kinidhamu kwa matendo yake aliyoyafanya jana
(juzi),” alisema.
Katika
taarifa hiyo, Mazrui alisema ibara hizo zinaeleza juu ya kulinda
heshima ya chama kwa kuwa na tabia njema, kutekeleza masharti ya Katiba,
kutii kanuni za sheria na sheria ndogondogo za serikali iliyoundwa
kihalali na.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba jana kutwa nzima alikuwa na kikao na walinzi wa chama hicho, (Blue Guard).
Pamoja
na mambo mengine, kikao hicho kilikuwa na ajenda mbili ikiwamo ya
kuimarisha ulinzi katika ofisi zote za chama na kujadili mali za chama
ambazo ni pamoja na magari saba na kompyuta zilizoibwa wakati wa vurugu.
Tamko la Kambaya
Pamoja
na hali hiyo jana Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya
Umma, Abdul Kambaya, alitoa tamko la kuwataka wanachama wa CUF kuwa
watulivu kwa ajili ya kukijenga chama hicho.
Alisema
pamoja na hali hiyo CUF ni taasisi na sio eneo la mtu fulani kwani
tamko la Naibu Katibu Mkuu CUF Zanzibar, Nassor Hamed Mazrui la kuukataa
ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa uliotolewa kwa mujibu wa Sheria
ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002 ni la upotoshaji.
“Kwa
mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2002, sehemu ya 20, tamko
la msajili ni uamuzi na si tu ushauri kama wanavyotaka kupotosha. Uamuzi
huu ni mzito kwa kiwango ambacho hata mahakama inaweza tu kuurejea
lakini si kuufuta (rejea ibara ya 20(2).
“Ieleweke
kwamba hii si mara kwanza msajili kufanya maamuzi kama haya. Mtakumbuka
kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wetu Ndugu James Mapalala alienda kwa
msajili baada ya kufukuzwa.
“Lakini
msajili alitoa uamuzi kwamba maamuzi yale yalikuwa sahihi Kwa kuwa
yalifuata katiba yetu ya CUF. Sasa iweje hawa wenzetu leo waseme kwamba
ule ni ushauri tu?,” alisema na kuhoji Kambaya ambaye ni mmoja wa wanachama waliosimamishwa na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi.
Alisema
kilichofanyika Vuga Zanzibar ni uasi wa hali ya juu, hivyo watakaa kama
chama kutafakari hatua za kuchukua baada ya kuzuia uasi na kile
alichodai mapinduzi haramu kwa chama hicho.
“Sasa
kazi yetu ni kujenga chama. Wenzetu walioendesha uasi wana hiari ya
kujirudi ili tuungane kufanya kazi ya ujenzi wa chama na kuhudumia
wananchi katika maeneo mbalimbali ambapo chama kimepewa ridhaa ya
kuongoza."
0 comments:
Post a Comment