ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Dk Jesca Msambatavangu amesema baada ya
kufukuzwa uanachama wa chama hicho, hatma yake kisiasa inategemea majibu
atakayopewa na Mwenyezi Mungu.
Akizungumza HabariLeo nyumbani kwake
mjini Iringa jana, Dk Msambatavangu alisema; “Mungu niye atakeyenionyesha njia
siwezi kuwa na majibu ya haraka, kilichonikuta hakina tofauti na kufiwa.”
Mbali na kufananisha tukio lililomkuta na
msibwa, alisema maamuzi ya kufukuzwa uanachama yaliyofanywa na Halmashauri Kuu
ya Taifa ya CCM hakuyapokea kwa mshutuko mkubwa kwasababu alisikia taarifa hizo
zikisemwasemwa kabla ya kikao hicho.
Pamoja na kwamba hajui tuhuma iliyomfukuzisha
uanachama kwakuwa bado hajapewa rasmi barua ya kufukuzwa uanachama huo, alisema
taratibu zilizofikia maamuzi hayo zilifuatwa.
“Kwahiyo nikipewa barua rasmi ya
kufukuzwa uanachama nadhani nitakuwa na lakuongea kwasababu ndani ya barua hiyo
kutakuwa na sababu iliyopelekea maamuzi hayo dhidi yangu,” alisema.
Alisema ameanza na atajitahidi kwa kadri
ya uwezo wake na kwa mapenzi ya Mwenyenzi Mungu kuishi nje ya mfumo wa CCCM alioupenda
toka moyoni mwake na ambao alikuwa tayari kupoteza maisha yake kwa ajili yake.
Akiwa mwana CCM wa kufana na kupona, Dk
Msambatavangu alisema alitumia akili, utaalamu na nguvu zake zote, na
rasilimali vitu na fedha kuhakikisha chama hicho kinaimarika na kuaminika kwa
watanzania.
“Wananchi wa mkoa wa Iringa ni mashahidi
wazuri kwangu, kazi niliyoifanya nikiwa ndani ya chama hicho ilikuwa kubwa na
kuna wakati ilitaka kuhatarisha maisha yangu,” alisema na kutoa mfano wa jinsi
alivyonusurika wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Kalenga, mwaka 2013.
Alisema huenda yote mazuri na makubwa aliyoyafanya
akiwa ndani ya chama hicho yakasahaurika na akaomba wenye mapenzi mema juu
yake, wamuombee avuke salama jaribio alilopitia.
“Sisi wakristo tunaamini kila jibu lina
mtihani wake. Huu ni mtihani wangu, Mungu ameruhusu nipite njia hii na yeye ndiye
atakayekuwa wa mwisho kutoa hukumu sahihi juu ya hili kwasababu sikuwahi
kufikiria kama kuna siku nitafukuzwa uanachama,” alisema.
Akiwatia moyo wanaCCM wanaobaki ndani ya
chama hicho alisema; “askari mmoja akifa vitani, ni wajibu wengine wakachukua
silaha yake na kuendeleza vita hiyo.”
Kuhusu Edward Lowassa
Dk Msambatavangu alisema kabla ya
mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka 2015, yeye na wanaCCM wengine
wengi walimuunga mkono Waziri Mkuu aliyajiudhuru, Edward Lowassa.
“Tulimuunga mkono tukijua hiyo haikuwa
dhambi kwakuwa ni mwanaCCM mwenzetu na tuliamini angeweza kupokea kijiti toka
kwa Dk Jakaya Kikwete na kusukuma gurudumu la maendeleo ya Taifa mbele zaidi,”
alisema.
Alisema kama ambavyo wao waliamua
kumuunga mkono Lowassa, wapo wana CCM wengine waliwaunga mkono wagombea
wengine, na kwa mujibu wa taratibu za chama hicho na ndio sababu wengi
walijitokeza kugombea nafasi hiyo.
Alisema baada ya CCM kukamilisha mchakato
wa kumpata mgombea wao, walikuwepo waliohama chama hicho lakini yeye na wanaCCM wengine
wengi waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa walibaki na kukisaidia chama kupata
ushindi kwasababu huo ndio wajibu wao.
“Na mimi nilibaki kwasababu CCM ilikuwa
kwenye damu yangu, sio mpitaji lakini lazima nikubaliane na hali halisi damu
hiyo itakwisha kwasababu si mwana CCM tena,” alisema.
Maisha yake nje ya siasa
Kuhusumaisha yake nje ya siasa, Dk
Msambatavangu alisema ataelekeza nguvu zake kuimarisha shughuli zake za
ujasiriamali.
“Nguvu yangu kubwa sasa itakuwa huko na
kwenye shughuli za kilimo na ufugaji. Nataka nilime sana na nifuge sana mifugo
aina mbalimbali jamii ya ndege, lakini na sungura pia.”
Kuhusu michango yake kwa jamii, alisema
ataendelea kujitolea kusaidia shughuli mbalimali za kijamii kama alivyokuwa
akifanya wakati akiwa mwanachama na kiongozi wa CCM.
0 comments:
Post a Comment