Thursday, March 16, 2017

MKURUGENZI MTENDAJI WA HALMASHAURI YA SONGWE AWATOLEA UVIVU MADIWANI, MBUNGE

Elias Nawera.

Na Brandy Nelson

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mkoani  hapa,Elias Nawera ambaye ameingia mgogoro na madiwani wake, ameibuka na kutoa msimamo wake kwamba atafanya kazi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni  za utumishi wa umma na si kwa matakwa  ya wanasiasa.

Hivi karibuni  Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Songwe, Phillipo Mulugo  walidai kutoridhishwa na hawana imani na utendaji kazi wa mkurugenzi huyo kwenye kikao chao kilichoitishwa kwa dharula kwa lengo la kumjadili na kumuazimia kumfuka kazi.

Akizungumza juzi , Nawera alisema kuwa amepelekwa kwenye halmashauri hiyo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi  na siyo kumtumikia mtu mmoja mmoja kwani kufanya hivyo ni kukiuka  misingi ya utawala bora.

"Unajua baraza la madiwani ni wawakilishi wa wananchi na ni siasa, na siasa mara nyingi  ilivyo ni nani kapata nini wakati gani vipi, kimsingi ndiyo siasa, wilaya yetu ni mpya  na kuna watu wanataka kufanya kazi kwa namna  walivyokuwa wamezoea kufanya mambo yao, kitu ambacho siwezi kukubaliana nacho hata siku moja,"alisema. 

Alisema tangu  alipofika katika halmashauri hiyo Septemba mwaka jana, alikuta mazoea ya watu kama wana ufalme  kana  kwamba  Serikali haipo, hivyo yupo Songwe kufanya kazi kimfumo wa kiserikali na  siyo kumtumikia mtu mmoja mmoja ambapo  jambo hilo  limekuwa likikwaza watu.

"Mfano  kwenye  kikao cha halmashauri nililazimishwa kumpa mtu kazi kwa jina,kufanya biashara na mtumishi wa halmashauri ,nikiuke sheria ya manunuzi  kwa kusema sheria nini,vitu ambavyo sikubaliani navyo kwani kufanya hivyo nikukiuka sheria,taratibu na misingi ya utawala bora ".alisema 

Mkurugenzi  huyo alisema amekuwa akienda  vijijini kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kusikiliza kero za wananchi lakini amekuwa akizuiwa kufanya hivyo na kuambiwa abaki ofisini.

"Nimewahi kukatazwa nisiende  vijijini,mimi ninajua rais amenileta huku nitumikie watu na  Ilani yenyewe  ya chama cha mapinduzi inasema lazima  twende chini  tufanye kazi  na watu, kwa hiyo ukiniambia kitu tofauti na hicho miongozo, sheria kanuni  na  taratibu mimi sitokusikiliza kwa sababu nitataka kutumikia  wananchi na kumsikiliza yule aliyenileta.'alisema  

Alisema  hata Mkuu wa Mkoa wa Songwe,   Chiku Galawa mara nyingi amekuwa akiwaagiza watendaji kutoka ofisini na kwenda vijijini kwa wananchi, kwani pia kuna watumishi ambao wapo huko na wanahitaji huduma lakini hawana uwezo wa kufika wilayani hivyo hutumia fursa hiyo kuwasikiliza mahitaji yao.

Aidha alisema ameshangazwa na utaratibu wa  Mkurugenzi kutakiwa kutoa taarifa katika ofisi ya mbunge au kwa katibu wa mbunge  anapotaka kwenda vijijini kufanya kazi.

"Ukisimamia kwenye  msimamo   wa kufuata misingi ya sheria kanuni na taratibu za utumishi wa umma hapo  ndipo unaonekana haufai,unakiburi au huna adabu"alisema 

Akizungumzia mgogoro huo, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Galawa alisema ni kitu cha kawaida katika utendaji kazi kwani hata katika familia hali hiyo hutokea na kwamba amewataka watumishi  wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa utulivu na kusahau yaliyopita.

Chanzo Gazeti la Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More