Mchungaji wa kanisa la Umoja wa Makanisa ya Ubatizo Lucas Machibya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani ) kuhusu baadhi ya shughuli za uraghabishi katika kijiji cha Pandagichiza |
Na Krantz
Mwantepele ,Shinyanga
Si mara nyingi viongozi wa kidini hujihusisha
moja kwa moja na harakati za kisiasa ila wamekuwa mstari wa mbele kukemea
matendo yanayofanywa na wanasiasa. Hawafanyi hivyo kwa bahati mbaya ila kutokana
na nafasi yao katika jamii, hususani kuwaongoza waumini wao kwenda mbinguni.
Hata hivyo, hii haimaanishi hakuna
kabisa viongozi wa dini waioamua kujiingiza katika harakati za siasa ili kuleta
maendeleo ya watu kwa haraka na ufanisi. Mchungaji Lucas Machibya ni mmoja kati
ya viongozi wachache wa dini wanaoingia katika siasa.
Huyu ni mchungaji wa kanisa la Umoja
wa Makanisa ya Ubatizo lililopo katika kijiji
cha Pandagichiza chenye wakazi wanaokadiriwa 2,481, idadi kubwa ikiwa ni ya
wanawake wanaokadiriwa kufikia 1,476. Hiki ni moja ya vijiji vilivyopo wilaya
ya Shinyanga Vijijini, jimbo la Solwa.
Machibya ni mmoja wa wachungaji
waraghbishi toka mkoa wa Shinyanga ambao uraghbishi wao umepelekea wananchi
kumchagua kuwa mwenyekiti wa kijiji. Kujibainisha kwake kama mtu mwenye uwezo
wa kusimamia anachokiamini na kushawishi wananchi kutambua majukumu na haki zao
na jinsi ya kuzidai vimekuwa nguzo yake kubwa ya kukubalika.
Kama walivyo wananchi wengi wa kijiji
chake, yeye ni mkulima mdogo ambaye pia ni mwanachama wa Mtandao wa Wakulima
Wadogo Tanzania (MVIWATA). Kupitia mwaliko wa mkulima mwenzake, Elizabeth
Edward, Machibya amefanikiwa kupata maarifa ya uraghbishi na jinsi ya kufanya
uraghbishi; uwezo wa kuwashawishi na kuwahusisha ama kuwachokoza watu ili
waweze kujitambua na kutojiona wao ni wa jamii ya chini.
Sifa iliyomfanya aalikwe kwenye
mafunzo ya uraghbishi ni uwezo wake wa kuhoji mambo mbalimbali pasipo kukata
tamaa kama anavyosema mwenyewe:
“Mimi ni mtu wa kuhoji vitu na si mtu
wa kuridhika ama kukaa kimya n’napoona kuna jambo sijalielewa. Kwa kweli yale
mafunzo yalinifanya kujiona mtu tofauti sana nikijilinganisha na nilivyokuwa
awali. Nilijihisi tayari nimekuwa mtaalamu wa masuala ya uwajibikaji na utawala
bora.”
Kwa kuwa wao ni wakulima, walianza uraghbishi
wao kwa kutaka kujua nini kinaendelea kuhusu bei ya pamba. mchungaji Machibya anaeleza
ilivyokuwa:
“Kule tulifundishwa jinsi ya kuuliza
maswali. Na cha kwanza tulichotaka kujua ni kwa nini bei ya zao letu la pamba
imeshuka sana. Hili tuliliuliza sisi sote, mimi na waraghbishi wengine.”
Hawakuishia hapo tu bali wakaanza pia kufuatilia
mapato na matumizi ya fedha za kijiji toka kwa viongozi wao. Walifanya hivyo
kwa kuwatembelea ofisini na kuomba kupatiwa taarifa hizo na pia walitaka
kufanyika mikutano ya hadhara. Baada ya harakati hizo kushika kasi, iliwabidi
waongeze watu wengine zaidi kwa kuwatembelea majumbani kwao na kuwaraghbisha.
“Mchungaji aliomba kunitembelea
nyumbani na alipofika alinipatia elimu. Kimsingi, alitaka nijitambue kwa kujua
wajibu na haki zangu. Alinitaka nisiogope kuuliza maswali kwenye mikutano kwa
kuwa tuna uhuru wa kufanya hivyo. Nikajua kuwa nina wajibu kuuliza na kujua mapato
ya fedha za kijiji na na matumizi yake kuwa hiyo ni haki yangu,” anaeleza Bw. Daudi
Denis toka kijiji cha Pandagichiza.
Kufanikisha haya yote kumewajengea
uaminifu mkubwa sana waraghbishi na baadhi yao wamekuwa wakishirikishwa katika
vikao muhimu vya maendeleo na serikali yao ya kijiji. Baadhi yao wametokea
kuaminika zaidi na jamii kiasi cha kuombwa wagombee nyadhifa mbalimbali za
uongozi wa serikali na ndani ya vyama vya siasa kama ilivyokuwa kwa mchungaji
Machibya.
Hivyo basi, waraghbishi wengi
wanaojihusisha na siasa wamejikuta wakinasa katika mtego huu wa migogoro ya
kimaslahi kati ya shughuli zao za uraghbishi na zile za kisiasa kwa kuchukiwa
na baadhi ya watu wanaotofautiana kimlengo wa kisiasa na kuonekana wasaliti na
watu wasiokuwa na misimamo.
Wakati mwingine wanachukiwa ikidhaniwa
kuhoji kwao mara kwa mara ni njia ya kujitafutia mtaji wa kisiasa na si
kuwatumikia wananchi na kuibua maovu kwa maslahi ya jamii nzima na kwamba uraghbishi
unawanufaisha wao binafsi na vyama vyao tu.
Uraghbishi ulimuingiza mchungaji Machibya
kwenye mgogoro mkubwa na walinzi wa jadi, Sungusungu. Katika maeneo mengi ya
Kanda ya Ziwa walinzi hawa wamekuwa na nguvu kubwa na wakati mwingine wanaweza
kutoa adhabu kali kwa yeyote anayebainika kutenda kosa.
Tofauti hiyo na Sungusungu ilisababisha
yeye na waraghbishi wengine sita kukamatwa na kutozwa faini ya shilingi laki
tano na elfu sitini (560,000/=) kwa mpigo kwa kisingizio cha kuvuruga amani
katika kijiji hicho. Hii ni kwa sababu tu walikuwa wanauliza maswali kuhusu
mapato yanayotokana na faini na michango mingine toka kwa wanakijiji.
Vitisho na maonyo ya uongozi viliwapunguza
kasi baadhi ya waraghbishi na kuingiwa hofu kiwa wangefikishwa pabaya zaidi ya
hapo. Ila mchungaji Machibya hakuishia hapo bali aliendelea na shughuli hizo
kama kawaida. Baadaye aliteuliwa kuwa katibu wa mtandao wa waraghbishi na huko
ndiko alikojizolea uaminifu na umaarufu zaidi baada ya kuanza kujihusisha na
kuhoji mambo makubwa ya kiutawala na utendaji kijijini hapo.
Hiyo ilimwongezea hamasa ya kuendelea
kuwatumikia watu kwa kuongeza juhudi katika shughuli za uraghbishaji na kufikia
hatua ya kuombwa na wananchi kugombea wadhifa kichama (siasa) na uongozi katika
serikali ya kijiji.
Na mwaka 2014 wakati wa mchakato wa
uchaguzi wa serikali za mitaa ukiendele, ndipo yeye alijikita kwa dhati kuomba
nafasi ya kugombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kufanikiwa kuteuliwa
kugombea. Akielezea ilivyokuwa, mchungaji Machibya anasema:
“Wapinzani wangu walipojua kwamba mimi
ndio nimepitishwa waliamua kujitoa katika vyama vyao na kuniunga mkono. Hii kwa
sababu hawakuona sababu ya kupingana nami kwa kuwa wanafahamu uwezo na umakini
wangu kiutendaji na kiuwajibikaji.”
Matokeo ya harakati hizo ni kwamba Mchungaji
Machibya alichaguliwa kwa kishindo kuwa mwenyekiti wa kijiji na baadaye
alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa wilaya nzima. Sanjari na nafasi mwenyekiti
wa kijiji, aliendelea pia kushika nyadhifa nyingine ikiwamo kuwa mraghbishi
kiongozi na mchungaji.
Hizi ni nyadhifa nyingi zinazoambatana
na majukumu mengi kwa mchungaji Machibya hivyo kujikuta kwenye mazingira magumu
sana ya kutumikia nyadhifa zote. Lakini pia alipata upinzani mkali sana kutoka
kwa viongozi wengine na hata wakati mwingine kushindwa kusimamia kwa pamoja
majukumu yote.
Huku ni mraghbishi na huku ni
mwenyekiti wa kijiji. Hii haikuwa changamoto ndogo kwake. Akifafanua hilo, mchungaji
Machibya anasema:
“Kwa sababu nilikuwa kiongozi wa
waragbishi ilikuwa ni kama nayajua maswali kabla ya mtihani na wenzangu
walikuwa wanashindwa kuhoji vizuri kwa kuwa mie ni kiongozi wao. Ndipo nikaamua
kujitoa uongozi na kuwa mraghbishi wa kawaida, lakini sikuishia hapo nikajivua
na majukumu ya uchungaji wa kanisa japo ni shughuli niliyoipenda sana na kuwa
mzee wa kanisa kawaida.”
Kwa haraka haraka, unaweza kusema
shughuli ya kuhoji mwenzio inafanana na kuhojiwa wewe binafsi. Mwanzoni alipata
ugumu kidogo kwa sababu kila mwananchi alikuwa anategemea mabadiliko ya haraka wakati
vitu vingine vilikuwa kimfumo zaidi. Hiyo ilimfanya achelewe kutoa majibu ya
haraka. Na ili asiangukie kwenye dimbwi la lawama, alihakikisha anakuwa muwazi kwa
wananchi na viongozi wake wa karibu katika kila jambo.
Kuna mbinu kadhaa alizotumia ikiwa ni
pamoja na kuteua viongozi wa halmashauli ya kijiji wanaoendana na falsafa yake ya
uwazi na uwajibikaji na pia aliendelea kuwatumia waragbishi wenzake katika
kuibua mambo pale alipohisi yanakwama. Mchungaji Machibya anafahamu kwamba yeye
kama kiongozi ana wajibu wa kuwa na uelewa wa mambo mbalimbali ikiwemo sheria na
sera za nchi. Kwa kuelewa hilo, alipoanza kutafuta fursa za mafunzo ya uongozi
na kukutana na mashirika mbalimbali yaliomwezesha kupata elimu.
Hakuishia hapo bali aliendelea kujenga
mizizi ya waraghbishi wengi zaidi na mpaka sasa amefanikiwa kuwajengea uwezo
wenyeviti wenzake 40 kati ya 126 wa wilaya nzima, na bado anaendelea kutafuta
maarifa mengine ili awape wenzake.
Kwa nafasi yake, anatafuta wadau na
mashirika yenye ujuzi huo ili awezeshe wenyeviti wote kupata mafunzo kwani wengi
wao wanatawala wananchi kimazoea tu. Hawana ufahamu wa namna nzuri ya kutekeleza
majukumu yao.
Kwa misingi hiyo, mchungaji Machibya ameamua
kutumia uraghbishi kama nyenzo ya kumuongezea ufanisi katika majukumu yake na
si kutengeneza uadui na waragbishi kama ilivyo kwa viongozi wengi wa vyama na
serikali. Kwa mfano huu, tunapata picha halisi ni kwa namna gani uragbishi
ukichukuliwa kwa mtazamo chanya unakuwa nyenzo muhimu ya kuongeza chachu ya
utawala bora katika serikali zetu za mitaa, kijiji na taifa kwa ujumla. Na kwa
sasa, anapambana na mambo makuu matano ikiwa ni pamoja na mradi wa maji utakaomwezesha
kukusanya kiasi cha shilingi 500,000.
Pamoja na mapato mengine yanayokusanywa
na Sungusungu pamoja na kuhamasisha kusomeshwaji kwa wingi kwa watoto wa kike.
Na tayari hatua za makusudi za kuhakikisha kwamba malengo ya kuongeza mapato na
hivyo kulipia watoto wa kike kuhudhuria shuleni zimeshachukuliwa.
Hii ikiwa ni pamoja kupunguza adhabu
kali za viboko, kuunda upya uongozi wa Sungusungu. Kwa upande wa mapato, wameweka
mikakati ya wazi ya kuhakikisha mapato yanayopatikana yanasomwa mbele ya
wananchi. Kwa upande wa shule, kila mzazi na jamii nzima imeandaliwa mikakati
ya makusudi kuwawajibisha wale wote wanaoshindwa kuwapeleka watoto wa kike. Waraghbishi
wamekuwa chachu kubwa katika uvumbuaji wa taarifa pamoja na uelimishaji pia.
Jambo la kwanza kwa kiongozi yeyote
anayetaka mafanikio katika uongozi wake ni kutanguliza maslahi ya wananchi
kwanza kabla ya maslahi binafsi au ya chama chake. Kinyume na hivyo anaweza kutia
doa hata huo uraghbishi wake. Utu wa mtu hupimwa kwa matendo yake na hata mtazamo
wa watu anaowaongoza.
Viongozi wengi wanatumia uraghbishi
kama nyenzo ya kujijengea umaarufu wakati wenyewe ni kama hulka ama tabia ya
mtu kupenda haki na mambo yakiwa yanasonga. Kwa hiyo unaweza kukuta waraghbishi
wengi sana kama matendo yako yatalenga kukomboa watu na si maslahi binafsi.
Jambo lingine ambalo alisisitiza ni
kwamba hawa viongozi wawe na utamaduni wa kutafuta maarifa na si kusubiri fursa
za kuletewa tu na wahisani. Kiongozi bora ni lazima aendane na mabadiliko ya
kila siku na si kuongoza watu kwa mazoea. Binadamu wanabadilika kila siku, hivyo
kuna umuhimu wa kuonesha tofauti kati ya kiongozi mraghbishi na wa kawaida. Hiyo
itaibua mwamko mkubwa wa viongozi wengi kuwa waraghbishi.
Kiongozi asiyejua sheria na sera za
nchi ni sawa na kipofu. Siri ya elimu na ufahamu ipo kwenye maandishi,
mafunzoni na kwenye semina elekezi kwani bila kufanya hivyo utauchukia uraghbishi.
0 comments:
Post a Comment