MWANASHERIA
Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu
amesema licha ya viongozi wa chama hicho kutishwa, kukamatwa na kuhojiwa
na Jeshi la Polisi, bado msimamo wao kuhusu operesheni Ukuta
itakayofanyika Septemba Mosi mwaka huu uko pale pale.
Chama hicho kinatarajiwa kufanya operesheni mpya iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta).
Operesheni
hiyo inatarajiwa kuwa itakwenda sambamba na uzinduzi wa mikutano ya
hadhara nchi nzima, ambayo itafanyika Septemba Mosi, mwaka huu.
Hatua
hiyo imefikiwa na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi kwa
siku nne mfululizo wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kutoa maazimio
matatu ambayo yatatekelezwa na chama hicho.
Pamoja
na mambo mengine, chama hicho kimesema lengo la operesheni hiyo ni
kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini, kiliyodai
kuwa yanafanywa na Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam baada ya kuhojiwa na
kuachiwa kwa dhamana Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Mwanasheria
Lissu alisema msimamo wao uko palepale na hakuna kilichobadilika.
“Wamemuhoji
kwa taarifa aliyoitoa mbele ya waandishi wa habari juu ya msimamo wa
chama wa kufanya mkutano nchi nzima. Tatizo jeshi letu wakisikia
maandamano, mkutano au mtu anamsema Magufuli basi anatuhumiwa kwa
uchochezi, wametumia muda mrefu kumuhoji lakini mwisho wamemwachia kwa
dhamana na amewahi ‘Airport’ ili aende kuhudhuria mazishi ya kamanda
wetu Senga (Joseph) na watamwita watakapomwihitaji tena,” alisema Lissu.
Alisema
pamoja na hayo bado msimamo wa chama hicho kufanya mikutano waliyoiita
Operesheni Ukuta ipo pale pale ifikapo Septemba Mosi, mwaka huu.
“Nafikiri
ni muhimu sana huko tunapoenda kuzungumza na wenzetu hii kitu inaitwa
uchochezi ni nini? Tunashitakiwa kwa sheria ya magazeti ya mwaka 1976
ambayo waliingiza vifungu vya uchochezi mwaka 1978 lengo lao kuu ni
kuwafunga watu midomo na ilitungwa wakati wa mfumo wa chama kimoja.
“Hata
hivyo Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ndiye wa kwanza
kushtakiwa kwa uchochezi pamoja na mwandishi Robert Makenge na mwenzao
Rashid Bagedae, kwa msingi huo sisi tunafuata nyayo zake,” alisema.
Lissu
ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema kuitwa
mchochezi, ni jambo la ufahari kupinga udikteta kama alivyokuwa Mwalimu
Nyerere.
“Nasema
hivyo kwa sababu Mwalimu Nyerere ndiye wa kwanza kuitwa mchochezi, ni
kitendo cha kufunga watu midomo ili washindwe kuwaita watu wajinga pale
wanapofanya ujinga.
“Tume
ya Jaji Nyalali mwaka 1992 wakati mfumo wa vyama vingi unatambulishwa
na kuanza nchini ilipendekezwa sheria hii ifutwe kwa sababu haiendani na
mfumo uliopo lakini hakuna kilichofanyika,” alisema.
Mwanasheria
huyo ambaye naye amefunguliwa kesi ya uchochezi katika Mahakama ya
Kisutu jijini Dar, aliwataka wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi
Agosti 2, mwaka huu mahakamani hapo.
“Dawa yao si majaji bali umma… umma ufurike, tutawashinda hawa watu makesi yenyewe ni haya ambayo hayana kichwa wala miguu,” alisema na kushangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Mbowe
alifika kituoni hapo akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa
Chadema akiwamo Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa ambaye hata hivyo
alizuiwa kuingia katika chumba cha mahojiano.
Askari
waliokuwa kwa wingi katika eneo hilo, walisikika wakisema kuwa
anayepaswa kuingia ndani ni Mbowe, Mwanasheria Tundu Lissu na Wakili wa
Chadema, John Mallya.
Lowassa,
wafuasi wa Chadema na waandishi wa habari walilazimika kubaki nje huku
askari wakiimarisha ulinzi wakiwa wamebeba bunduki zao huku magari yenye
maji ya kuwasha yakiwa yameegeshwa pembeni.
Wakati
chama hicho kikijiandaa kutekeleza Operesheni Ukuta Septemba Mosi,
tayari Rais Magufuli amezuia operesheni hiyo na kuwaonya wale wote
watakaokaidi agizo lake na kuamua kuandamana.
0 comments:
Post a Comment