MFANYABIASHARA
maarufu, Mustapha Jaffer Sabodo ametangaza kutoa dola za Marekani
bilioni 5 (Sh trilioni 10) kwa ajili ya kuwekeza mkoani Dodoma, ikiwa ni
njia ya kumuunga mkono Rais John Magufuli kuhamisha makao makuu ya
serikali kwenda mkoani humo.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Sabodo alisema atawekeza kiasi hicho cha fedha,
iwapo serikali yote itahamia mkoani humo, itakuwa ametimiza ndoto ya
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambaye alitamani kuona mkoa huo
unakuwa makao makuu ya nchi.
Alisema
alichofanya Rais Magufuli, kimewashinda marais wengine waliomtangulia,
hivyo yeye kama mfanyabiashara na mtu mwenye mapenzi makubwa kwa nchi
yake, lazima aunge mkono hatua hiyo ya Serikali kuhamia Dodoma ambayo
aliita ‘Azimio la Dodoma’.
“Niliposikia
anatangaza kwenye televisheni ya taifa kwamba Serikali itahamia Dodoma,
ilikuwa mara yangu ya kwanza baada ya miaka mingi kupita, nilitabasamu
moyoni, jambo ambalo lilinitokea miaka 10 ya kwanza ya uongozi wa
Mwalimu Julius Nyerere.
“Leo nimesikia kutoka kwako nimeona ile roho ya Nyerere imezaliwa tena.
“Kwa
hiyo natangaza kuunga mkono Azimo la Dodoma kwa kuwekeza dola za
Marekani bilioni 5, ambazo zitatumika kwa ajili ya uwekezaji mkubwa
katika huduma mbalimbali za jamii mkoani humo,” alisema Sabodo.
Sabodo
alisema atatoa fedha hizo ili zitumike kuwekeza kwenye viwanda kama vya
mvinyo, viwanda vya kusindika mihogo na viwanda vingine ambavyo
vitahitajika katika mkoa huo.
Alisema
kuwepo kwa huduma hizo mkoani Dodoma, kutasaidia kuufanya mji huo
kukidhi matakwa ya watumishi wa umma watakaohamia huko.
Mfanyabiashara
huyo aliongeza kuwa atafanya uwekezaji mkubwa huo kwa sababu lengo lake
ni kuona mji wa Dodoma, unaungana na miji ya jirani kama Mpwapwa,
Kondoa na Manyoni ili kutoa fursa ya kupanua huduma mbalimbali katika
makao makuu hayo ya nchi.
Sabodo
alisema kwamba juhudi zake za kuwekeza katika huduma za jamii kama
shule, pia ataziendeleza katika mkoa huo kwa kuhakikisha kwamba
zinajengwa shule kadhaa za kisasa, ambazo zitamudu mahitaji ya watu wa
eneo hilo.
Kwa
upande wa huduma ya afya, Sabodo alisema atatumia umaarufu wake
kuwashawishi wamiliki wa Hospitali ya kimataifa ya Apollo ya India ili
waje nchini wakashirikiane naye kujenga hospitali ya kisasa, ambayo
itakuwa inatoa huduma za kisasa mkoani humo.
“Mnaifahamu
hospitali ya Apollo ni wawekezaji wakubwa katika huduma za afya, kwa
kusukumwa na hatua hii ya Rais nitaongea nao tushirikiane katika kujenga
huduma za jamii katika mji huo,” alisema Sabodo.
Pia
alisema atawashawishi wawekezaji wengine kutoka nchi za India,
Singapore na kwingineko kuja kuwekeza katika mji huo wa Dodoma katika
sekta ya viwanda, kuhakikisha kwamba azma ya Rais Magufuli ya kujenga
uchumi wa viwanda inatimia.
Sabodo
ambaye alisema wazi kuwa utendaji wa Rais Magufuli, umemvutia kutokana
na hatua yake ya kupiga vita rushwa, alitangaza kuwa kuanzia sasa
hatatoa tena msaada kwa vyama vya upinzani kama ambavyo amefanya miaka
ya nyuma kama njia ya kuimarisha demokrasia nchini.
“Huko
nyuma nilikuwa nawapa Chadema fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na
kuimarisha demokrasia, sasa natangaza tena kwamba sitawapa tena fedha,
niwape za nini wakati Rais aliyeko madarakani anafanya kazi ambayo ndio
nilikuwa naipigania?" alihoji Sabodo.
Sabodo
ni mfanyabiashara wa kitanzania mwenye asili ya Kihindi ambaye
alizaliwa mkoani Lindi. Katika maisha yake amekuwa anafanya biashara
katika nchi za Kenya, Ufaransa, India, Sudan na Zimbabwe.
Pamoja
na biashara zake, Sabodo amekuwa anajihusisha kuchangia katika miradi
ya maendeleo ya huduma za jamii, uimarishaji wa demokrasia nchini na pia
alishiriki kutunisha mfuko wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha
bahati nasibu.
1 comments:
Tanzania Kwanza,Ni hatua nzuri hiyo
Post a Comment