WIZARA ya Maliasili na Utalii ipo katika
mchakato wa kutunga kanuni zitakazowazuia wafanyakazi wa hoteli wasio na vyeti
vinavyotambulika na serikali kutoa huduma katika sekta ya utalii.
Kanuni hiyo ambayo msingi wake unalenga
kuendeleza na kuboresha huduma katika ya sekta hiyo, utahusisha pia kuvibana
vyuo vya hoteli na utalii ili vitoe mafunzo yanayokidhi viwango.
“Baada ya kutungwa na kuanza kutumika kwa
kanuni hizo, waajiri katika sekta hiyo watalazimika kuwaajiri wafanyakazi wenye
sifa ambao wamesajiliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii,” alisema Mkurugenzi
Msaidizi wa Idara ya Utalii, Paskas Mwiru.
Aliyasema
hayo jana kwenye mafunzo ya siku tatu ya ukarimu na utalii yanayoshirikisha
watoa huduma zaidi ya 100 wanaofanya biashara inayohudumia watalii mkoani
Iringa.
Mafunzo hayo yanayotolewa na wizara hiyo
kwa kushirikiana na Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini
mwa Tanzania (SPANEST), yanafanyika kwa siku tatu mjini Iringa.
Mwiru alisema mafunzo hayo ya muda mfupi yameanza
kutolewa katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini baada ya serikali kubaini baadhi
ya vyuo vinavyotoa mafunzo hayo; kuyatoa chini ya viwango.
“Pamoja na changamoto hiyo, baadhi ya
waajiri wamekuwa wakiajiri wafanyakazi katika sekta hiyo kwa misingi ya udugu
na urafiki bila kuzingatia vigezo vya elimu na ujuzi ili kukwepa gharama,”
alisema.
Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole
Meing’atakia alisema changamoto hizo zimesababisha huduma duni katika maeneo ya
mapokezi, chakula, vinywaji na malazi, na hivyo kuleta malalamiko makubwa sana
kwa wageni.
Kwa kupitia mafunzo hayo mafupi
Meing’ataki alisema; “ni mtarajio yetu maarifa watakayopata washiriki hawa
yatawawezesha kutambua wajibu wao ili wageni wanaopata wapate huduma
wanazotarajia.”
“Sekta ya utalii ina changamoto nyingi,
lakini eneo hili la huduma ni muhimu kwasababu linaweza kusaidia kumrudisha
mgeni tena na tena na kumfanya awe balozi kwa watu wengine,” alisema.
Kwa wawekezaji katika sekta hiyo, haitoshi
tu kuwa na hoteli kubwa kama itakuwa haina huduma bora kwa wageni wake.
Akifungua mafunzo hayo jana, Kaimu Katibu
Tawala wa Mkoa wa Iringa, Fikira Kissimba alisema licha ya ukanda wa nyanda za
juu kusini kuwa na vivutio vingi vya utalii, idadi ya watalii wanaovitembelea
ni ndogo na moja ya sababu yake ni uduni wa huduma katika sekta hiyo ya utalii.
Akishukuru wizara na SPANEST kwa kutoa
mafunzo hayo, Kissimba alisema yatakuwa chachu katika kukuza na kuendeleza
utalii kusini mwa Tanzania kwa kutoa huduma bora kwa watalii.
Aliwataka wahudumu katika sekta hiyo
waache tabia ya uvivu, kufanyakazi kwa mazoea na wawe wepesi kujifunza ili
kuboresha huduma zao.
0 comments:
Post a Comment