Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mh. Jamhuri William ametoa muda wa siku 15 kwa watu binafsi na vikundi vilivyokopeshwa kupitia Saccos pamoja na Fedha za Halmashauri Wilayani humo, wawe wamerejesha mikopo yao mara moja na kuonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa wakopaji pamoja na wadhamini wao endapo watakaidi kutekeleza agizo hilo.
Taarifa ya kitengo cha habari na mawasiliano cha halmashauri ya wilaya ya Mufindi imefafanua kuwa, mkuu wa wilaya ametoa agizo hilo baada ya kubaini uwepo wa vikundi vingi pamoja na watu binafsi waliokopa kwenye mfuko wa Halmashauri na Saccos pasipo kurejesha licha ya muda wa kukamilisha marejesho ya mikopo hiyo kupita.
“Natoa fursa kwa yeyote ambaye alikopa aidha kupitia mfuko wa wanawake na vijana wa halmashauri au saccos, awe amerejesha kwa hiali ifikapo tarehe 15 ya mwezi ya mwezi wa 9, baada ya hapo haitakuwa tena suala la mkopo ilikuwa suala la uhalifu na uwizi”
Aidha, mkuu huyo wa Wilaya amesema kunahaja ya kuvitathimini upya vigezo vya utoaji mikopo kwani baadhi ya viongozi wa Saccoss wamewakopesha watu ambao hawana udhibiti nao hivyo, pesa nyingi ziko mikononi mwa watu jambo ambalo linawanyima fursa ya kukopa wananchi wengine.
Katika hatua nyingine, Mh. Jamhuri William amewataka wananchi kuzingatia na kudumisha amani iliyopo nchini huku akipiga marufuku vyama au kikundi chochote Wilayani Mufindi kujihusisha na maandamano yaliyopangwa kufanyika September mosi.
0 comments:
Post a Comment