Wednesday, August 10, 2016

Matabibu Mbadala waomba kibali kuishtaki Serikali kuwafutia usajili

MATABIBU wanne wa Tiba Asilia na Mbadala akiwemo mmiliki wa Kliniki ya Sure Herbal, Simon Rusigwa wamewasilisha maombi ya kuomba ruhusa ya kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa kufutiwa leseni za kutoa huduma za kitabibu.

Wamewasilisha maombi hayo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mbali na Rusigwa, matabibu wengine waliowasilisha maombi hayo kupitia kwa Wakili Dk Lucas Kamanija, ni Abdallah Mandai wa kliniki ya Mandai Herbalist, Fadhili Kabujanja wa Fadhaget Sanitarium na John Lupimo wa Lupimo Sanitarium.

Maombi hayo yalitakiwa kusikilizwa jana mbele ya Jaji Ama–Isario Munisi wa mahakama hiyo, hata hivyo kabla ya kuanza kusikilizwa, Serikali iliwasilisha pingamizi la awali ikidai kuwa maombi hayo hayakufuata misingi ya kisheria.

Katika pingamizi hilo serikali inadai kuwa maombi hayo yana kasoro kwa kuwa waombaji hawajapita njia zote zinazotakiwa wazifuate ndipo waende mahakamani pia wanadai maombi hayana miguu ya kusimamia kwa kuwa hati ya viapo vya walalamikaji vina upungufu ya kisheria.

Baada ya kuwasilishwa kwa pingamizi, Jaji Munisi aliahirisha shauri hilo hadi kesho saa 8 mchana, ambapo alizitaka pande zote zinazohusika ziwepo ili kusikiliza pingamizi hilo.

Katika maombi yao, matatibu hao wanadai, wameamua kupeleka maombi hayo mahakamani, kwa kuwa wanaamini walifutiwa leseni bila kufuata taratibu za kisheria.

Wamedai wanaamini uamuzi uliochukuliwa umetolewa bila kupitia Kamati ya Maadili ya Baraza la Tiba Asilia na Mbadala, huku wakidai kuwa huo si uamuzi bali zilikuwa tuhuma mpya, lakini hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.

0 comments:

Post a Comment

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More