Wednesday, March 1, 2017

WAZIRI DK.CHARLES TIZEBA KUFUNGUA KONGAMANO LA WADAU WA KILIMO JIJINI DAR ES SALAAM KESHO

Enles Mbegalo

WAZIRI wa Kilimo ,Chakula,Mifugo na Uvuvi Dk. Charles Tizeba (pichani), anatarajia kufungua kongamano la siku  tatu la wadau wa sera za kilimo kesho jijini Dar es Salaam.

Aidha, kongamano hilo litahudhuriwa na wadau zaidi ya 200 kutoka nchi mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa  Kampuni ya Agricultural Non State Actors Forum (ANSAF), Audax Rukonge, alisema serikali imekusudia kuweka kipaumbele kwenye viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo.

Kongamano hilo litalenga kuongeza uelewa miongoni mwa watunga sera kuhusu mchango wa kilimo katika kuhamasisha ukuaji wa viwanda Tanzani.

“Wadau  watajadili kupata tafsiri halisi ya sekta ya uchakataji mazao ya kilimo katika muktadha wa mageuzi ya viwanda Tanzania,”alisema

Rukonge alisema kongamano hilo limedhaminiwa na USAID, Benki ya Dunia,ANSAF,JICA na wadau wengine ambao wamesaidia kuleta watalamu wakiwamo wakulima, watafiti,wafanyabiashara na watunga sera.

Mratibu wa Jukwaa la Sera ya Kilimo na Mchumi mwandamizi Wizara ya Kilimo, Sophia Mlote alisema kongamano hilo la tatu litajadili maendeleo ya kilimo nchini ikiwamo kujadili namna ya kutetea sera,sheria,kanuni.

Pia alisema kongamano hilo litajikita katika kujadili juu ya mpango wa kilimo cha mihogo,mikunde, samaki, mazao, usafirishaji pamoja na vifungashio kwa kuwa wazalishaji wengi hawana vifungashio.


0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More